Friday, November 4, 2016

Johnson: Magaidi 130 wa Uingereza wameuawa nchini Syria

Boris Johnson ameliambia Bunge la Uingereza kwamba, karibu Waingereza 850 wamekwenda Syria na kujiunga na kundi la kigaidi la Daesh tangu mwaka 2011 na kwamba karibu nusu yao wamerejea nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema kuwa, idadi ya raia wa nchi hiyo wanaojiunga na kundi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi huko Syria imepungua na kuongeza kuwa, propaganda za kundi la kigaidi la Daesh zimepungua kwa asilimia 70 kuanzia mwaka jana wa 2015.
Boris Johnson amesisitiza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh linadhoofika siku baada ya siku na kwamba kundi hilo litaangamizwa kikamilifu baada ya kukombolewa mjini wa Raqqa nchini Syria ambayo ndio ngome kuu ya magaidi hao.
 
  Serikali ya Syria na washirika wake wanapambana na wapiganaji wa makundi ya kigaidi hususan Daesh na Jabhatu Nusra ambayo yaliingia nchini humo kwa msaada wa nchi kama Marekani, Saudi Arabia, Uturuki na washirika wao

Mogherini: Ni haki ya watu wa Ulaya kuisusia Israel

Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya amesema kuwa ni haki ya watu wa nchi za bara hilo kuisusia Israel. 

Federica Mogherini ambaye alikuwa akijibu maswali ya mwakilishi wa Ireland katika Bunge la Ulaya kuhusu harakati ya kuususia utawala wa Kizayuni wa Israel (BDS) amesema kuwa, haki ya uhuru wa kujieleza watu wanaotaka kushiriki katika kuisuia Israel inapaswa kuheshimiwa. 
 
Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, Ulaya inaunga mkono na kutetea uhuru wa kujieleza wa jumuiya mbalimbali ikiwemo ile ya kuisuia Israel.

Federica Mogherini ameyasema hayo akijibu maswali ya mwakilishi wa Ireland katika Bunge la Ulaya, Martina Anderson ambae ni miongoni mwa watetezi wa haki za Wapalestina. 

Anderson alimtaka Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya, Bi Mogherini aweke wazi misimamo yake kuhusu harakati ya kuisusia Israel barani Ulaya maarufu kwa kifupi kwa jina la BDS.
 
Msimamo wa wazi wa Federica Mogherini wa kutetea haki ya watu wa Ulaya kuisusia Israel umekaribishwa kwa mikono miwili na harakati mbalimbali za kupigania ukombozi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Russia: Marekani inalenga makazi ya raia Mosul, Iraq

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani na washirika wake yanalenga zaidi makazi ya raia katika mji wa Mosul nchini Iraq.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amesema kuwa, mashambulizi ya Marekani na washirika wake katika mji wa Mosul katika mkoa wa Neinawa nchini Iraq yanawalazimisha raia kukimbia nyumba na makazi yao. Zakharova amesisitiza kuwa, Russia ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya raia wa kawaida katika mji wa Mosul.
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi ameashiria harakati za Marekani na washirika wake huko Mosul na kusema kuwa, licha ya kutumia jina kubwa la eti muungano wa kupambana na ugaidi, Marekani na washirika wake hawajafanya lolote katika operesheni ya kukomboa mji wa Mosul unaoshikiliwa na magaidi wa Daesh.

Al Abadi amesisitiza kuwa, serikali ya Iraq haihitaji muungano wa huo na kwamba Wairaqi wana uwezo wa kukomboa ardhi na nchi yao wenyewe.

Jeshi la Iraq na makundi ya kujitolea ya wananchi tarehe 17 Oktoba yalianza operesheni kubwa ya kukomboa mji wa Mosul ambao unakaliwa na kundi la kigaidi la Daesh. Magaidi wa kundi hilo sasa wanazingirwa kila upande na operesheni hiyo inaendelea kwa mafanikio.