Thursday, September 17, 2015

Dk John Magufuli - mapokezi ya kishindo mjini Kigoma

Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli jana alipata mapokezi ya kishindo mjini Kigoma alikofanya mkutano mkubwa na wa kihistoria.
Dk Magufuli alipokewa na umati mkubwa wa wananchi waliofurika katika uwanja wa Kawawa kwa ajili ya kumsikiliza.
Akiwahutubia maelfu ya wananchi hao, Dk Magufuli aliwaomba wananchi hao kumchagua kuwa rais kwa kuwa atachagua mawaziri watakaowatumikia wananchi kwa nguvu zao zote na wataongozwa na waziri mkuu makini.
“Nitateua mawaziri ambao wataweza kwenda na kasi ya maendeleo mtakayohitaji, nitasimamia mimi mwenyewe pamoja na waziri mkuu makini na watakuwa tayari hata kuumwa na mbu, kunguni wakati wote ili mradi wawatumikie watanzania hata usiku wa manane,” alisema.

Lowassa Kuwakabidhi Wananchi Kiwanda Cha Mtibwa

Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zinaendelea, wagombea wameendelea kutoa ahadi zinazolenga moja kwa moja matakwa ya wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo jana mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa aliwagusa wakazi wa Morogoro.
Lowassa aliwaahidi wakazi hao kuwa akichaguliwa kuwa rais atahakikisha anafuatalia na kutafakari taratibu na sheria kuona uwezekano wa kukirudisha kiwanda cha sukari cha Mtibwa mikononi mwa wananchi hao.
“Lakini ninaamini hilo suala linawezekana, kukitaifisha kiwanda hiki kuwa kiwanda cha umma,” alisema.
Katika hatua nyingine, Lowassa aliwaahidi wananchi hao kuwa atahakikisha serikali yake inakuwa serikali rafiki ya wananchi wa kima cha chini hususan mama ntilie, bodaboda na wafanyakazi wadogowadogo huku akiisisitiza ahadi yake ya kuanzisha benki yao.
Kadhalika, Lowassa alisema kuwa ahadi ya serikali yake kuwa itatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu itazingatia utoaji wa elimu bora na sio bora elimu.

Godbless Lema Amgeukia Wema Sepetu


Kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu zina hamasa ya aina yake huku kila kambi ikihakikisha hailiachi jiwe lolote la upande hasimu bila kugeuzwa.
Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ameukejeli uamuzi wa CCM kumchagua Wema Sepetu kuwa mwenyekiti msaidizi wa kampeni ya chama hicho ya ‘Mama Ongea Na Mwanao’, yenye lengo la kuwashawishi akina mama kuwaambia watoto wao waichague CCM.
“Hivi kwa nini watanzania tunadanganywa mchana kweupe na akina Wema Sepetu na wenzake, eti wameanzisha kampeni inaitwa ‘mama ongea na mwanao’, hivi kweli kuna mtu asiyejua tabia na mienendo ya Wema Sepetu ilivyo!? Sasa ataongeaje na watoto wetu,” alisema Lema kwenye mkutano wa Kampeni uliofanyika wilayani Karatu.
Wema Sepetu ni mwenyekiti msaidizi wa kampeni ya Mama Ongea na Mwanao ya CCM, iliyo chini ya uenyekiti wa Steve Nyerere.

Mbatia: Tunataka Mdahalo Na CCM

Mwenyekiti mwenza wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia
Mwenyekiti mwenza wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia ameomba kufanyika mdahalo kati ya vyama vinavyounda umoja huo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbatia alitoa ombi hilo jana usiku katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo aliwasihi viongozi wa CCM kuwachagua wasemaji wao ili waweze kujumuika pamoja katika mdahalo kwa lengo la kunadi sera na ilani za vyama vyao.
“Tunawataka CCM wachague msemaji wao, na kwa kuwa Ukawa haitambuliki kama chama cha siasa, vyama vyote vya upinzani vitaweka wasemaje wao, ili tuache porojo na maneno maneno,” alisema Mbatia na kuongeza kuwa vyama ndivyo vinavyowakilisha mfumo wa serikali inayotarajiwa na sio mtu mmoja.
Kadhalika, Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi alizungumzia taarifa zilizoeleza kuwa mgombea wa Chadema aliomba kura kanisani. Alisema habari hizo ni za uongo kwa kuwa Lowassa aliwaomba waumini wa dini yake kumuombea na sio kumpigia kura. Alisema Lowassa sio mshirikina na ndio sababu amemtanguliza Mungu kwenye kampeni zake.
Aidha, alieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) walipaswa kumkemea mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa kauli yake kuwa mabadiliko yanaweza kuisababishia nchi matatizo kama ya Libya. Alisema badala ya kumkemea NEC iliwaeleza kuwa kauli hiyo ni ‘vionjo vya kisiasa’. Alisema kauli hiyo haikuwa kauli ya busara kwa kuwa ililenga katika kuwashawishi wananchi kwa kuwatishia hali ya usalama.
Katika hatua nyingine, Mbatia alimkosoa mgombea urais wa CCM kwa kile alichodai kuwa anataka kujitenganisha chama chake ili aonekane kuwa yeye sio chama katika kukwepa kubeba majukumu ya maswali ya watanzania kwa chama hicho.
“CCM ni Magufuli na Magufuli ni CCM, watanzania msirubunike,” alisema Mbatia akitoa mfano wa mabango ya mgombea huyo kuwa hivi sasa yameandikwa ‘Chagua Magufuli’ huku yakikitenga chama tofauti na miaka iliyopita ambapo wananchi walihimizwa kuchagua Chama sio mtu.chanzodar24.com