Afisa polisi wa Uturuki aliyekuwa akisema maneno ya "Allahu Akbar" na "Aleppo" amemshambulia kwa risasi na kumuua balozi wa Urusi nchini humo na kusababisha Rais Vladmir Putin kula kiapo cha hatua zaidi dhidi ya ugaidi.
Balozi Andrei Karlov alifariki dunia kutokana na majeraha ya kupigwa
risasi mjini Ankara katika kituo cha maonesho ya sanaa. Shambulio lake
limekuja wakati mawaziri wa kigeni wa mataifa hayo mawili pamoja na Iran
wakikutana kwa mazungumzo muhimu mjini Moscow kuhusu mgogoro wa Syria.
Picha
za tukio hilo zilimwonyesha mwanaume huyo akimmiminia risasi balozi
huyo mgongoni wakati akifungua maonesho ya picha za Urusi. Mshambuliaji
huyo aliyekuwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai alikuwa
amesimama nyuma ya balozi na alijihami kwa silaha. Baada ya kumfyatulia
risasi alisikika akitamka maneno ya "Allahu Akbar" yaani Mungu ni mkubwa
na kisha akasema "usisahau kuhusu Syria, usisahau kuhusu Aleppo, wale
wote walioshiriki katika dhuluma hii watawajibishwa".
Wizara ya
mambo ya ndani ya Uturuki imemtambua mshambuliaji huyo kama Mevlut Mert
Altintas, kijana mwenye miaka 22 aliyewahi kufanya kazi katika idara ya
polisi ya kupambana na maandamano kwa kipindi cha miaka miwili na nusu
iliyopita.
Rais Vladmir Putin akiwa na balozi Andrei Karlov aliyeuawa
Mauaji
hayo yamekuja siku kadhaa baada ya kutokea kwa maandamano nchini
Uturuki ya kupinga ushiriki wa Urusi nchini Syria, ingawa Moscow na
Ankara kwa hivi sasa zinafanya kazi kwa pamoja katika kuwahamisha raia
kutoka mjini Aleppo.
Rais Vladmir Putin wa Urusi ameyaita mauaji
hayo kuwa ni "uchokozi" na kuongeza kuwa uhalifu huo pasi na shaka ni
uchokozi unaolenga kuhujumu mahusiano baina ya Urusi na Uturuki pamoja
na hatua za amani Syria zinazopiganiwa na Urusi, Uturuki, Iran na
mataifa mengine yanayotaka kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa ndani wa
Syria.
Putin amesema jawabu kubwa ni kuzidisha mapambano dhidi ya
ugaidi wakati akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni
wa mataifa matatu mjini Moscow.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip
Erdogan ameunga mkono kauli ya Putin akiahidi kuchukua hatua za pamoja
katika uchunguzi wa mauaji hayo. "Uhusiano wetu na Urusi ni muhimu sana
kwetu. Ni muhimu sana kwa ukanda wetu. Natoa wito kwa wote wanaotaka
kuyadhoofisha mahusiano haya. Matarajio yenu yote hayatatimia,
yatapotea. Tumethibitisha malengo yetu na tutaendelea na dhamira hiyo
hiyo." amesema rais Erdogan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon na rais mteule wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi
waliolaani mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment