Thursday, December 1, 2016

"Yoyote ambae anafikra ya kwamba Uislam ni dini ambayo haina huruma huyo atakuwa hajautambua Uislam",-Sheikh Jalala.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
MAADHIMISHO KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) MWEZI 28, SAFAR 1438.

Napenda kuanza na mazungumzo yangu katika Qur’an Mungu ansema “Hatujakutuma ewe Muhammad (s.a.w.w) ila ni huruma kwa viumbe wote” siku hii ya leo ya mwezi 28,mfungo tano kwa kalenda ya Hijiria ndio siku ambayo Kiongozi wa watu wote duniani, kiongozi wa Waislam Mtume  wetu Muhammad (s.a.w.w) ndio ameaga dunia.

Weusi huu mnaouona, matembezi haya ya amani mnayoyaona yote ni kwasababu ya kukumbuka kifo cha mtukufu na mtakatifu Mtume Muhammad (s.a.w.w), Lakini lakujiuliza kubwa ni kwanini mtu huyu tumkumbuke katika kifo chake, zaidi ya miaka 1400 iliyopita. 

Sababu kubwa ya kukumbuka kifo cha Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuna sababu nyingi mmno, lakini niseme sababu mbili tatu kwa harakaharaka, Sababu ya kwanza kama anavyosema Mwenyezimungu katika Qur’an kwamba “Wewe tumekutuma ukawe ni huruma kwa watu wote” sio huruma kwa Waislam, 

Sasa unapomuangalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) wakati bado yupo hai, akiwa yuko katika mji wa makka na baada ya kuwa madina, tulimpata mtume alikuwa na huruma kwa watu wote, mtume alikuwa huruma kwa wasiokuwa waislam, mtume alikuwa na huruma kwa waislam, mtume alikuwa huruma kwa wtu waliokuwa wanaabudu masanamu, kwa watu waliokuwa wanaabudu lata, wanaabudu manata na wanaabudu hubal,
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habari katika Matembezi ya Amani ya Kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) Kigogo Round About, Leo Jijini Dar es salaam.Ambayo yalianzia Ilala Boma hai Uwanja wa Pipo Kigogo.

 hawa walikuwa ni waungu wakiabudiwa na warabu, lakini mtume aliishi vizuri na alikuwa ni huruma kwa watu hao, mpaka amana za watu hao aliziweka katika  nyumba yake,
Mtume alipokuwepo maka na madina vilevule alikuwa na huruma kwa Ahlulkitab / Wakristo, yaani alikuwa ni huruma kwa Wakristo, alikuwa na huruma kwa mayahudi na alikuwa ni huruma kwa watu wenye dini zote.

Naamimi ya kwamba huruma hii aliyokuwa nayo Mtume Muhammad (s.a.w.w) kabla hajaondoka duniani, naamini ya kwamba Watanzania na walimwengu huruma hii wanaihitajia.
Leo hii tunapotembea matembezi haya ya amani kwa ajili ya kukumbuka Mtume Muhammad (s.a.w.w) kifo chake, kubwa la kulienzi ni hili la Huruma ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) inahitajika na ni muhimu, 

Naamini yakwamba Watanzania wote wanahitajia huruma aliyokuwa nayo mtume, huruma ambayo haikumfanya Mtume asiwapende wasiokuwa waislam.

Huruma ambayo ilimfanya mtume akae meza moja na Wakristo katika ardhi ya madina, Huruma ambayo ilimfanya Mtume akae meza moja na Mayahudi, huruma ambayo ilimfanya Mtume akae na Wakristo / Ahlulkitabu.

Naamini yakwamba leo hii Waislam watanzania Masheikh na Maimam na Maustadhi wanayonafazi kubwa yakumuenzi Mtume katika kukaa kwao na Wachungaji, wao na Maaskofu, wao na Mapari, wao na wenzi wao ambao wanatofautiana nao kidini, Naamini ya kwamba Matembezi haya yawe ni chachu yakuwafanya watanzania wote waiige huruma ya Mtume,

 ambayo huruma hiyo ilikuwa haimbagui mtu, huruma hii leo hii inahitajika mahala pakubwa.Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa ni huruma kwa watu wote kwanini kwasababu alikuwa na huruma na watu.

Jambo la pili Mtume ambae tunamkumbuka leo hii, ni mtume alieng’ang’ania na alieenzi Umoja kabla ya mtume hajaondoka makka alitengeneza umoja kati ya maswahaba wake, na alipoondoka makka kwenda madina vile vile akatengeneza umoja kati ya wakazi wa madina (Answar) na kati ya watu waliotoka Makka(Muhajirun).

Akatengeneza Umoja kati ya makabila mawili yaliyokuwa yanavutana kabila la Ausi na Azraj, akatengeneza umoja wa Kidini ndani ya ardhi ya madina,naamimi ya kwamba leo hii, uwepo wa umoja wa Kidini ndani ya ardhi ya Tanzania,kipindi hiki ambacho huruma imekosekana , 

kipindi ambaho kuvumiliana kumekosekana, naamimi ya kwamba mafunzo haya Mtume Muhammad (s.a.w.w) yanahitajika leo hii kwa Watanzania na watu wote bila ya kuwabagua waislam wala wakristo wote wanahitajia umoja huu, wanahitajia kuishi huku kwa pamoja ameyoyafunza Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Nimalizie kwa kusema yoyote ambae anafikra ya kwamba Uislam ni dini ambayo haina huruma huyo atakuwa hajautambua  Uislam, yoyote ambae anafikiria ya kwamba Mtume alikuwa ni mtu wa Misimamo ya kutisha ambayo hawezi kukaa na watu hayo hajamtambua Mtume. 

“Kwasababu ya huruma uliyokuwa nayo ewe Muhammad (s.a.w.w) watu wote wameweza kukukubali, umeweza kukaa na Wakristo, umeweza kukaa na Mayahudi,umeweza kukaa na Mapagani na umeweza kukaa na watu wa aina zote”

Jambo la Mwisho Mtume Muhammad (s.a.w.w) kama alivyoenzi Umoja, ulienzi utulivu, alienzi maelewano na alienzi amani, na ninaamini yakwamba Tanzania leo hii inayohaja kubwa yakuenzi Utulivu, yakuenzi Amani, yakuenzi Mshikamano watu kukaa pamoja, tofauti zetu za kifikra na za kimtazamo zisitufanye kutokuwa wamoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki wanadini wote walioko Tanzania, wabariki Viongozi wa Dini wahubiri Upendo, Maelewano, Mshikamano pamoja na Amani katika nchi hii,Vilevile Viongozi wetu na Serikali ambayo inatusimamia katika mambo yetu. 

Imetolewa na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
30-11-2016,Jumatano.