Tuesday, December 20, 2016

Mkurugenzi wa JamiiForums atoa ya moyoni

Hatimaye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo amerejea uraiani akitokea mahabusu baada ya kuachiwa kwa dhamana jana huku akisema, ameshtakiwa kwa msimamo wake wa kulinda haki za watumiaji wa mtandao huo.
Melo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Ijumaa iliyopita akikabiliwa na kesi tatu kwa mahakimu watatu tofauti.

Ameshtakiwa kwa kosa la kuendesha mtandao wa kijamii ambao haujasajiliwa kwa kanuni za tovuti za Tanzania na kuzuia upelelezi wa polisi.

Katika kesi hizo, Melo alifanikiwa kupata dhamana kwa kesi mbili, huku akikwama kupata dhamana ya kesi moja baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana na kulazimika kupelekwa rumande.

Hata hivyo, jana Melo alifanikiwa kukamilisha masharti na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa na alimpatia dhamana kwa masharti.

Masharti hayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao walisaini bondi ya Sh5 milioni na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha Mahakama. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 29.

Baada ya kuachiwa, Melo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuishukuru wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa mjadala wa kutaka aachiwe huru kwa dhamana, tangu aliposhikiliwa na polisi kabla ya kupandishwa kizimbani.

Melo aliwatoa hofu watumiaji wa mtandano huo na kuwahakikishia kuwa JamiiForums ipo salama na haijachukuliwa taarifa zake.
“Hivyo Max nimekuwa mfano tu kwani haya ya kukamatwa yanaweza kumkuta mtu mwingine pia. Kikubwa inatakiwa uhuru wa kujieleza pamoja na kulinda siri za watumiaji wa mitandao,” alisema Melo.

No comments: