Idadi ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa
imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo
kutotekelezwa nchini humo tangu mwaka 1994.
Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili
kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais
Magufuli aliibuka mshindi.
Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu
Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya
pili nchini Tanzania, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri
adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.
Ofisa
Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, amesema Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa
haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za
walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo.
Hata hivyo, Mponezya amesema kuwa, watetezi wengi wa haki za binadamu
nchini Tanzania wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha
haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya
wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa,
jambo linalowaathiri kisaikolojia.