Saturday, December 24, 2016

Russia kuimarisha nguvu zake za kijeshi nchini Syria

Mbunge moja wa Russia amesema kuwa, Moscow imeamua kuimarisha nguvu zake za kijeshi nchini Syria.

Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Andrei Nekrasov Naibu wa Mkuu wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Russia DUMA ametangaza habari hiyo na kusema kuwa, Russia inafanya juhudi za kuimarisha kambi yake ya kijeshi katika bandari ya Tartus nchini Syria na hivyo kurejea katika misimamo yake ya zamani ya kumarisha uwepo wake kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Andrei Nekrasov ametoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Russia za kupambana na magenge ya kigaidi na kuongezeza kuwa, kinyume kabisa na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO, Shirikisho la Russia linapigania usalama duniani na mfano wa wazi kabisa ni jinsi jeshi la Russia lilivyopata mafanikio makubwa huko nchini Syria.
Mfumo wa kujilinda kwa makombora wa Russia S400

Naibu wa Mkuu wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Russia ameongeza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo hivi sasa wameelekeza nguvu zao kwenye kuwafurusha magaidi nchini Syria.

Kabla ya hapo Rais Vladimir Putin wa Russia alitaka kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi baina ya Moscow na Damascus kwa nia ya kuimarisha harakati ya jeshi la majini la Russia katika bandari ya Tartus nchini Syria na kuwataka maafisa wa kijeshi wa Russia kuzungumza na maafisa wenzao wa kijeshi wa Syria kuhusu suala hilo kama ambavyo aliitaka pia Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilipe uzito mkubwa jambo hilo.

No comments: