Wednesday, August 8, 2018

“Kukua kwa Uchumi na Biashara msingi wake ni Amani na Utulivu” Maulana Sheikh Jalala

Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania Maulana Sheikh Hemed Jalala amesema kuwa kama watazania wanataka kuwa na Uchumi wa Kati na kuhakikisha Biashara zinafanyika ni lazima watanzania wahakikishe kuwa na Amani na Utulivu katika nchi yao.
Maulana Sheikh Jalala amesema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari jana jijini Dar es salaam, ikiwa ni katika kutoa Ujumbe kwa Wahujaji Watarajiwa na kwa Watanzania kwa Ujumla, Ujumbe ukiwa ni  Hijja ni Mkusanyiko wa Kuienzi Amani na Maelewano.
“Sisi watazania na wasiokuwa watanzania kama tunataka Biashara zetu ziboreke , lazima tuwe na Utulivu, lazima tuwe na amani, kama tunataka Tanzania iwe Tanzania ya Viwanda haiwezekani kuwa ya viwanda lazima Tanzania hii iwe na amani, kama tunataka Tanzania ipigiwe mfano kwa uchumi wa kati kwa uchumi Mkubwa hilo haliwezekani mpaka tuweze kuiboresha amani na utulivu.” Alisema Maulana Sheikh Jalala.
Aidha Maulana Sheikh Jalala Amesema kuwa moja ya mafunzo yanayopatika kwa kuwa na Nabii Ibrahimu  ambae anakubaliwa na watu wote wenye dini tofauti, Fikra tofauti na Madhehebu tofauti ni Jambo la Kuvumilana kati ya dini zote.
“Hijja ni Ibada ya kuenzi Amani na alietangaza ni Mtume Ibrahim (a.s) anaekubalika na Dini zote, kwanini awe ni yeye mtangazaji? Moja ni kitu muhimu sana cha kutambua ni kitu cha kuvumiliana, kana kwamba Mungu alitaka Walimwengu watatofautiana kifikra, Kirai,Kimtazamo, Kimadhehebu na Kidini, lakini akawataka hawa wawe na Nabii mmoja Ibrahimu ambae ni Nabii wa hawo watu wote Mnamkubali, wajifunze kitu kinachoitwa Kuvumiliana katika Dini” Alisisitiza Maulana Sheikh Jalala
“Kwahivyo Falsafa ya Hijja aliyoitangaza Nabii Ibrahimu (a.s) moja yake ilikuwa ni amani, utulivu na kuenzi hali hali ya utulivu, uwe ni utulivu wa Kiroho au uwe ni utulivu wa Kifikra, ambayo hii ni utulivu wa aina ya Pili,” Alisema Maulana Sheikh Jalala
Hatahivyo Maulana Sheikh Jalala ameeleza baadhi ya Viashiria vya Ufunjifu wa Utulivu na  Amani katika Jamii ikiwa ni pamoja na matukio ya Ubakaji, Matumizi mabya ya Pesa za Umma, wizi,Makosa ya Jinai, Mauaji, Unyanyasaji na Wanaofanya Biashara ya Kuuza Miili yao.

“Jamii yoyote inayowafanyakazi yanaohujumu mali ya Umma, Jamii yoyote ambayo ina wezi, Jamii yoyote ambayo Kubaka ni kitu cha kawaida, Jamii ambayo ndani yake kuna mauaji, kuna ukatili, kuna kuchinjana, Jamii yoyote ambayo biashra ya Madawa ya Kulevya ni jambo la kawaida, Jamii ambayo inamakosa ya Jinai, ijue jamii hiyo ni jamii ya watu wasio kuwa na Utulivu na amani”.Alisema Maulana Sheikh Jalala