Wednesday, December 21, 2016

'Askofu' feki atuhumiwa kutapeli viongozi

JESHI la Polisi limesema limemkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la Wilfred Masawe (36), mkazi wa Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, ilieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli, zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa WhatsApp.

Alisema pia alikuwa akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamhusu na hivyo kutoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

"Pia alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano haya," alisema Bulimba katika taarifa yake hiyo.

Alisema baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

"Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake," alisema Bulimba.

Bulimba alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwatahadharisha wananchi wote kuwa makini na mtandao wa matapeli hao na yeyote mwenye taarifa za matapeli aziwasilishe polisi.

"Mnaombwa kama mna taraifa za matapeli mzifikishe haraka katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu ili waweze kushughulikiwa haraka," alisisitiza Bulimba.Chanzo.Habarileo

No comments: