Ndugu waandishi wa habari;
Tumewaita
hapa kuwaomba muwaeleze Watanzania wenzetu, jumuiya ya kimataifa na
marafiki zetu wengine wa ndani na nje, kwamba hatukubaliani na matokeo
ya uchaguzi mkuu wa rais, yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), kote nchini.
Hii
ni kwa sababu, upo ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba utangazaji wa
matokeo hayo umevurugwa kwa makusudi na watendaji ndani ya NEC kwa
kusaidiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika
maeneo mengi ambako matokeo yameshatangazwa mpaka sasa, kilichoripotiwa
kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais, hakifanani wala kuendana na matakwa
halisi ya wananchi.
Matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai na yameandaliwa kwa lengo maalum la kumbeba mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli.
Katika
baadhi ya majimbo ya uchaguzi, kura zetu zimepunguzwa na kuongezwa kwa
mgombea wa CCM; maeneo mengine, kura zilizotangazwa zimetofautiana na
idadi halisi ya kura zilizopigwa.
Kwa
mfano, matokeo yaliyotangazwa na NEC katika majimbo ya Mkoani na
Mtambile, kisiwani Pemba, Makunduchi, Kiwengwa, Donge, Tunduru, Tunduma,
Same Mashariki, Chambani, Tandahimba, Kilindi na kwingi kwingineko, ni
miongoni mwa matokeo yanayothibitisha kuwa hiki kinachotangazwa na NEC,
siyo kura za uchaguzi mkuu wa rais. Tunaweza kuiita, “mzimu wa
uchaguzi.”
Ndugu waandishi wa habari;
Hata
hivyo, Tume imeendelea kutangaza matokeo hayo, bila kujali kile ambacho
tumekieleza na kukilalamikia, kana kwamba tunachokisema ni ujinga,
uzushi na uwendawazimu. Hili halikubaliki.
Aidha,
katika maeneo mengine, likiwamo jimbo la Ubungo, matokeo yaliyoko
mikononi mwa msimamizi wa uchaguzi, yanatofautiana na yale ambayo
yamekusanywa kutoka katika vituo vyote vya jimbo hilo.
Hali
kama hiyo ipo pia katika majimbo yote ambayo wagombea wa CHADEMA na
wale wa vyama washirika vya CUF na NCCR – Mageuzi, ama wamekuwa na nguvu
kubwa au wameibuka washindi.
Upo
ushahidi wa wazi ambao, ninyi waandishi mnaweza kwa kutumia uandishi
wenu kuuthibitisha kwamba, katika majimbo yote ambako wagombea wa UKAWA
wameshinda, TUME imechelea kutangaza matokeo ya urais kwa sababu
zinazothibitisha kuwapo kwa mikakati ya hila.
Ikumbukwe
kwamba matukio yote haya ya NEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa
yamekuja baada tu ya Jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vitatu vya
kuhesabia kura na kuwakamata wataalam wetu waliokuwa wakipokea matokeo
ya kura za rais nchi nzima ambayo hadi uvamizi huo ulipofanyika tulikuwa
tukiongoza katika maeneo mbalimbali.
Ndugu waandishi wa habari;
Tunaamini
kwa dhati kwamba, uvamizi huo ulifanyika mahususi kwa malengo ya
kufanikisha uchakachuaji huo ambao sasa tunauona ukiendelea kufanyika
kupitia matangazo yanayoendelea kutolewa sasa na NEC.
Wakati
tukijua kwamba NEC ndiyo mamlaka pekee ya kisheria ya kutangaza matokeo
ya urais, tunapenda kuwataarifu Watanzania na jumuiya ya kimataifa
kwamba hadi wakati uvamizi huo ulipofanyika kura zetu za urais
tulizokuwa tumezikusanya zilikuwa zikionyesha tukiongoza kwa asilimia
zaidi ya 60.
Kutokana
na makosa hayo makubwa na ya makusudi yanayofanywa na watendaji wa NEC,
mimi Edward Ngoyai Lowassa, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano na
Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, tunautangazia umma wa Watanzania na
Jumuiya ya Kimataifa, kwamba hatukubaliani na matokeo yanayotangazwa na
NEC.
Ndugu waandishi wa habari;
Kutokana
na makosa hayo makubwa, tunaitaka NEC kusitisha mara moja utangazaji wa
matokeo ya urais na kuanza upya kufanya uhakiki wa kile wanacholetewa
na wasimamizi wa majimbo ambacho ushahidi unaonyesha kuwapo kwa vitendo
vya hila ambavyo vinafanywa na NEC.
Ndugu wana habari
Kile
kinachofanywa na NEC hapa ndiyo kile kile kinachoendelea kufanywa kule
Zanzibar leo na ZEC ambako kunafanyika juhudi kubwa na za makusudi
kupora kwa hila na kwa mabavu mwelekeo wa wazi wa ushindi wa Mgombea
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF anayeungwa mkono na UKAWA, Maalim
Seif Sharif Hamad.
EDWARD LOWASSA
MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
chanzo dutigite.com
No comments:
Post a Comment