|
Baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma wakiwa katika kikao kazi kupitia njia ya video kwa makatibu
tawala wa mikoa na wasaidizi wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za
mitaa na wakuu wa idara za utawala na rasilimali watu katika mamlaka za
serikali za mitaa kwenye mikoa ya Dares Salaam, Kagera,
Tanga,Tabora,Manyara, Morogoro, Rukwa na Katavi kilichofanyika leo
kwenye ukumbi wa Wakala wa Mafunzo kwa Mtandao iliyopo jijini Dares
Salaam. |
Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma HAB Mkwizu wa pili kulia akifafanua
jambo wakati kikao kazi kupitia njia ya video kwa makatibu tawala wa
mikoa na wasaidizi wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na
wakuu wa idara za utawala na rasilimali watu katika mamlaka za serikali
za mitaa kwenye mikoa ya Dares Salaam, Kagera, Tanga,Tabora,Manyara,
Morogoro, Rukwa na Katavi kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Wakala wa
Mafunzo kwa Mtandao iliyopo jijini Dares Salaam.
Picha zote na Magreth Kinabo – MAELEZO
Serikali imefanikiwa kuboresha
utendaji kazi wa utumishi wa umma kwa kuendesha mikutano kupitia njia
ya video(TEHAMA) katika taasisi zake,wizara idara ili kuongeza kwa
ufanisi na tija kwa gharama nafuu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwa
muda mfupi.
Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma HAB Mkwizu
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uendeshaji wa kikao
kazi kupitia njia ya video kwa makatibu tawala wa mikoa na wasaidizi
wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na wakuu wa idara za
utawala na rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa kwenye
mikoa ya Dares Salaam, Kagera, Tanga,Tabora,Manyara, Morogoro, Rukwa na
Katavi kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Wakala wa Mafunzo kwa Mtandao
iliyopo jijini Dares Salaam.
“Serikali imebuni sera ya TEHAMA
na Serikali Mtandao katika kutekeleza majukumu yetu kwa kulenga tija na
ufanisi. Leo tunazungumzia mpango wa Matokeo Mkubwa Sasa (BRN) ili
tupate matokeo ya BRN kwa ufanisi na kwa wakati hatuna budi kutumia
TEHAMA,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo.
Mkwizu alisema mkutano huo ni wa
awamu ya kwanza kufanyika kwa kupitia njia hiyo, hivyo vikao vitatu
vimefanyika, kikao cha kwanza kufanyika kilifanyika Septemba 15,mwaka
huu ambao ulihusisha watendaji hao kwenye mikoa ya Mwanza, Mbeya,
Kilimanjaro, Dodoma , Ruvuma Kigoma,Lindi na Geita.
Aliongeza kwamba mkutano wa awamu
ya pili ulifanyika Septemba 17, mwaka huu ambapo ulihusisha watendaji
hao kwenye mikoa ya Arusha, Singida,Pwani,Iringa, Mara,Mtwara,
Shinyanga, Njombe na Simiyu.
Alizitaja mada zilizojadiliwa
katika mikutano hiyo kuwa ni Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010
na kanuni zake, wajibu wa waajiri katika ufuatiliaji na uzingatiaji wa
maadili katika utumishi wa umma , ukaguzi wa rasilimali watu katika
utumishi wa umma, ambalo ni jukumu la msingi la Tume ya Utumishi wa
Umma,ambao wanakagua mifumo yamenejimmenti rasilimali watu ya utumishi
wa umma na kuona inatekelezwa vipi na tathimini ya kazi katika utumishi
wa umma ili kulinganisha kazi mbalimbali na hatimaye kuja na
mapendekezo kazi mbalimbali watu walipwe vipi kulingana na unyeti,
madaraka ili zinazofanana zilipwe sawa na zisizofanana zilipwe tofauti.
Alisema awamu ya pili ya uendeshaji wa mikutano kwa kutumia njia hiyo itafanyika Novemba mwaka huu.
Mkwizu alifafanua kwamba tayari
Serikali imeshaweka mwongozo katika taasisi zake na mamlaka za
Serikali ili ziweze kufanya mikutano au kikao kazi kwa njia video. Hivyo
mikoa yote imeshafungiwa vifaa maalum kwa ajili ya matumizi hayo
isipokuwa mikoa mipya ambayo ambayo hujiunga na mikoa mama.
Kwa upande wake Mkurungezi
Mtendaji wa Wakala wa Mafunzo wa Serikali Mtandao(TaGLA), Charles
Senkondo alisema ulianzishwa mwaka 2011 ili kuongeza kasi ya uboreshaji
wa huduma.
Alisema mfumo huo umewezesha
madaktari bingwa wa hapa nchini kuweza kutibu wagonjwa kwa kuwasiliana
na madaktari wenzao mabingwa kutoka nje ya nchi, watu kufanya usaili na
kupata kazi za kimataifa na mahakama kuendesha kesi kwa kuwasiliana na
mashahidi walioko nje ya nchi.
Alizitaja changamoto wanazokutana
nazo kuwa ni pamoja na baadhi ya watu kuwa na fikra potofu katika
matumizi ya TEHAMA, wengine wanafikiri ni kitu kigumu na kuwa na woga
wa kutumia lakini kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wadau
mbalimbali wameendesha mikutano mingi na wanao uwezo wa kutoa ushauri
na mwongozo inayosaidia kuendesha mikutano kupitia njia hiyo ili iweze
kufanyika vizuri.
“Watanzania wafahamu kwamba wakala
wa mafunzo kwa njia ya mtandao imeanzishwa na Serikali kwa ajili yao,
hivyo ninatoa wito waweze kuitumia na kupeleka taarifa kwa urahisi
ambazo zinawafikia watu wengi kwa wakati mmoja na sisi tuko tayari
kutoa ushauri ili mikutano kufanyika ipasavyo”, alisema Senkondo.