Wednesday, December 21, 2016

Mwenyekiti Wa CCM Taifa Rais Magufuli Akutana Na Viongozi Wapya Wa Chama Aliowateua Hivi Karibuni Na Dc Mteule Wa Ubungo

 
Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori akishuhudiwa na viongozi wapya wa CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016.


 
Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) pamoja na viongozi wapya wa CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016.
  
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) akibadilishana mawasiliano na na viongozi wapya wa CCM walioteuliwa hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo na Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga walipoenda kujitambulisha kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam  PICHA NA IKULU

Wafanyakazi wizarani kuhamia Dodoma Januari

http://www.habarileo.co.tz/images/Frequent/dodoma1.jpgWIZARA ya Katiba na Sheria imeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuhamia mjini Dodoma kabla ya Februari mwakani.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome awamu ya kwanza ya watumishi wa wizara hiyo inategemea kuondoka jijini Dar es Salaam Januari kwenda Dodoma.
“Kuhamia Dodoma haina mjadala, si sisi tu, ni wizara zote, awamu ya kwanza watawasili Dodoma kabla ya Februari. 

Watumishi wakaobaki watakwenda katika awamu zitakazofuata ambazo mtajulishwa baadaye," amesema Profesa Mchome.

Katibu huyo, aliwataka watumishi wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma.

Awali, tangazo la wizara hiyo lilisambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu orodha ya watumishi wake wanaohamia Dodoma kuwa ipo tayari na wataondoka Januari.

Profesa Mchome alisema mambo mengine ni ya ndani na asingependa kuyazungumza wazi lakini alisisitiza kuwa, kikubwa kuhamia Dodoma ni lazima na itafanyika kwa awamu hadi kukamilika mwaka 2018.Chanzo Habarileo

'Askofu' feki atuhumiwa kutapeli viongozi

JESHI la Polisi limesema limemkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la Wilfred Masawe (36), mkazi wa Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, ilieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli, zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa WhatsApp.

Alisema pia alikuwa akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamhusu na hivyo kutoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

"Pia alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano haya," alisema Bulimba katika taarifa yake hiyo.

Alisema baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

"Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake," alisema Bulimba.

Bulimba alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwatahadharisha wananchi wote kuwa makini na mtandao wa matapeli hao na yeyote mwenye taarifa za matapeli aziwasilishe polisi.

"Mnaombwa kama mna taraifa za matapeli mzifikishe haraka katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu ili waweze kushughulikiwa haraka," alisisitiza Bulimba.Chanzo.Habarileo