Friday, October 9, 2015

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Yaema Pato la Taifa limeongezeka kwa Asilimia 7.9

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Morrice Oyuke (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa za pato la taifa robo ya pili ya mwaka kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2015. Kushoto ni Meneja Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa.

Na Dotto Mwaibale
 
OFISI ya Taifa ya Takwimu imesema pato la taifa limeongezeka kwa asilimia 7.9 huku sekta ya madini na uzalishaji umeme ikifanya kuongezeka kwa pato katika kipindi cha robo mwaka 2015 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2014.
Akizungumza  Dar es Salaam leo asubuhi wakati wakati akitoa taarifa za pato la taifa robo ya pili ya mwaka kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2015, Mkerugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Morrice Oyuke alisema ongezeko hilo la takwimu ni la miezi mitatu ya mwaka huu.
Oyuke alisema ongezeko hilo la pato la taifa linaenda sanjari na matokeo ya thamani ya pato la taifa kwa mwaka huu ambalo lilikuwa ni trilioni 89.0 ambapo  katika robo ya mwaka ni trilioni 45.5 ikilinganishwa na trilioni 39.0 katika mwaka 2014.
Alisema thamani ya pato la taifa ya robo mwaka ya trilioni 45.5 ni kubwa hivyo kusababisha  pato la taifa la mwaka mzima linaweza kukuwa kama uchumi hautotetereka.
“Kama uchumi hautaweza kuguswaguswa na matatizo mingene inaweza ikasababisha pato la taifa la mwaka huu likaongezeka badala ya ile iliyotegemewa hapo mwanzo,”alisema.
Alisema ongezeko hilo la pato la taifa limechangiwa na sekta mbalimbali kufanya vizuri katika kipindi cha robo mwaka.
Alisema sekta ambazo zimeongoza katika kipindi cha robo mwaka ni sekta ya madini,umeme,kilimo na mifugo,viwanda na ujenzi na huduma za kitaalamu.
Alisema sekta ya uzalishaji umemere imekuwa kwa asilimia 18.5 huku bidhaa za viwandani ni asilimia 6.9 madini mawe na kokoto  zimeongezeka asimilia 8.3 limeongezeka kutokana na shghuli za kiuchumi.
“Kutokana na taarifa hii ya pato la taifa kwa robo mwaka taarifa hizi zitumike katika kupanga na kurekebisha sera mbalimbali za maendeleo ya nchi,” alisema.

Benki Kuu ya Tanzania yaanzisha mfumo mpya wa malipo kwa massa 24, Utajulikana kama TISS

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bernard Dadi (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kuhusu benki hiyo kuanza kutumia mfumo wa malipo baina ya benki na benki kwa masaa 24 kwa siku saba za wiki kwa mwaka utakajulikana kama TISS. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki, Marcian Kobello.

Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea. Walioipa kamera mgongo kutoka kushoto ni Meneja Msaidizi wa Idara ya  Uhusiano wa benki hiyo, Vicky Msima na kulia ni Kaimu Meneja Huduma za Kibenki, John Kayombo.
Na Dotto Mwaibale
 
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuanzia mwakawa fedha ujao itaanza kutumia mfumo wa malipo baina ya benki na benki kwa masaa 24 kwa siku saba za wiki kwa mwaka ambapo utakuwa ukijulikana kama TISS.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo  mchana na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo BoT, Bernard Dadi na kuongeza mfumo huo utaweza kufanya kazi kwa ufanisi iwapo wafanyabiasha na wananchi kwa ujumla watauchangamkia kwani kwa sasa inapatikana kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku kwa benki za kibiashara zilizojiunga.
“Kwa sasa kuna mfumo huu wa TISS ambao umekuwa ukifanya kazi siku za kazi hadi saa mbili usiku na siku za mapumziko na sikukuu unafanya kazi kuanzia saa tatu hadi saa nane, ila tunatarajia mwaka wa fedha ujao utakuwa unafanya kazi kwa masaa 24,” alisema.
Alisema kimsingi mfumo huo una lengo la kuondoa mfumo wa kutumia hundi ambao unatumia muda mrefu na wakati mwingine kuna makosa ambayo yanatokea ya mtu anavyoandaa hivyo kuchelewa.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Marcian Kobello alisema uhaba wa sarafu ya shilingi 500 mitaani unachangiwa na wananchi wenyewe ambao wakienda benki hawachukui fedha hizo hivyo kusababisha zibakie huko kwenye mabenki.
Alisema sarafu za shilingi 500 zipo zaidi ya milioni 100 BoT lakini hadi sasa ni milioni 20 ndizo zipo katika mzunguko hali ambayo inachangia kuadimika kwa fedha hizo.
Alitoa mwito kwa wananchi na wafanyabiashara kuchukua sarafu hizo katika mabenki ili ziweze kufika katika mizunguko na dhana kuwa sarafu hiyo ina madini ya fedha ni uongo kwani asilimia 94 ni chuma na asilimia 6 ni nikoni.
Aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupeleka fedha ambazo zimechakaa katika mabenki ili waweze kubadilishiwa kwani utaratibu wa kuuza fedha haupo kisheria pamoja na ukweli kuwa hakuna sheria inayokataza.
 

TANZIA--Mgombea Ubunge wa ACT-Wazalendo,Arusha Mjini Afariki dunia

                                            
                  TAARIFA KWA VYOMBO 
                           VYA HABARI
Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Zuberi Kabwe anatoa  pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama  kwa ujumla kwa kuondokewa na kiongozi mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na aliyekuwa na mapenzi mema na nchi yake.

Amemuelezea Marehemu Mallah kuwa mbali na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Raslimali Taifa pia alikuwa mgombea Ubunge wa jimbo la  Arusha mjini  kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Mwenyekiti wa kwanza wa Ngome ya wazee  Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa.

Kutokana na Msiba huo Kamati ya Uongozi Taifa, imeagiza  kusimama kwa kampeni za ACT-Wazalendo kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 09 Oktoba hadi Jumapili tarehe 11 Oktoba 2015. Aidha bendera za chama kwa nchi nzima zitapepea nusu Mlingoti kwa siku tano kuanzia leo Oktoba 9 – 13, 2015.

Akimuelezea   Marehemu Mallah,Zitto, alisema “Nilimtambua Mzee Estomih Mallah kwa misimamo yake ya kupigania usawa na amani tokea akiwa katika CHADEMA na hakuogopa kupoteza nafasi ya udiwani aliyokuwa akiishikilia kwa sababu ya kukataa kuyumbishwa”

Amesema Mallah amefariki akiwa anapigania ukombozi wa watu wa jimbo la Arusha mjini na kwamba ACT-Wazalendo itamuenzi   kwa kukemea yale maovu yote aliyoanza kukemea na  kuendeleza mema yote aliyoyaacha.

“ACT-Wazalendo  itaendelea kumkumbuka daima kwa busara zake na uongozi wake uliotukuka, alijitoa kulitumikia taifa bila ubaguzi wala upendeleo wowote, hivyo Chama kitamuenzi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, 

Taratibu na Miongozo mbalimbali aliyoshiriki kuiasisi wakati wa uhai wake”
Oktoba 6 mwaka huu,  Mzee Mallah alishindwa kupanda jukwaani katika mkutano wa kampeni za mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, katika eneo la Ngaramtoni baada ya kujihisi kizunguzungu na kichwa kumuuma.

Baada ya hali hiyo alipelekwa katika hospitali ya St. Thomas alipopata mapumziko hadi jana Oktoba 8 alipohamishiwa hospitali ya KCMC.  

Mzee Mallah alifariki dunia wakati madaktari na wauguzi wakiendelea kumpatia huduma. Taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu.Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe.

Samson Mwigamba,
   KATIBU MKUU.

"Upo udharura wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli"

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran amesema kuwa kuna udharura wa kuundwa kamati ya uchunguzi ya kutafuta ukweli ili kuwatambua wahusika na wanaopaswa kubeba dhima kuhusu maafa ya Mina na kuvunjiwa heshima miili ya mahujaji walioaga dunia katika maafa hayo huko Saudi Arabia. 

Hujatul Islam wal Muslimin Kadhim Sediqi ameashiria katika hotuba ya Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran kuhusu madhara makubwa ya maafa ya Mina na kusisitiza kuwa madhara na mateso yaliyosababishwa na maafa hayo yameumiza nyoyo za Waislamu kote ulimwenguni, na kwamba hayawezi kusahaulika haraka. 

Hujatul Islam wal Muslimin Sediqi amekosoa kadhia iliyo nyuma ya pazia ya utawala wa Aal Saud kuhusiana na idadi kamili ya mahujaji waliopoteza maisha katika ibada ya Hija na kueleza kuwa viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanapasa kufanya juhudi zote na kuwa jadi ili kuweza kupata ukweli halisi kuhusiana na maafa haya yaliyoathiri ibada ya Hija ya mwaka huu na kupata ufumbuzi ili kuzuia kukaririwa matukio kama hayo.

Imam wa muda wa Swala ya Ijumaa ya jiji la Tehran amesema kuwepo udhaifu katika kusimamia marasimu ya Mina ni moja ya sababu kubwa za kutokea maafa huko Mina na kwamba Saudi Arabia haikufanya jitihada zozote za kusimamia vyema ibada ya Hija. 
Hii ni kwa sababu nchi hiyo hii leo inafikiria tu kuendesha vita huko Yemen na kuwauwa watu wa nchi hiyo wasio na hatia. Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameongeza kuwa, ushahidi unaonyesha kuwa baada ya kujiri maafa ya Mina, 

polisi wa Saudia si tu kuwa hawakuchukua hatua yoyote ya maana, bali walishindwa kufika kwa wakati katika eneo la tukio; polisi badala ya kuwasaidia mahujaji, waliamiliana vibaya na kwa mabavu na mahujaji waliojeruhiwa na walioaga dunia mara baada ya kufika katika eneo la tukio.  Chanzo Irib

Wanajeshi wa Israel wawaua shahidi Wapalestina 6

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mapema leo wamewaua shahidi Wapalestina 6 katika Ukanda wa Gaza. Duru za hospitali zinasema kuwa, Hammoud Hisham, Ahmad al-Harbawi, Abed al-Wahidi na Hussam Dawla wamefariki dunia kutokana na majeraha mabaya ya risasi. Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wametumia risasi hai kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Shejaiya huko Gaza ambapo mbali na kuwaua shahidi watu 6 pia wamewajeruhi wengine kadhaa. 
Wapalestina wanaandamana kupinga hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti mtakatifu wa Al-Aqsa. Kwa siku kadhaa sasa, Israel imekuwa ikiwavamia Wapalestina na kuwakamata ovyo huku ikiwazuia kuingia na kufanya ibada katika msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.    
Wanajeshi wa Kizayuni pia wamewavamia waandamanaji wa Kipalestina katika Nablus huko ukingo wa magharibi wa Mto Jordan na habari zinasema watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wengi kukamatwa.Chanzo irib