Sunday, March 16, 2014

Bodaboda 400 waandamana hadi ofisi za Chadema Kinondoni

Zaidi ya waendesha pikipiki na bajaji 400 wameandamana kuelekea Makao Makuu ya Chadema, yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kupinga kitendo cha kukatazwa kuingiza vyombo vyao vya moto katikati ya Jiji. 
 
Vijana hao wakiwa na vyombo vyao vya usafiri pamoja na mabango yenye ujumbe tofauti walifika kwenye ofisi hizo jana asubuhi wakitokea maeneo tofauti jijini.
 
Baadhi ya mabango yao yalisomeka hivi ‘ubakaji, wizi utaongezeka.
Baada ya kuwasili kwenye ofisi hizo, madereva hao walianza kuimba ‘tunamtaka Rais wetu, tunamtaka Rais wetu, peoples power”, wakiimaanisha Dk. Wilbroad Slaa.
 
Wakati nyimbo hizo zikiendelea nje ya ofisi hizo, Dk. Slaa alikuwa hayupo na alipowasili alipokelewa na kelele ‘Rais wetu, Rais wetu, Rais wetu’. Dk. Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema, mara baada ya kushuka kwenye gari lake aliwatuliza vijana hao na kuwaeleza kuwa baada ya kupata taarifa zao aliwasiliana na vyombo vya dola.
 
“Nimewasiliana na ngazi zote za polisi akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, kamanda wa jeshi la polisi mkoa na mkuu wa upelelezi na kukubaliana nao hakuna mabomu,” alisema na kuongeza:
 
“Mtu anapokimbilia hapa maana yake yupo katika usalama, Chadema isiyopenda kumwaga damu tunaweza kupata suluhu bila mabomu,” alisema.
 
Dk. Slaa alisema amezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na kwamba amekubali kukutana nao Jumatatu wiki ijayo

7 Wafariki katika msongamano wa kutafuta kazi Nigeria

Watu wasiopungua saba wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika mji mkuu wa Nigeria Abuja kufuatia msongamano wa maelfu ya watu. 

Msongamano huo ulijiri Jumamosi wakati watu walipokusanyika kuajiriwa katika idara ya uhamiaji. Zoezi hilo lilikuwa likifanyika katika uwanja wa kitaifa wa michezo Abuja. 

Walioshuhudia wanasema mkanyagano ulijiri pale watu walipojaribu kufika katikati ya uwanja ambapo kulikuwa na mlango moja tu uliokuwa wazi katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 60,000. 

Bado haijabainika idadi ya watu waliokuwa ndani ya uwanja wakati wa msongamano huo. Idara ya uhamiaji Nigeria ilikuwa inaendesha zoezi hilo katika maeneo kadhaa nchini humo.

Ukosefu wa ajira ni changamoto kubwa katika nchi hiyo tajiri kwa mafuta ya petroli  magharibi mwa Afrika ambapo imearifiwa kuwa asilimia 37.5 ya vijana walio chini ya umri wa
miaka 25 hawana kazi.irib