Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema imesikitishwa na kitendo cha
mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kujitangazia
ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba, 2015
na imevitaka vyombo vinavyosimamia utii wa sheria kumchukulia hatua
kiongozi huyo wa CUF.
“kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi amevunja kifungu cha 42 (5)
cha sheria ya mwaka 1984 ambacho kinaipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kuwa
chombo pekee chenye mamlaka hayo” Mwenyekiti huyo alifafanua.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari leo, Mweyekiti wa ZEC Jecha Salum
Jecha alisema kuwa Maalim Seif ametenda kosa la jinai hivyo mamlaka
zinazohusika zinapaswa kumchukulia hatua.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akithibitika ametenda kosa hilo
atahukumiwa kulipa faini ya Tzs laki tano au kwenda jela miaka mitano au
adhabu zote.
“Tume haina mamlaka ya kumkamata wala kumhoji Maalim lakini viko vyombo
vyenye mamlaka hayo hivyo itakuwa ni vyema vikatimiza wajibu wao kwa
kumkamata na kumhoji mhusika hasa ukizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili
kwa Maalim Seif kutenda kosa kama hilo” Mwenyekiti wa Tume alieleza.
Alibainisha kuwa Tume yake imekijadili kitendo hicho kwa makini na uzito
unaostahiki na kubainisha kuwa tangazo hilo linaweza kusababisha
uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
Bwana Jecha alibainisha kuwa Maalim Seif, kama walivyo wagombea wengine
13 wa nafasi ya urais wa Zanzibar wanaelewa fika sheria hiyo hivyo
alitoa wito kwa wagombea wengine kuwa watulivu kama walivyo wananchi.
Kuhusu kasi ndogo ya Tumeyake kutangaza matokeo, Mwenyekiti huyo alisema
hivi sasa kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakiki kura kujua kama hakuna
tofauti ya kura baina ya zile zilizoandikwa na hali halisi.
“Wanaoandika na kuhesabu kura wote ni binadamu hivyo wanaweza
kuchanganya mahesabu na ndio maana kazi yetu hivi sasa ni kulinganisha
kura”alisisitiza Mwenyekiti wa Tume.
Kuhusu kukamatwa kwa karatasi za kupigia kura huko katika jimbo la
uchaguzi la Chonga, Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba, Bwana
Jecha alikiri kutokea kwa hilo na kwamba suala hilo sasa liko chini ya
mikono ya Jeshi la Polisi.
Alitahadharisha juu vitendo vya baadhi ya wagombea kuchukua vyeti bandia
vinavyoonesha kuwa tayari wao wameshinda nafasi za ubunge au ujumbe wa
Baraza la Wawakilishi.
chanzo kengete.com
No comments:
Post a Comment