Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na
kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa
kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi.
Mbowe
alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini
Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa
inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa.
Alisema
yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu
wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake.
“Ndugu
zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa
suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale
ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema Mbowe.
Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.”
Katika
hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba imeendelea
kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo mahabusu. Alisema
hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani.
Akijibu
madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani
alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa mbalimbali
vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi haimkamati
mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha sheria.
“Hayo
yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi.
Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa
mjomba wangu tutamkamata.”
Msigwa kidedea
Katika
uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliibuka
kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na asilimia
58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa.
Akitangaza
matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
(Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na
Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na asilimia 88 ya
kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika.
Mnyika alisema kuwa nafasi ya mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa
kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa.
Mnyika
alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au hapana
kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa kuweka
wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya chama.
“Hivyo
Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea wote
na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata
kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo" Alisema Mnyika
No comments:
Post a Comment