MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad
ametangaza rasmi kuwa yeye si makamu tena kwa sababu muda wa serikali
iliyoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein kikatiba ulikwisha tangu tarehe 2
Novemba, 2015.
Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 28(2), muda halali wa rais utakuwa umefikia kikomo itakapotimu miaka mitano tangu siku ambayo kiongozi huyo alikula kiapo cha utii cha kushika wadhifa huo.
Wakati huohuo, amesema Rais John Magufuli anapaswa kuchukua uongozi
wa juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, baada
ya kuonekana kuwa wenzake hawana nia njema.
Maalim Seif amewaambia wahariri na waandishi wa habari kwenye ukumbi
wa Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam leo kwamba Dk. Shein na
mawaziri wake wamekuwa wakibakia madarakani kwa ubabe tu kwa kuwa
kikatiba muda wa serikali yake ulishakwisha.
“Mimi si Makamu wa Kwanza tena. Kama kubakia basi nimebaki kwa sababu
ya kuweka kinga tu ya wafuasi wetu kwa kuwa hata mwenzangu Dk. Shein
ambaye pamoja na mimi ndio hatutegemei kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi,
yupo lakini si rais halali kwa sababu hiyo hiyo ya kumaliza muda wake,”
amesema.
Hilo la kama yeye bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais au laa, ni moja ya
maswali aliyoulizwa katika mkutano huo aliouitisha kwa lengo la
kuzungumzia mazungumzo yanayofanyika ya kutafuta utatuzi wa mgogoro wa
kisiasa wa Zanzibar.
“Ukweli uongozi wa Dk. Shein upo kibabebabe tu lakini ulishamaliza
muda wake rasmi Novemba 2, 2015. Ndio maana tunasema kwamba kitendo cha
Jecha Salim Jecha kuufuta uchaguzi pasina kuwa na mamlaka kumeifanya
Zanzibar kutokuwa na serikali wala Baraza la Wawakilishi,” amesema.
Amesema yeye yupo kwa sababu na hao wenzake wanaendelea kushikilia
nafasi zao, lakini kwake kuwepo ni muhimu kwa kuwa bila ya hivyo wafuasi
wake watapata madhara makubwa.
Maalim Seif ametoa msimamo huo huku akiwa ameshasoma taarifa ndefu ya
maandishi iliyojaa ufafanuzi wa vifungu mbalimbali vya sharia kuelezea
msimamo wake na Chama cha Wananchi (CUF) kuwa Dk. Shein si rais halali
na wala mawaziri si halali.
CUF ilishatangaza kuwa mawaziri wake saba katika Baraza la Mawaziri
la Dk. Shein hawapo kazini tangu Novemba 12 siku ambayo kimahesabu
ilitarajiwa kuwa ya mwisho kwa mamlaka ya Rais kuweza kuitisha Baraza la
Wawakilishi iwapo kungetokea dharura kabla ya kuapishwa kwa baraza
jipya baada ya uchaguzi.
Maalim Seif ambaye aliambatana mkutanoni hapo na wasaidizi wake
katika chama, wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT),
amesema mazungumzo yake na Dk. Shein pamoja na marais wastaafu wa
Zanzibar, yamefikia hatua ngumu kukamilika.
Amesema kwamba baada ya kuwa hawajaafikiana kutoka na kila upande
kubaki na msimamo wake – yeye akishikilia kuwa uchaguzi haukufutwa
kihalali kwa mujibu wa sharia, na wenzake CCM Dk. Shein na Makamu wa
Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kushikilia lazima uchaguzi urudiwe –
ilitakiwa Dk. Shein aitishe kikao cha mwisho cha kusomwa taarifa ya yale
waliyojadiliana.
“Dk. Shein amekuwa akikwepa kuitisha kikao hicho kwa wiki mbili
ameshinda kukiitisha licha ya mimi kumuandikia barua na kumkumbusha…
amekuwa akisema kwamba bado wanahitaji muda zaidi kujadiliana na
wenzake,” amesema na kuamini kuwa tayari mwenendo huo ni uthibitisho
kuwa tangu awali Dk. Shein hakuwa na nia njema katika kuitisha
mazungumzo hayo.
Maalim Seif amesema baada ya vikao vinane kufanyika huku wananchi
wakiwa wamekaa kimya wakisubiri, anadhani ni muhimu wananchi wajulishwe
kinachoendelea hasa kwa kuwa haoni kama viongozi wenzake hao wa CCM wana
dhamira njema ya kuondoa mgogoro.
Katika taarifa aliyoisoma huku matangazo ya mkutano huo yakirushwa
moja kwa moja hewani na vituo vitatu vya televisheni – Azam, ITV na Star
TV – Maalim Seif amesema badala ya Dk. Shein kuitisha kikao cha
kuwezesha taarifa iliyoandaliwa na sekretarieti kusomwa, zipo taarifa za
uhakika kuwa CCM imeagiza Tume ya Uchaguzi ikutane Januari 14, ili
kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio.
Amesema hoja ya uchaguzi wa marudio ilishindwa mapema, kwa sababu
haina msingi wowote wa kisheria hasa kwa vile Tume yenyewe iliridhika
kuwa uchaguzi ulikwenda vizuri mpaka hatua ya utangazaji wa matokeo.
“Hata ukisoma tovuti ya Tume ya Uchaguzi utakuta taarifa ya mwisho
iliyomo ni inayosema uchaguzi katika hatua zake zote mpaka kufikia
kutangaza matokeo ya kura ulikwenda vizuri… ukizingatia na taarifa za
waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa, hakuna hoja ya kurudiwa
uchaguzi.
“Hawa CCM kila wanakokwenda na hata katika mazungumzo wanapotakiwa
wawasilishe mezani ushahidi wa uchaguzi kuvurugika wanashindwa kutoa
vielelezo vyovyote. Sasa uchaguzi urudiwe kwa hoja ipi kama hakuna
ushahidi kuwa uliharibika,” amesema.
Maalim Seif amesema wakati Jecha anatoa tangazo la kufuta uchaguzi,
Oktoba 28, mwenyekiti huyo mwenyewe alikuwa ameshatangaza matokeo ya
majimbo 33 na majimbo yaliyobaki kura zilishajumuishwa.
Amesema Oktoba 28 ilikuwa siku ya mwisho kisheria kwa Tume
kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya urais na kwa hivyo “ilitakiwa
Jecha aongoze kikao cha kukamilisha kazi hiyo lakini hakuonekana kazini,
na makamu mwenyekiti akalazimika kuendesha kikao lakini ghafla Jecha
akasikika anatoa tangazo la kufuta uchaguzi, hatua ambayo hana mamlaka
nayo kisheria.”
Maalim Seif amesita kueleza CUF itakachokifanya iwapo Tume itaridhia
shinikizo za uongozi wa juu wa CCM Zanzibar, kutangaza tarehe ya
uchaguzi wa marudio.
Hata hivyo amesema hali hiyo itakapotokea itakuwa ni juu ya kikao cha
juu cha chama – Baraza Kuu la Uongozi – kutoa uamuzi baada ya kupata
maelezo ya matokeo ya mazungumzo.
Amesema ni wakati sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. John Magufuli kutumia mamlaka yake kuongoza juhudi za utatuzi wa
mgogoro huo kwa kuwa bado anaamini kuwa ana dhamira ya kutimiza ahadi
yake ya kusisitiza haja ya mgogoro huo kutatuliwa kwa amani na
maridhiano.