Friday, November 4, 2016

Russia: Marekani inalenga makazi ya raia Mosul, Iraq

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani na washirika wake yanalenga zaidi makazi ya raia katika mji wa Mosul nchini Iraq.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amesema kuwa, mashambulizi ya Marekani na washirika wake katika mji wa Mosul katika mkoa wa Neinawa nchini Iraq yanawalazimisha raia kukimbia nyumba na makazi yao. Zakharova amesisitiza kuwa, Russia ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya raia wa kawaida katika mji wa Mosul.
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi ameashiria harakati za Marekani na washirika wake huko Mosul na kusema kuwa, licha ya kutumia jina kubwa la eti muungano wa kupambana na ugaidi, Marekani na washirika wake hawajafanya lolote katika operesheni ya kukomboa mji wa Mosul unaoshikiliwa na magaidi wa Daesh.

Al Abadi amesisitiza kuwa, serikali ya Iraq haihitaji muungano wa huo na kwamba Wairaqi wana uwezo wa kukomboa ardhi na nchi yao wenyewe.

Jeshi la Iraq na makundi ya kujitolea ya wananchi tarehe 17 Oktoba yalianza operesheni kubwa ya kukomboa mji wa Mosul ambao unakaliwa na kundi la kigaidi la Daesh. Magaidi wa kundi hilo sasa wanazingirwa kila upande na operesheni hiyo inaendelea kwa mafanikio.

No comments: