Baadhi ya wafanyakazi wa Tanroads wakikagua kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo Kimara ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia mia moja jana jijini Dar es Salaam. |
Wafanyakazi wa Mradi wa Mabasi ya endayo haraka Dar es salaam
(DART ),Wakalawa Barabara(TANROADS) pamoja na Umoja wa wamiliki wa
Daladala Dar es Salaam (UDART) wamefanya ziara ya kufahamu na kuelewa
miundo mbinu ya mradi huo.
Akizungumza na waandishiwa Habari jana jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Mifumo DART Bw. Junn Mlingi alisema mabasi hayo yatatumia
dakika 45 mpaka 35 kutoka kituo cha Kivukoni mpaka kituo cha Kimara na
kutumia dakika mbili kusimama kila kituo ili kuruhusu basi lingine
lifike katika kituo husika baada ya dakika tano.
“Mradi huu unatarajiwa kukabidhiwa mnamo Novemba mwaka huu kwani
mpaka sasa mradi umekamilika kwa asilimia 80 katika kipindi cha kwanza
ambapo unaanzia Kivukoni mpaka Kimara mwisho na Sheria ya matumizi ya
miundombinu ya DART ipo na inasema kwa yeyote atakayekamatwa akihujumu
miundombinu atatozwa faini ya shilingi laki tatu au kutumikia kifungo
cha miezi sita hadi mwaka mmoja ama kutumikia adhabu zote mbili”,
alisema Bw. Mlingi.
Akiendelea kuzungumza katika ziara hiyo Bw. Mlingi alisema
waratibu wa mradi huo wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora za
usafiri kwa wananchi na wakazi wa jiji la Dar es salaam kwa kuboresha
sheria , taratibu na miundombinu itayotumika kutumia usafiri huo wa
mabasi yaendayo harakakatika barabara zake maalumu.
Aidha Mratibu wa Mji DART Bw. Edwin Hema alisema Mabasi hayo
yatakua yanatembea kwa mwendo wa kawaida kwa kilomita 50 kwa saa ikiwa
ni kasi ya juu na kilomita 20 kwa saa ikiwa ni kasi ya wastani kutoka
kituo cha Kivukoni mpaka kituo cha Kimara na kuwa na muda maalumu wa
kushusha abiria na kupakia.
Mbali na hayo Bw.Hema alisema wananchi hawatatakiwa kugombania
mabasi kwani yatazingatia muda uliyopangwa katika taratibu zakubeba
abiria na pale gari itakapohitaji kusimama dereva atatangaza kituo na
abiria watatakiwa kukaa mbali na mlango mpaka milango itakapofunguka.Naye Mkurugenzi wa Mifumo alisema wameweka utaratibu kwa
walemavu wote watakaotumia usafiri huo kwa urahisi na haraka na kuweza
kuwahi kwenye shughuli zao bila yausumbufu kwa kuwa wana sehemu zao za
kukaa na kwa wale wanaotumia baiskeli za kusukumwa wataweza kupanda na
baiskeli zao ndani ya basi hilo.
Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar
es Salaam (UDART) na mradi wa mabasi hayo Bw. Sabri Mabruki amesema
mpaka sasa wameingia mkataba wa kuleta mabasi 76 ya kuanzia kupitia
Kampuni ya Golden Dragon kutoka Japan.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tanroads wakipanda gari la Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka jana jijini Dar es Salaam katika ziara ya kukagua Miundo Mbinu ya Mradi wa DART kabla ya kuanza kutumika . |