Saturday, January 12, 2019

Sera ya Kiwahabi ni Sera ya Kuwagawa Waislamu-Maulana Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala akitoa Khutba ya Swala ya Ijumaa, Masjid Ghadir, Kigogo Post Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa katika jambo la kusikitisha na kuhuzunisha leo katika Ulimwengu wa Kiislamu ni kundi la Kiwahabi kufanya bidii na mikakati ya hali na mali, mikakati ambayo ni ya kuwagawa Waislamu, kuhakikisha Waislamu hawezekani wakawa kitu kimoja.

Maulana Sheikh Jalala alisema hayo jana  katika Khutba ya Swala ya Ijumaa, iliyoswaliwa Masjid Ghadir, Kigogo Post, Dar es salaam,akizungumzia Je, Uwahabi na Usuni ni Kitu Kimoja?, na kusema kuwa Kundi la Kiwahabi limefanikwa kuingia katika Jamii ya Waislamu Ahlul Sunna na kujiita wao ni Ahlul Sunna.

Maulana Sheikh Jalala alisema kuwa Mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Swalafun Swaleh yanaharamisha Kumkufurisha Mtu anaetoa Shahada Mbili hatakama mnatofautiana rai, lakini jambo la kushangaza kundi la Kiwahabi wanakufurisha Mtu anaetoa Shahada Mbili kwa kuwa wanatofautiananae rai.

“Watu walikuwa wamoja, Waislamu walikuwa ni Kitu kimoja, kutoka Mtume Muhammad (s.a.w.w), Moja ya jambo ambalo ukilisoma katika historia ya kipindi hicho cha watu ambao ni Salafun Swaleh, moja ya kitu walichokuwa wanapambana nacho na hawakikubali ni jambo la kumkufurisha mtu anaetamka Shahada Mbili, ila Kundi la Kiwahabi linakufurishana” alisema Maulana Sheikh Jalala.

Maulana Sheikh Hemed Jalala aliongeza kuwa kundi la Kiwahabi ndio kundi cha kwanza kuzuka duniani lililokuja kumkufurisha mtu wa Qibla, na kuhalalisha Umwagaji wa Damu yake na Unyaganyi wa Mali zake na kusema kuwa hayo sio Mafundisho ya Ahlul Sunna.

 “Kundi la Kiwahabi lilipokuja, lilipodhihiri, lilipozuka Duniani ndio Kikundi cha kwanza lililokuja kumkufurisha Mtu wa Qibla, yani Mtu anaesema Ashahadu allaa illaah ilallah waashahadu anna Muhammad Rasulullah, kwa kuwa hakubaliani na fikra zao huyo ni Kafiri, na damu yake ni halali na mali yake ni hali” aliongeza Maulana Sheikh Jalala.

Hatahivyo Maulana Sheikh Jalala alisisitiza kuwa Jamii ya Kiislamu haina misamiati ya kukufurishana wala kuitana Mushriki kwa watu wanaotoa Shahada Mbili, kwasababu wanatofautiana rai na mtazamo na kusema kuwa hayo sio Mafundisho ya Ahlul Sunna.

“Jamii ya Waislamu haijazoea, haijasikia wala haijalelewa katika Misamiati hii huyu ni kafiri, huyu ni Mshirikina, haipo kwenye kamusi ya Kiislamu, kwa waislamu wenyewe kwa wenyewe kutuhumiana na Shirki, kwa kosa gani? Kwa kosa la kutoafautiana rai na mtazamo ambapo sio Mafunzo na Maelekezo ya Maimam wanne wa Ahlul Sunna”alisisitiza Maulana Jalala.


No comments: