Sunday, October 11, 2015

Urusi yaendeleza mashambulizi dhidi ya IS Syria

Mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Urusi yameyalenga maeneo 55 ya kundi la Dola la Kiislamu-IS nchini Syria katika kipindi cha saa 24 zilizopita. 
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa mashambulizi ya hivi akribuni yamefanywa kwenye majimbo ya Damascus, Aleppo, Hama, Raqa na Idlib na kuharibu kambi 29 za mafunzo kwa magaidi, maeneo 23 ya kijeshi, vituo viwili vya kamandi na ghala la risasi. 
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov, amesema leo kuwa Urusi itazungumza na wizara ya ulinzi ya Marekani kuhusu kujiepusha na ajali kwenye anga ya Syria, wakati ambapo muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani yanaendesha operesheni tofauti nchini humo. 
Wakati huo huo, muungano huo wa kijeshi jana umefanya mashambulizi 25 ya anga yakiyalenga maeneo ya IS nchini Iraq. Mashambulizi hayo yamefanyika karibu na Al-Hasakah, Ar Raqqah, Manbij na Mar'a na kuharibu magari na jengo la IS.chanzo dw

Rais Kikwete azindua miundombinu ya gesi Mtwara

Rais Kikwete leo amezindua miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam kupitia Somanga, katika hafla iliyofanyika katika eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Katika hotuba yake Rais Kikwete amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu kuelekea katika taifa lenye uchumi wa kati kwa kuimarisha huduma za nishati ya umeme pamoja na uchumi katika Nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda kwa kuwa gesi hiyo itamaliza kabisa tatizo la umeme.
Katika uzalishaji wa umeme, Rais Kikwete amewaagiza watendani wa shirika la umeme nchini TANESCO na lile la mafuta TPDC kuwa makini katika mchakato wa manunuzi kwa kufuata sheria ili matatizo yaliyowahi kulikumba taifa hili kutokana na ukiukwaji wa taratibu mwaka 2006 yaliyosababishwa na uhaba wa umeme, yasijirudie tena.
Rais Kikwete licha ya kuishukuru serikali ya China kuwa tayari kujenga miundombinu hiyo, ameziagiza mamlaka husika kuhakikiksha kwamba zinatoa huduma muhimu za jamii ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na barabara kwa wakazi wa Mtwara ili wanufaike na gesi hiyo.
Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Tanzania Dkt. James Mataragio ameeleza kuwa miundombinu hiyo imekamilika na tayari gesi imeshaanza kusukumwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Dkt Mataragio amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu dola za kimarekani bilioni 1.53 sawa na trillion 2.926 za kitanzania ikiwa ni pamoja na gharama ambazo hazikuwa ziko nje ya gharama halisi ya miundombinu hiyo.
Amesema kuwa asilimia 95 ya gharama hizo zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China huku asilimia 5 ikitoka serikalini.
Akizungumzia faida za miundombinu hiyo, Dkt Mataragio ametaja faida kadhaa za gesi hiyo ikiwa ni pamoja na kutumika katika uzalishaji wa umeme jambo litakaloifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika.
Ametaja faida nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza pato la taifa kutokana na uuzaji wa gesi hiyo nje ya nchi, kuokoa fedha za kigeni ambazo hutumika kuagizia mafuta kutoka nje ya nchi, kukuza uchumi kupitia ukuzaji wa sekta ya viwanda, kuongeza mapato ya halmashauri kupitia mirabaha pamoja na kuchochea utafiti wa mafuta na gesi.
Amesema miundombinu hiyo itakuwa na uwezo wa kusukuma futi za ujazo milioni 784 kwa siku ifikapo mwaka 2020, ambapo kwa sasa inasukuma futi za ujazo milioni 80 pekee.
Akimkaribisha Rais Kikwete, waziri wa Nishati na madini George Simbachawene, amesema kuwa huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwamba serikali ina mpango wa kujenga mitambo ya umeme mkoani Mtwara itakayozalisha zaidi ya Mega Watt 600 kwa ajili ya mikoa ya kusini.
“Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana kwa jitihada zako, kuna watu wanabeza wanahoji eti utatuachaje, mimi nawaambia kwamba ulipoingia ulitukututa na gesi ya futi za ujazo trillion 8, lakini unatuacha na futi za ujazo trillion 52”, amesema Simbachawene na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utazalisha ajira zaidi ya 1363 katika eneo hilo la Mtwara.chanzo eatv

Mogherini: Ulaya imekuwa msambazaji wa ugaidi

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, Ulaya imegeuka na kuwa msambazaji wa ugaidi katika nchi zinazokabiliwa na migogoro zikiwemo Iraq na Syria.
Federica Mogherini amebainisha kwamba, ukweli wa mambo ni kuwa bara la Ulaya ndilo linaosambaza ugaidi zaidi. Mogherini ameongeza kuwa, Iraq na Syria zinakabiliwa na ongezeko la magaidi wa kigeni hususan kutoka barani Ulaya na kwamba, viongozi wa madola ya Magharibi hadi sasa hawajaweza kuzuia wimbi la magaidi hao wa Ulaya wanaoingia Syria wakipitia katika ardhi ya Uturuki.
Hivi karibuni kulitolewa ripoti iliyoonesha kuwa, wapiganaji elfu tano kutoka katika nchi mbalimbali za Ulaya wanapigana bega kwa bega na makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq. 
Mwezi uliopita pia gazeti la New York Times liliwanukuu maafisa usalama wa Marekani wakisema kwamba, kuna zaidi wapiganaji elfu thelathini kutoka nchi zaidi ya 100 waliojitolea kwa ajili ya kwenda kupigana chini ya mwavuli wa makundi ya kigaidi kama lile la Daesh.Chanzo Irib

Velayati:Tume ya kuchunguza maafa ya Mina ni lazima

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya siasa amesema Saudi Arabia inawajibika kulinda usalama wa Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Dakta Ali Akbar Velayati amesema kuwa Iran itafuatilia kisheria kadhia ya wahusika wa maafa yaliyotokea Mina nchini Saudi Arabia wakati wa ibada ya Hija na kuongeza kuwa, Riyadh inawajibika kushirikiana na kamati ya kuchunguza ukweli ili kubaini sababu cha maafa hayo na nani walizembea au kusababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji. 
Amesisitiza kuwa wahusika wa maafa hayo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema kwa mujibu wa misingi ya Kiislamu na kibinadamu na vilevile makubaliano ya Vienna nchi mwenyeji inapaswa kulinda usalama wa wageni hivyo Saudia inapaswa kuwajibika katika suala la maafa ya Mina. 
Dakta Velayati amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu italifuatilia suala hilo na maafa ya Mina kisheria. Maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kutoka pembe mbalimbali za dunia wakiwemo mahujaji 465 wa Iran walifariki dunia katika mkanyagano uliotokea Mina, Saudi Arabia katika siku ya Idul Adh'ha wakati wa ibada ya kumpiga mawe shetani.chanzo irib