Saturday, December 24, 2016

MBOWE AVUNJA UKIMYA KUHUSU KUPOTEA KWA BEN SAANANE

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi. 

Mbowe alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa. 

Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake. 

“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema Mbowe. 

Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.” 

Katika hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba imeendelea kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo mahabusu. Alisema hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani. 

Akijibu madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa mbalimbali vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi haimkamati mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha sheria. 

“Hayo yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi. Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa mjomba wangu tutamkamata.” 

Msigwa kidedea 
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliibuka kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na asilimia 58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa. 

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na asilimia 88 ya kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika. 

Mnyika alisema kuwa nafasi ya  mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa. 

Mnyika alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au hapana kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa kuweka wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya chama. 

“Hivyo Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea wote na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo" Alisema Mnyika

Russia kuimarisha nguvu zake za kijeshi nchini Syria

Mbunge moja wa Russia amesema kuwa, Moscow imeamua kuimarisha nguvu zake za kijeshi nchini Syria.

Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Andrei Nekrasov Naibu wa Mkuu wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Russia DUMA ametangaza habari hiyo na kusema kuwa, Russia inafanya juhudi za kuimarisha kambi yake ya kijeshi katika bandari ya Tartus nchini Syria na hivyo kurejea katika misimamo yake ya zamani ya kumarisha uwepo wake kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Andrei Nekrasov ametoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Russia za kupambana na magenge ya kigaidi na kuongezeza kuwa, kinyume kabisa na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, Shirikisho la Russia linapigania usalama duniani na mfano wa wazi kabisa ni jinsi jeshi la Russia lilivyopata mafanikio makubwa huko nchini Syria.
Mfumo wa kujilinda kwa makombora wa Russia S400

Naibu wa Mkuu wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Russia ameongeza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo hivi sasa wameelekeza nguvu zao kwenye kuwafurusha magaidi nchini Syria.

Kabla ya hapo Rais Vladimir Putin wa Russia alitaka kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi baina ya Moscow na Damascus kwa nia ya kuimarisha harakati ya jeshi la majini la Russia katika bandari ya Tartus nchini Syria na kuwataka maafisa wa kijeshi wa Russia kuzungumza na maafisa wenzao wa kijeshi wa Syria kuhusu suala hilo kama ambavyo aliitaka pia Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilipe uzito mkubwa jambo hilo.

Baraza la Usalama lapasisha azimio dhidi ya Israel, ushindi kwa Palestina

Hatimaye baada ya vuta nikuvute, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kutaka kusimamishwa mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Azimio hilo ambalo ni la kwanza kupasishwa na Baraza la Usalama dhidi ya Israel katika kipindi cha miaka minane, liliungwa mkono kwa kura 14, huku nchi moja pekee ikijizuia kupiga kura.
Awali azimio hilo lilitazamiwa kupigiwa kura siku ya Alkhamisi, lakini Misri ambayo iliandaa rasimu ya azimio hilo ikalazimika kuakhirisha, kufuatia mashinikizo ya Washington.
Rais mteule wa Marekani, Donald Trump
Hapo jana, Rais mteule wa Marekani, Donald Trump alimpigia simu Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi na kuitaka Cairo iakhirishe uwasilishaji wa rasimu ya azimio hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aidha kabla ya hapo, Trump alitaka kupigiwa kura ya turufu azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel tokea mwaka 1967.

Wakati huo huo, Saeb Uraikat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina amepongeza hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupasisha azimio hilo na kufafanua kuwa, kura hiyo ni ushindi na haki kwa Wapalestina. Aidha amemtaka Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kuchagua kati ya "uhalali wa kimataifa" au kuwaunga mkono "Maghasibu na wenye misimamo mikali".
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel
Inaarifiwa kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel ameingiwa na kiwewe kufuatia hatua hiyo ya Baraza la Usalama la UN, na kusisitiza kuwa utawala huo khabithi hautayaheshimu maamuzi hayo ya Umoja wa Mataifa, sambamba na kumlaumu Rais wa Marekani anayeondoka, Barack Obama kwa kushindwa 'kuilinda Israel'.

Sheikh Jalala awatakia Salam za Kheri na Fanaka ya Kuzaliwa Yesu kwa Wakristo Wote



Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Itnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akitoa salam za kheri na fanaka ya kuzaliwa Yesu Kristo kwa Ndugu zetu Wakristo,au Nabii Issa (a.s) kwa sisi Waislam, Kulia kwake ni Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya Al-Mustafa Alkhairiya Sheikh Jafar Mwazoa leo Dar es salaam.
TAARIFA KWA UMMA
SALAMA ZA KHERI NA FANAKA KWA WAKRISTO WOTE KWA KRISMAS NJEMA.24/12/2016


Amani ya Mwenyezimungu iwe juu yenu nyote.Salam hizi za Mkono wa Krismas kwa ndugu zetu Wakristo wa Tanzania na Wakristo wote wanaosheherekea Mazazi (Kuzaliwa) kwa Nabii Issa   (a.s) Mtume wa Mungu kwa ndugu zetu wakristo ni Yesu Kristo.

Mkono huu wa Kristmass, Mkono huu wa Eid ni Mkono uliobeba Umoja, ni mkono uliobeba Mshikamano ni Mkono wa Eidi, ni mkono wa Krismaa uliobeba amani na Maelewano. Lakini kubwa zaidi la kujiuliza na huenda wengi wakajiuliza swali hii kwamba kwanini Viongozi wa Dini wa Kiislam katika siku hii ya kuzaliwa Yesu Kristo au Nabii Issa (a.s) kwa Wiaslam, viongozi hawa wa Kiislam hususan Wafuasi wa Madhehebu ya Ahlulbayt (a.s) au Mashia watoe Mkono wa Krismas,mkono wa kheri, 

mkono wa Baraka kwa ndugu zao wakristo Watanzania na wa Dunia kwa ujumla ni kwasababu chache za harakaharaka nitakazozieleza
Sababu ya kwanza tutambue sisi Waislam na ndugu zetu Wakristo sote tunakusanywa na neon moja kwamba sisi ni Waumini, 

sote tunamuamini Mungu mmoja ambae ndie aliyeumba Mbingu na ardhi na akawaumba wanadam wote hilo la kwanza, Sote tunaamini kwamba kuna vitabu vya Mungu vilivyoshushwa hapa duniani, tunaamini uwepo utumwa mitume wa Mungu na vilevile tunaamini siku ya mwisho.

Kwahivyo kuyaamini haya yanatukusanya sisi watanzania Waislam na Wakristo chini ya mwamvuli mmoja wa imani, kwahivyo leo hii waislam tunapotoa mkono wa Krismas, mkono wa eid kwa ndugu zetu wakristo ni kwasababu ni waumini wenzetu katika kumuamini Mungu mmoja, katika kuamini siku ya mwisho na katika kuamini mitume waliotumwa na kutuletea ujumbe hili la kwanza.

La pili kwanini mkono wa Krimsaa kwa ndugu zetu Wakristo, ni kwasababu sisi wote tunakusanya  na anuani ya Utanzania, Waislam tulioko hapa ni Watanzania, wakristo tulioko hapa ni Watanzania, kama sote ni watanzania ni wajibu wetu sote kuilinda Tanzania yetu. Kama sisi Wislam na Wakristo ni Watanzania ni wajibu wetu umoja na mshikamano wetu kama Watanzania, kama sisi sote ni watanzania ni makosa makubwa kufungua mwanya wowote wa mvutano kati ya Waislam na Wakristo hapa Tanzania, kwanini kwa sababu sote tunakusanywa  ni Utanzania.

Kwasababu sisi sote ni watanzania ni lazima tuwe na sifa ya kuvumiliana, itikadi zetu, fikra zetu na mitazamo yetu isitugawanye kwa kuwa sisi tunakusanywa na neon Utanzania,Na Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa sisi waislam anasema “kupenda inchi yako ni katika imani” kwahivyo leo hii sisi kama Viongozi na kama Waislam na kama Waislam Shia Ithnasheriya tunapotoa Mkono wa Krisma, mkono wa Baraka na mkono wa Eid kwa ndugu zetu Wakristo moja ni kuenzi huu Utanzania tuliokuwanao ambao ni kitu muhimu na ni kitu kikubwa,Lingine ni kwanini tunatoa mkono wa Krismas, 

ni kwasababu sisi Waislam, Dini ya Uislam ni dini ya Mapenzi, Dini ya Uislam ni dini ya kufahamiana, Dini ya Uislam ni dini ya amani, Dini ya Uislam ya kupendana, anaeueleza Dini ya Uislam sio dini ya kupendana huyo hajauelewa Uislam.

Kwahivyo Uislam ni dini ya Mapenzi, ni dini ya Maelewano ni dini ya Maelewano,Mtume Muhammad (s.a.w.w) anatufunza siku zote anasema “ penda watu wapate kile ambacho unachopenda ipate nafsi yako” kwahivyo Uislam ni dini ya upendo, uislam ni dini ya Maelewanoni dini ya masikilizano leo hii tunapotoa mkono wa Baraka na mkono wa kheri na fanaka katika Eid ya Krismass malengo makubwa ni kuwaonyesha ndugu zetu wakristo kwamba Uislam ni dini inayompenda kila mtu, Uislani dini iliyohimiza ujirani mwema na ujirani huu mwema hauwezi kudhibitika wala kufanyika pasi na watu kupendana.

Kwahivyo mkono huu wa Krismass ni mkono wa kuwaonyesha ndugu zetu Wakristo Wayanzania kwamba Uislam ni dini ya mapenzi, kwamba uislam ni dini ya kuelewana, Sayyidina Ali (a.s) kiongozi baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) anawausia watoto wake anawambia “Hala hala nawahusieni majirani” Sayyidina Ali (a.s) alipokuwa anawahusia watoto wake swala la Majirani, hajawaambia Majirani Waislam, hajawaambia Majirani wachamungu la, kawaambia Majirani yaani majirani wote ima wachamungu, Wakristo, Waislam na hata wasiokuwa na Dini.

Kwahivyo kitendo cha leo cha sisi kutoa Mkono wa Krismass, mkono wa Kheri na Baraka kwa ajili ya ndugu zetu watanzania wasiokuwa Wiaslam ni kutaka kuwaonyesha kuwa Uislam ni dini ya mapenzi uislam ni dini ya maelewano.Nukta nyingine muhimu kwanini Mkono wa Krismass,mkono wa Kheri na Baraka kwa ndugu zetu Wakristo  kwa sababu hakuna uadui kati ya Uislam na Ukristo, hakuna Uadui kati ya Waislam na Wakristo, 

Ukimsoma Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ukiisoma Qur’an yetu na ukisoma mwenendo wa watu waliokuja baada ya mtume Muhammad (s.a.w.w) utapata yakwamba wanavyoueleza Uislam, Uislam na Ukristo sio uadui kati yao bali ni Udugu na maelewano kati yao.

Iangalie Qur’an inavyowasemesha Wakristo inawaitaje, inawaita “Ahlul Kitabu” enyi watu waliopewa Injili, enyi watu mliopewa Taurat, enyi watu mliopewa Zaburi hivi ndivyo Qur’an inavyowasemesha Wakristo, kwahivyo Mkono huu wa Kheri na Baraka ni kuonyesha ya kwamba hakuna Uadui hata kidogo kati ya Uislam na Ukristo, kati ya Waislam na Wakristo.

Ukiisoma Qur’an, Qur’an ina sura nzima inayoitwa suratul Mariam yaani sura ya Mariam, mariam ambae kwa ndugu zetu Wakristo wanamwita “Bikira Maria” sisi kwetu Waislam tunamwita “Mariam Mtakatifu” ni sura nzima inayobeba jina la Mariam, kwahivyo lau Uislam ungelikuwa na Uadui na Ukristo kusinge kuwa na sura inayoitwa sura ya Maria.

Vilevile ndani ya Qur’an kuna sura ya Ruum yani sura ya Roma, Roma ni Wakristo ndani ya Qur’an, na Waislam wanaisoma sura hiyo kila siku ya asubuhi na mchana
Mwisho nimalizie kwa nukta yakwamba Kitendo cha sisi kutoa Mkono wa Kheri ya Krismass kwa ndugu zetu Wakristo watanzania ni kuonyesha yakwamba Uislam ni dini ya Amani, Uislam ni dini inayopenda watu wakae vizuri, Uislam ni dini inayopenda mahusiano mazuri kati yao na ndugu zao Wakristo, 

na kwamba Uislam katika vitu inavyovipiga vita ni kitu kinachoitwa Ugaidi, Uislam na Ugaidi ni vitu viwili tofauti, ni kuontesha ya kwamba Uislam hauna kitu ukatili kwa wasiokuwa Waislam
Kitendo hiki cha kutoa mkono wa Krismas kwa ndugu zetu Wakristo ni kuonyesha kwamba Uislam hauna chinja chinja kwa Wakristo, Uislam hauna ukatili kwa Wakristo, 

Uislam ni amani na maelewano kwa Waislam na wasiokuwa Waislam.mwisho niwatakie ndugu zetu wakristo Watanzania Eid njema, Krismass njema ya kusheherekea kuzaliwa Yesu Kristo au Nabii Issa (a.s).

Na vilevile ni itakie amani serikali yetu ya awamu ya tano ambayo imeweza kutufikisha hapa kwa utulivu na kwa maelewano sisi Waislam Watanzania na Wakristo wa Tanzania, na ninamuomba Mwenyezimungu Serikali hii awape hekima, awape busara ili waendelee kutuongoza kwa salama na kwa amani na 

vilevile mwenyezimungu nchi hii azidi kuboresha maelewano kati yetu sisi Waislam na kati ya ndugu zetu Wakristo, na yeyote ambae anania ya kuleta chokochoko ya kuvunja amani hii, basi chokochoko yake isiweze kuingia katika nchi yetu ya Tanzania na katika taifa hili, Mungu azidishe kulibakiza Taifa hili la Tanzania katika Amani na kisiwa cha amani na mahala pa maelewano.Asanteni sana na Mungu awabariki.

Imetolewa Na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala