Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema katika
kuhakikisha Serikali inapambana na uhalifu, Jeshi la Polisi limeanza
ukaguzi maalumu wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu
ili kufuatilia matukio mbalimbali.
“Kutokana na majambazi kubuni
mbinu mpya kila siku, ikiwamo ya kutumia bodaboda kuvamia benki na
wanaotoka benki na kuwapora fedha, kuanzia sasa bodaboda, hasa aina ya
boxer zitasimamishwa wakati wowote na kupekuliwa,” alisema Kitwanga
katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es
Salaam.
Alisema polisi wameweka ulinzi maalumu na waendesha
bodaboda watakaooneka kupakia kitu chochote na kukiweka mbele (katika
tenki la mafuta) au kiti cha nyuma, watasimamishwa na kupekuliwa kwa
maelezo kuwa maeneo hayo ndiyo hutumika kuficha silaha.
“Tunaomba wananchi watuvumilie kipindi hiki tukipambana na bodaboda kutokomeza uhalifu,” alisema.
Katika
miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya
wananchi kuvamiwa na kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya
kuzichukua benki huku wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa
taarifa za wateja.
Mara zote majambazi hutumia bodaboda
kufanikisha uhalifu huo, huku wakiwa na silaha ambazo huzitumia
kutishia, kujeruhi na wakati mwingine kuua.
Tukio la hivi karibuni
ni la Desemba 28 mwaka jana, ambako majambazi waliokuwa katika bodaboda
walimvamia meneja wa operesheni wa kampuni ya simu za mkononi ya
Zantel, Gabriel Raphael na kumpora Sh10 milioni na kumuua kwa risasi.
Kuhusu
ujambazi huo, Kitwanga alisema watu wanaovamiwa na kuporwa fedha, wengi
hutokea katika benki za ndani si za nje.“... Hii inatokana na utaratibu
wa malipo katika benki hizi. Kwa mfano, benki za nje ukiwa na hundi
inapitiwa na watu wachache tofauti na benki za ndani ambazo hupitiwa na
watu wengi.”
“Inawezekana katika mlolongo huo wa benki za ndani
kukawa na wafanyakazi wanaoshirikiana na majambazi. Tunachokifanya sasa
ni kuongeza ulinzi tu wa askari.”
Kuhusu CCTV, Kitwanga ambaye pia
ni mbunge wa Misungwi alisema teknolojia hiyo itasaidia kubaini matukio
ya uhalifu na kwamba tayari Serikali imeshazungumza na China kuhusu
upatikanaji wa kamera hizo, “Ufungaji wa utaanza mwaka ujao wa fedha
unaoanza Julai na tutaanzia Dar es Salaam.”
Alisema Jeshi la
Polisi lina askari wachache ambao hawawezi kuwapo kila eneo, hivyo
mpango wa kuweka kamera hizo ni kuhakikisha kila jambo linafuatiliwa kwa
ukaribu.
“Wapo waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika katika matukio
ya kuwapiga watu risasi na kuwapora fedha. Baadhi yao wamekiri kuhusika
na wengine wamekana,” alisema Kitwanga.
Alipoulizwa silaha
zinazotumika zinatoka wapi, alisema, “wanazopewa raia kihalali
hazitumiki katika matukio haya. Ni zile zinazoingia nchini kinyemela.”
Kuvamiwa vituo vya polisi
Alisema
matukio ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi yana harufu ya ugaidi:
“Tanzania ugaidi haujakomaa na magaidi hawajawa na nguvu. Wanachofanya
ni kuvamia kituo cha polisi, kuchukua silaha na kuzitumia kufanya
uhalifu kupata fedha ili kuendesha maisha yao. Kuna dalili kubwa kwamba
huu ni ugaidi.”
Alisema licha ya Serikali kuwakamata, wapo
wanaoendelea kuingia nchini na ili kumaliza suala hilo ni lazima uwekwe
mpango wa muda mrefu.
“Kwa sasa tunaendelea kujadiliana kuhusu
mpango wa kutambua raia wetu na wanafunzi katika shule mbalimbali.
Lazima tujue wangapi wameacha shule na wamekwenda wapi. Ugaidi ukikomaa
katika nchi unakuwa tatizo kubwa.
“Magaidi hawatengenezwi nchini,
wanatoka hapa (Tanzania) wanakwenda Somalia wanafundishwa na kisha
wanarudi kufanya ugaidi. Lazima tutambue raia waliotoka Tanzania
walikwenda nchi gani na kwa sababu gani. Bado tunajadiliana tuone
tutaliendesha vipi jambo hili.”
Kitwanga alisema ili polisi iweze
kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima iwe na mfumo imara kuanzia makao
makuu hadi ngazi ya chini (ulinzi shirikishi), akisema moja ya
changamoto alizokumbana nazo baada ya kuteuliwa kuwa waziri ni dosari
katika mfumo wa utendaji kazi.
Alisema nchi ina polisi 45,000 na kati yao wanaoishi kambini ni 10,000 tu na kwamba kuishi uraiani kunashusha nidhamu.
“Hii
ni changamoto kwa sababu ukitaka kuwakusanya wote hutaweza maana wengi
wanaishi uraiani. Rekodi za kimataifa askari mmoja anapaswa kulinda watu
350. Kwa Afrika askari mmoja analinda kati ya watu 500 hadi 700 lakini
kwa Tanzania analinda watu 1,000 hadi 1,200,” alisema.
Alisema ili
kufikia rekodi za kimataifa, nchi inapaswa kuwa na askari kati ya
95,000 hadi 100,000 na idadi hiyo itakuwa ikiongezeka kila mwaka. Mwaka
huu askari 3,600 watahitimu mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.