Serikali ya Marekani kwa mara nyingine tena imesema
kuwa, chaguo bora kabisa kwa Washington la kuamiliana na Iran ni kupitia njia
za kidiplomasia na kwamba, nguvu za kijeshi katu haziwezi kusimamisha miradi ya
nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wendy Sherman, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani ambaye pia ni mkuu wa timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Marekani
amesema bayana kwamba, njia itakayokuwa na taathira nzuri zaidi ni ya
kidiplomasia.
Amedai kuwa, hatua yoyote ile ya kijeshi ya Israel au Marekani
dhidi ya Iran itaweza tu kuirejesha nyuma Iran miaka miwili au mitatu hivi.
Sherman alikuwa akisema hayo katika mazungumzo yake na ujumbe wa kidiplomasia
wa Israel ikiwa ni katika juhudi za Washington za kuifikishia Israel na lobi za
Kizayuni ujumbe wake kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko
Lausanne Uswisi kati ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Marekani, Uingereza,
Ufaransa, Russia, China pamoja na Ujerumani.