Wednesday, October 28, 2015

Mwenyekiti wa NEC Damian Lubuva "Atoa Sababu 13 za Uchaguzi Tanzania Bara Kuendelea"

Sheria ya mwaka 1977, ibara ya 74,kifungo kidogo cha 6 (b),inaipa tume ya uchaguzi mamlaka ya kisimamia  na kuratibu uendeshaji uchaguzi wa Raisi, Ubunge na Udiwani.

Pili uchaguzi wa uraisi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ni tofauti na uchaguzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .hii ni kwa sababu tume hizi zinasimamiwa na Katiba na Sheria tofauti.

Tatu uchaguzi wa Zanzibar  unasimamiwa na katiba na sheria ya Zanzibar  ya mwaka wa 1984, ya uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano inasimamiwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Nne, Ibara ya 38, kifungu kidogo cha katiba ya Jamhuri ya Muungano inaelezwa kuwa Raisi atachaguliwa na Wananchi kwamujibu wa Masharti  ya katiba  na kwa mujibu wa sheria itakayoweka masharti,kuhusu  uchaguzi wa Raisi ambapo itatungwa na bunge la Jamhuri ya Muungano.

Tano Ibara ya 104, kifungu kidogo cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inasema,  kuwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Serikali ya Zanzibar  atachaguliwa na Wananchi wa Tanzania Zanzibar  kwa mujibu wa masharti ya katiba ya Zanzibar  na kwa kufuata utaratibu  uliowekwa  kwa mujibu wa sheria  uliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar  inayohusu Uchaguzi  kwa Ujumla na uchaguzi Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 

Sita, Sheria ya Uchaguzi ya sura ya 343, inaweka masharti ya uchaguzi wa Raisi ,Wabunge na Udiwani  wa Jamhuri ya Muungano .

Saba, Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza masharti ya sheria ya Taifa ya Uchaguzi  ambayo inasimamia uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imeweka Vituo  vya kupigia na kuhesabu kura, daftari kwa kila kituo,masanduku ya kupigia kura  na fomu mbalimbali ambayo ni tofauti na Tume ya Uchaguzi wa  Zanzibar 

Nane, pmoja na Hilo tume ya Taifa ya Uchaguzi , kwa upande wa Uchaguzi wa Kura za Uraisi na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano,  Zanzibar kuteuliwa na kuweka mtendaji wake ambao watatoa taarifa wa uchaguzi moja kwa noja kwa tume na sio kwa ZEC .
Tisa,katika zoezi la upigaji kura pamoja na kupandika kura ya raisi , na wabunge wa Jamhuri ya Muungano upande wa Zanzibar ,Tume ya Taifa ya Uchaguzi , kusimamia yenyewe  mchakato wote huu .
Kumi, Hadi sasa Tume imeshapokea  matokeo ya kura za Uraisi kutoka majimbo yote ya Zanzibar na imeshayatangaza .

Kumi na Moja, Hakuna taarifa zozote za dosari kuhusu mchakato wa Upigaji kura za Uraisi,Ubunge na Udiwani wa Jamhuri ya Muungano kutoka Zanzibar ambazo zimepokelew.
 
Kumi na Mbili, kwa maana hiyo basi tume ya taifa ya uchaguzi inapenda kuwaarifu  Watanzania wote  kuwa mchakato wa Uchaguzi wa Uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Unaendelea  kama kawaida iliyokuwa imepangwa.

Kumi na Tatu, taarifa za Uvumi,kuwa Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungamo kuwa Umefutwa hiyo si kweli, ni Uvumi, ni Uongo na Upotoshaji na sio taarifa sahihi na zinapaswa kupuuzwa na sasa tunaendelea na  utangazaji wa Matokeo ya Awali kama kawaida .chanzo radio one

CUF watoa Tamko baada ya Kufutwa kwa Matokeo


chanzo

Mazrui Media

ZEC yaitaka Vyimbo Husika Kumchukulia Hatua za Kisheria Maalim Seif

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema imesikitishwa na kitendo cha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kujitangazia ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba, 2015 na imevitaka vyombo vinavyosimamia utii wa sheria kumchukulia hatua kiongozi huyo wa CUF.

“kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi amevunja kifungu cha 42 (5) cha sheria ya mwaka 1984 ambacho kinaipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kuwa chombo pekee chenye mamlaka hayo” Mwenyekiti huyo alifafanua.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari leo, Mweyekiti wa ZEC Jecha Salum Jecha alisema kuwa Maalim Seif ametenda kosa la jinai hivyo mamlaka zinazohusika zinapaswa kumchukulia hatua.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akithibitika ametenda kosa hilo atahukumiwa kulipa faini ya Tzs laki tano au kwenda jela miaka mitano au adhabu zote.
 
“Tume haina mamlaka ya kumkamata wala kumhoji Maalim lakini viko vyombo vyenye mamlaka hayo hivyo itakuwa ni vyema vikatimiza wajibu wao kwa kumkamata na kumhoji mhusika hasa ukizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili kwa Maalim Seif kutenda kosa kama hilo” Mwenyekiti wa Tume alieleza.

Alibainisha kuwa Tume yake imekijadili kitendo hicho kwa makini na uzito unaostahiki na kubainisha kuwa tangazo hilo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.

Bwana Jecha alibainisha kuwa Maalim Seif, kama walivyo wagombea wengine 13 wa nafasi ya urais wa Zanzibar wanaelewa fika sheria hiyo hivyo alitoa wito kwa wagombea wengine kuwa watulivu kama walivyo wananchi.

Kuhusu kasi ndogo ya Tumeyake kutangaza matokeo, Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakiki kura kujua kama hakuna tofauti ya kura baina ya zile zilizoandikwa na hali halisi.

“Wanaoandika na kuhesabu kura wote ni binadamu hivyo wanaweza kuchanganya mahesabu na ndio maana kazi yetu hivi sasa ni kulinganisha kura”alisisitiza Mwenyekiti wa Tume.

Kuhusu kukamatwa kwa karatasi za kupigia kura huko katika jimbo la uchaguzi la Chonga, Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba, Bwana Jecha alikiri kutokea kwa hilo na kwamba suala hilo sasa liko chini ya mikono ya Jeshi la Polisi.

Alitahadharisha juu vitendo vya baadhi ya wagombea kuchukua vyeti bandia vinavyoonesha kuwa tayari wao wameshinda nafasi za ubunge au ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

chanzo  kengete.com

Lowassa aitaka NEC kusitisha zoezi la kutoa Matokeo ya Urais.


Ndugu waandishi wa habari;
Tumewaita hapa kuwaomba muwaeleze Watanzania wenzetu, jumuiya ya kimataifa na marafiki zetu wengine wa ndani na nje, kwamba hatukubaliani na matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kote nchini.
 
Hii ni kwa sababu, upo ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba utangazaji wa matokeo hayo umevurugwa kwa makusudi na watendaji ndani ya NEC kwa kusaidiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Katika maeneo mengi ambako matokeo yameshatangazwa mpaka sasa, kilichoripotiwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais, hakifanani wala kuendana na matakwa halisi ya wananchi.
 
Matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai na yameandaliwa kwa lengo maalum la kumbeba mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli.
 
Katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi, kura zetu zimepunguzwa na kuongezwa kwa mgombea wa CCM; maeneo mengine, kura zilizotangazwa zimetofautiana na idadi halisi ya kura zilizopigwa.
 
Kwa mfano, matokeo yaliyotangazwa na NEC katika majimbo ya Mkoani na Mtambile, kisiwani Pemba, Makunduchi, Kiwengwa, Donge, Tunduru, Tunduma, Same Mashariki, Chambani, Tandahimba, Kilindi na kwingi kwingineko, ni miongoni mwa matokeo yanayothibitisha kuwa hiki kinachotangazwa na NEC, siyo kura za uchaguzi mkuu wa rais. Tunaweza kuiita, “mzimu wa uchaguzi.”
 
Ndugu waandishi wa habari;
Tangu kuanza kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi huu, viongozi wetu wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) – mimi mwenyewe juzi na jana Mhe. Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Abdallah safari walilieleza kasoro zilizojitokeza katika matokeo ya rais,
Hata hivyo, Tume imeendelea kutangaza matokeo hayo, bila kujali kile ambacho tumekieleza na kukilalamikia, kana kwamba tunachokisema ni ujinga, uzushi na uwendawazimu. Hili halikubaliki.
 
Aidha, katika maeneo mengine, likiwamo jimbo la Ubungo, matokeo yaliyoko mikononi mwa msimamizi wa uchaguzi, yanatofautiana na yale ambayo yamekusanywa kutoka katika vituo vyote vya jimbo hilo.
 
Hali kama hiyo ipo pia katika majimbo yote ambayo wagombea wa CHADEMA na wale wa vyama washirika vya CUF na NCCR – Mageuzi, ama wamekuwa na nguvu kubwa au wameibuka washindi.
 
Upo ushahidi wa wazi ambao, ninyi waandishi mnaweza kwa kutumia uandishi wenu kuuthibitisha kwamba, katika majimbo yote ambako wagombea wa UKAWA wameshinda, TUME imechelea kutangaza matokeo ya urais kwa sababu zinazothibitisha kuwapo kwa mikakati ya hila.
 
Ikumbukwe kwamba matukio yote haya ya NEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa yamekuja baada tu ya Jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vitatu vya kuhesabia kura na kuwakamata wataalam wetu waliokuwa wakipokea matokeo ya kura za rais nchi nzima ambayo hadi uvamizi huo ulipofanyika tulikuwa tukiongoza katika maeneo mbalimbali.
 
Ndugu waandishi wa habari;
Tunaamini kwa dhati kwamba, uvamizi huo ulifanyika mahususi kwa malengo ya kufanikisha uchakachuaji huo ambao sasa tunauona ukiendelea kufanyika kupitia matangazo yanayoendelea kutolewa sasa na NEC.
Wakati tukijua kwamba NEC ndiyo mamlaka pekee ya kisheria ya kutangaza matokeo ya urais, tunapenda kuwataarifu Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba hadi wakati uvamizi huo ulipofanyika kura zetu za urais tulizokuwa tumezikusanya zilikuwa zikionyesha tukiongoza kwa asilimia zaidi ya 60.
 
Kutokana na makosa hayo makubwa na ya makusudi yanayofanywa na watendaji wa NEC, mimi Edward Ngoyai Lowassa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, tunautangazia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa, kwamba hatukubaliani na matokeo yanayotangazwa na NEC.
 
Ndugu waandishi wa habari;
Kutokana na makosa hayo makubwa, tunaitaka NEC kusitisha mara moja utangazaji wa matokeo ya urais na kuanza upya kufanya uhakiki wa kile wanacholetewa na wasimamizi wa majimbo ambacho ushahidi unaonyesha kuwapo kwa vitendo vya hila ambavyo vinafanywa na NEC.
 
Ndugu wana habari
Kile kinachofanywa na NEC hapa ndiyo kile kile kinachoendelea kufanywa kule Zanzibar leo na ZEC ambako kunafanyika juhudi kubwa na za makusudi kupora kwa hila na kwa mabavu mwelekeo wa wazi wa ushindi wa Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF anayeungwa mkono na UKAWA, Maalim Seif Sharif Hamad.
 
EDWARD LOWASSA
MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
chanzo dutigite.com

NEC Yamjibu Mh Lowassa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ( Nec), imesisitiza kuwa inatangaza matokeo kwa kadiri inavyopokea na siyo kwa kupendelea upande wowote au kujali aliyeshinda.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva , alitoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam jana baada ya kutangaza matokeo ya urais katika majimbo 35.
Jaji Lubuva alisema madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa wanatangaza matokeo ya maeneo ambayo Chama Cha Mapinduzi kimeshinda ili kuaminisha umma kuwa ni washindi, siyo ya kweli.
"Wakati huu tusingependa kulumbana na chama au vyama vya siasa hata mgombea yeyote, matokeo tunayoyapokea ndiyo tunayatangaza, malalamiko ya kuwa Nec inatangaza kwa mwelekeo wa kupendelea, siyo kweli, tunatangaza bila upendeleo na kujali ameshinda nani," alibainisha.
Alisema siku ya kwanza (juzi), walipokea majimbo matatu na kuyatangaza na kwamba haikuwa rahisi kusubiri majimbo yote ndipo matokeo yatangazwe.

Waangalizi wa muungano wa Ulaya wamesema Tume ya uchaguzi ya NEC na ZEC zimejitahidi katika kufanikisha uchaguzi wa amani.

WAANGALIZI wa muungano wa Ulaya katika uchaguzi mkuu Tanzania wamesema kuwa tume za uchaguzi za NEC na ZEC zimejitahidi katika kufanikisha uchaguzi wa amani.
Mkuu wa waangalizi hao Judith Sargentini amesema kuwa tume hizo mbali na kukabiliwa na changamoto mbalimbali,lakini wamejitahidi katika kuhakikisha kila raia mwenye haki ya kupiga kura anapiga kura.
Aidha Judith amesema kuwa kitendo cha tume hizo kutoa matokeo nusu nusu kumevifanya vyama vya siasa kuanza kupoteza imani nayo huku wakisema kuwa changamoto hiyo inafaa itatauliwe haraka ili kuepusha hali ya hatari baadaye.
Amesema kuwa ni vema tume ikaja na matokeo kamili ambayo yatakuwa yamejitosheleza tofauti na jinsi yanavyotangazwa hivi sasa.
Aidha kwa upande mwingine Judith amevipongeza baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimeonyesha uwajibikaji stahiki na kuepukana na kupendelea vyama fulani.
Amesema kuwa ni vyema vyombo vingine ambavyo viliripoti kwa upendeleo vikajifunza kutoka katika vituo ambavyo havikufanya hivyo kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya taaluma ya habari.