Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akiongea na Waandishi wa Habaei jana Masjid Ghadir Kigogo Post Dar es salaam. |
Napenda kuanza Mazungumzo yangu kwa kuanza maneno
kutoka katika Quran suratul Kauthar, Mwenyezimungu aliposema “Hakika sisi
tumekupa kheri nyingi” kheri nyingi hizi Wasomi wa Kiislam wametafsiri kwamba makusudiwa
hapa ya kheri nyingi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupewa Binti anaeitwa Fatuma
(a.s) akijylikana maarufu kwa Jina la Fatuma Zahra (a.s) .
Siku hii ya leo tunakumbuka kuzaliwa kwa binti yake
Mtume Muhammad (s.a.w.w), Bi Fatuma (a.s) alizaliwa tarehe 20 Rabil Akhiral
mwaka wa 615 AD, Siku ya kuzaliwa Mama huyu ni siku kubwa ambayo sisi Waislamu
tunapenda kumuenzi huyu mwanamke na kuieleza jamii na Walimwengu vipi Waislamu
wanamuangaliwa MWANAMKE, vipi waislamu wanamtazama Mwanamke.
Mtakubaliana na mimi kabla ya Uislamu mwanamke
kwenye makabila tofauti na kwenye dini tofauti alikuwa hana dhamani, bali
tunakumbuka baadhi baadhi ya dini zilikuwa hazimruhusu mwanamke hata kuingia
msikitini kuswali , hata kuingia kwenye nyumba ya Ibada iwe ni Sinagogi au iwe
ni kanisa au iwe ni Msikiti.
Lakini Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuja kusomesha
tofauti akaja Mtume akamuonyesha Mwanamke kwamba ni Mwanadamu kama mwanadamu
mwingine, Mtume akamuonyesha Mwanamke
kwamba kama vile Mwanaume kuwa na haki vile vile mwanamke ana haki,
Mtume akaonyesha usawa kati ya Mwanaume na Mwanamke “Tumewaumbeni kwa Mwanaume
na Mwanamke”.
Kwahivyo Mtume akaonyesha usawa kati ya Mwanamke na
Mwanaume kwamba hakuna tofauti kwa haki zinazowastahiki kutoka kwa
Mwenyezimungu (swt) si hilo tu Uislamu kupitia Mtume Muhammad (s.a.w.w) na
katika Quran tukufu, kwamba la si kama watu wanavyomtafsiri Mwanamke, Mwanamke
ni Mwanadamu aliekamilika kama alivyokuwa Mwanaume amekamilika.
Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Kikao hicho cha Kumzungumzia Nafasi ya Mwanamke katika Uislamu katika jamii kwa mtazamo wa Kiislamu. |
Uislamu ukatupa mafunzo makubwa zaidi na kutuonyesha
Mwanamke ndie anaetengeneza Umma, mwanamke ndie anaetengeza watu, ndie
alietengeza wanaume waliofanya mabadiliko, maeneno mashuhuri “Jambo lolote
kubwa unaloliona ujue nyuma kuna mwanamke, hivi ndivyo mwanamke uislamu
unavyomuangalia.
Kila jambo kubwa unaloliona nyuma yake yupo
Mwanamke, Nabii Mussa (a.s) mmoja katika mitume wa Mungu, ni kwanini aliweza
kumshinda Firauna au Farao, ni kwasababu nyuma yake kulikuwa na Mwanamke ambae
ni Mama Asia (a.s), Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwanini aliweza kuueneza Uislamu,
kwasababu nyuma yake kulikuwa na Mwanamke amabe ni Mama Khadiha (a.s).
Kwahivyo unapoangalia watu wakubwa duniani nyuma
palikuwa na Mwanamke, Mwanamke ndie alieleta mabadiliko , lakini sio hivyo tu,
unatambua wewe ili uwe Raisi ili kuwa waziri,ili uwe mtu wa Kitaifa au
Kimataifa inahitaji malezi kwanza, Msimamizi wa Malezi hakuna isipokuwa ni Mama
amabe ni Mwanamke tu.
Kwahivyo Uislamu unamuangaliwa Mwanamke ndie
anaetengeneza watu, ndie anaetengeneza wanaume, ndie anaetengeza ushindi, na
tumemuona Mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyohamiliana kwake na watu, katika
kuhamiliana na wanawake na akionyesha mfano wa ajabu, tunamuona mtume Muhammad
(s.a.w.w) akifanya mbele ya huyu Fatuma (a.s)
amabae tunakumbuka leo kuzaliwa kwake.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) huyu Bint Fatuma (a.s)
anaingia nyumbani kwake, anapoingia Fatuma (a.s) Mtume Muhammad (s.a.w.w)
anamsimamia bint Fatuma (a.s), na sio kumsimamia tu, bali anamsimamia pamoja na
kukamata mkono wake na kuubusu alafu anamkalisha karibu yake, jambo ambalo
kipindi hicho katika jamii ile ilikuwa ni jambo halipo.
Nukta Maranyingi hujadiliwa Sana duniani kwamba
Uislamu mbona unaaina fulani ya dhulma kwa mwanamke, tunasema la au Hapana,Bali
katika dini ambazo zimempa haki mwanamke
hakuna kama vile Dini ya Uislamu, na kama zipo bali ninasema Uislamu ni dini ya
kwanza kwa taratibu nzuri, na kwa mbinu nzuri na kwa namna nzuri.
Kwa mfano haki ya Kumiliki, Je, Mwanamke anaruhusiwa
kumiliki ndani ya Uislamu? Uislamu kupitia Quran inajibu wazi wazi kama vile
mwanaume anavyoweza kumiliki mali yake pia Mwanamke anaouwezo wa kumiliki mali
yake, kwahivyo haki ya kumiliki ni haki ya Mwanaume na Mwanamke ndani ya
Uislamu.
Uislamu haukufanya anaemiliki ni Mwanaume tu,
hapana,anaemiliki ni Mume anaemiliki ni Mke. Wote wawili wanayohaki ya
kumiliki.
Haki ya Uongozi, Je mwanamke katika uislam anayohaki
ya kuwa Kiongozi? Uislamu unasema ndio. Mwanamke anayohaki na nafasi ya kuwa
Kiongozi kuanzia ngazi ya Uwakilishi, ngazi ya wizara, ngazi ya usimamizi wa
mambo katika ngazi hizi zote mwanamke anaouwezo wa kusimamia na mwanamke
anaouwezo wa kuongoza.
Haki ya Kufanya Kazi, Mwanamke katika dini ya
Uislamu anayohaki ya kufanya kazi awe ni Bosi, iwe ya kuajiri, iwe ni kuajiriwa
haki hiyo anayo katika uislamu kama alivyokuwa nayo Mwanaume.Bila shaka Uislamu
umeweka utaratibu ni nguo gani anatakiwa kuvaa mwanamke, bila shaka ni kwa
maslahi na heshima ya mwanamke. Kwasababu Uislamu unamuangalia Mwanamke kwamba
ni mtu mtakatifu, Uislamu unamuangalia Mwanamke ni mtu anaetengeneza watu.
Kwahivyo Mwanamke hazuiliwi kufanya kazi yoyote
ambayo ipo ndani ya misingi ya Uislamu na ambayo ipo ndani ya Misingi ya
Sheria.
Na katika jambo linguine dunia inajiuliza , je
mwanamke anayohaki ya kuendesha gari? Ndio mwanamke anayohaki ya kuendesha
gari, mwanamke anayo haki kama aliyonayo haki Mwanaume, haki ya kuendesha gari,
iwe gari ya kuajiliwa, gari binafsi muda wa kuwa hajatoka katika mipaka ya
Kiislamu.
Haki ya kusimama mbele ya Wanaume, Mwanamke katika
Uislamu anayo haki kutoa Mada mbalimbali, anayohaki ya kuzungumza mbele ya watu
wa aina yoyote muda wa kuwa hilo halivunji taratibu na misingi ya Dini ya
Uislamu, tumeona wanawake katika Uislamu waliosimama mbele za watu wakawa
wahubiri, wakasema, Bi Fatma (a.s) ninaemzungumza leo hii, amabe tunakumbuka
kuzaliwa kwake, tunamkuta katika historia vipi ametoka nyumbani kwake ameenda
mpaka msikitini kutoa Khutba , kuongea na watu,
Si hivyo tu tunamuona Bi FATMA (a.s) akizungumza kwa
watu aina tofauti waliokuwa wanamzunguka, sio yeye tu wapo wanawake wengi kama
Bi Zaynab (a.s), Bint wa Sayyidina Ali (a.s) tunamkuta nay eye anatoa Khutba
mbele za Wafalme, mbele za watawala, na mbele za watu toafauti.
Haki ya kurith, je mwanamke anaweza kurith? Ni katika
maneno yanayotumika kuuzungumza vipaya Uislamu. Naema hapana, Uislamu umemrithisha
mwanamke, mwanamke anayohaki ya kuruthi katika namna mbili, upande wa kwanza,
mwanammke anayohaki ya kurithi upande wa familia yake, kwa ibara nzuri mwanamke
anayohaki ya kumrithi Baba yake, Mama yake, Kaka yake na Mtoto wake awe wa
kiume au wakike,upande wa pili anayohaki ya kurithi upande wa Mume wake pindi
mume wake anapofariki dunia.
Katika siku kama ya leo tunapokuwa tunakumbuka
kuzaliwa kwa Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Bi Fatma Zahra (a.s) ni siku ya kuwaeleza watu, Umma na Dunia Nafasi
ya Mwanamke katika Jamii kwa mtazamo halisi wa Uislamu halisi wa Mtume Muhammad
(s.a.w.w) vipi umemuweka Mwanamke.
Mwisho napenda kutoa hongera kwa ndugu zangu wote,
Waislamu na Watanzania na wasiokuwa Watanzania na watanzania wote kwa kuzaliwa
Mama huyu, Bint wa Mtume (s.a.w.w), ni siku ya sisi ya kumueleza mwanamke haki
alizopewa na vipi Uislamu ulivyomnyanyua Mwanamke na kumuweka daraja kwamba ni
mwanamke Muheshimiwa ni mtu kama mtu wa kawaida na wala hana mapungufu yoyote
ambayo unaweza kusema. Asanteni sana Alhamdulillah Rabil aalamiiin.
Imetolewa
na
Kiongozi
Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
20/03/2017
sawa na 20 Rabil Akhir 1438