Hatimaye baada ya vuta nikuvute, Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kutaka kusimamishwa
mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za
Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Azimio hilo ambalo ni la kwanza kupasishwa na Baraza la Usalama
dhidi ya Israel katika kipindi cha miaka minane, liliungwa mkono kwa
kura 14, huku nchi moja pekee ikijizuia kupiga kura.
Awali azimio hilo lilitazamiwa kupigiwa kura siku ya Alkhamisi,
lakini Misri ambayo iliandaa rasimu ya azimio hilo ikalazimika
kuakhirisha, kufuatia mashinikizo ya Washington.
Hapo jana, Rais mteule wa Marekani, Donald Trump alimpigia simu Rais
wa Misri Abdul Fattah al-Sisi na kuitaka Cairo iakhirishe uwasilishaji
wa rasimu ya azimio hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Aidha kabla ya hapo, Trump alitaka kupigiwa kura ya turufu azimio hilo
la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina
zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel tokea mwaka 1967.
Wakati huo huo, Saeb Uraikat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya
Harakati ya Ukombozi wa Palestina amepongeza hatua ya Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa ya kupasisha azimio hilo na kufafanua kuwa, kura
hiyo ni ushindi na haki kwa Wapalestina. Aidha amemtaka Rais mteule wa
Marekani, Donald Trump kuchagua kati ya "uhalali wa kimataifa" au
kuwaunga mkono "Maghasibu na wenye misimamo mikali".
Inaarifiwa kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala bandia wa
Israel ameingiwa na kiwewe kufuatia hatua hiyo ya Baraza la Usalama la
UN, na kusisitiza kuwa utawala huo khabithi hautayaheshimu maamuzi hayo
ya Umoja wa Mataifa, sambamba na kumlaumu Rais wa Marekani anayeondoka,
Barack Obama kwa kushindwa 'kuilinda Israel'.
No comments:
Post a Comment