Sunday, January 17, 2016

Kitwanga atangaza vita ya bodaboda

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, CharlesWaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema katika kuhakikisha Serikali inapambana na uhalifu, Jeshi la Polisi limeanza ukaguzi maalumu wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu ili kufuatilia matukio mbalimbali.

“Kutokana na majambazi kubuni mbinu mpya kila siku, ikiwamo ya kutumia bodaboda kuvamia benki na wanaotoka benki na kuwapora fedha, kuanzia sasa bodaboda, hasa aina ya boxer zitasimamishwa wakati wowote na kupekuliwa,” alisema Kitwanga katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam.

Alisema polisi wameweka ulinzi maalumu na waendesha bodaboda watakaooneka kupakia kitu chochote na kukiweka mbele (katika tenki la mafuta) au kiti cha nyuma, watasimamishwa na kupekuliwa kwa maelezo kuwa maeneo hayo ndiyo hutumika kuficha silaha.

“Tunaomba wananchi watuvumilie kipindi hiki tukipambana na bodaboda kutokomeza uhalifu,” alisema.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuvamiwa na kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzichukua benki huku wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa taarifa za wateja.

Mara zote majambazi hutumia bodaboda kufanikisha uhalifu huo, huku wakiwa na silaha ambazo huzitumia kutishia, kujeruhi na wakati mwingine kuua.
 
Tukio la hivi karibuni ni la Desemba 28 mwaka jana, ambako majambazi waliokuwa katika bodaboda walimvamia meneja wa operesheni wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Gabriel Raphael na kumpora Sh10 milioni na kumuua kwa risasi.

Kuhusu ujambazi huo, Kitwanga alisema watu wanaovamiwa na kuporwa fedha, wengi hutokea katika benki za ndani si za nje.“... Hii inatokana na utaratibu wa malipo katika benki hizi. Kwa mfano, benki za nje ukiwa na hundi inapitiwa na watu wachache tofauti na benki za ndani ambazo hupitiwa na watu wengi.”

“Inawezekana katika mlolongo huo wa benki za ndani kukawa na wafanyakazi wanaoshirikiana na majambazi. Tunachokifanya sasa ni kuongeza ulinzi tu wa askari.”

Kuhusu CCTV, Kitwanga ambaye pia ni mbunge wa Misungwi alisema teknolojia hiyo itasaidia kubaini matukio ya uhalifu na kwamba tayari Serikali imeshazungumza na China kuhusu upatikanaji wa kamera hizo, “Ufungaji wa utaanza mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai na tutaanzia Dar es Salaam.”
 
Alisema Jeshi la Polisi lina askari wachache ambao hawawezi kuwapo kila eneo, hivyo mpango wa kuweka kamera hizo ni kuhakikisha kila jambo linafuatiliwa kwa ukaribu.

“Wapo waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika katika matukio ya kuwapiga watu risasi na kuwapora fedha. Baadhi yao wamekiri kuhusika na wengine wamekana,” alisema Kitwanga.

Alipoulizwa silaha zinazotumika zinatoka wapi, alisema, “wanazopewa raia kihalali hazitumiki katika matukio haya. Ni zile zinazoingia nchini kinyemela.”

Kuvamiwa vituo vya polisi
Alisema matukio ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi yana harufu ya ugaidi: “Tanzania ugaidi haujakomaa na magaidi hawajawa na nguvu. Wanachofanya ni kuvamia kituo cha polisi, kuchukua silaha na kuzitumia kufanya uhalifu kupata fedha ili kuendesha maisha yao. Kuna dalili kubwa kwamba huu ni ugaidi.”

Alisema licha ya Serikali kuwakamata, wapo wanaoendelea kuingia nchini na ili kumaliza suala hilo ni lazima uwekwe mpango wa muda mrefu.

“Kwa sasa tunaendelea kujadiliana kuhusu mpango wa kutambua raia wetu na wanafunzi katika shule mbalimbali. Lazima tujue wangapi wameacha shule na wamekwenda wapi. Ugaidi ukikomaa katika nchi unakuwa tatizo kubwa.

“Magaidi hawatengenezwi nchini, wanatoka hapa (Tanzania) wanakwenda Somalia wanafundishwa na kisha wanarudi kufanya ugaidi. Lazima tutambue raia waliotoka Tanzania walikwenda nchi gani na kwa sababu gani. Bado tunajadiliana tuone tutaliendesha vipi jambo hili.”

Kitwanga alisema ili polisi iweze kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima iwe na mfumo imara kuanzia makao makuu hadi ngazi ya chini (ulinzi shirikishi), akisema moja ya changamoto alizokumbana nazo baada ya kuteuliwa kuwa waziri ni dosari katika mfumo wa utendaji kazi.

Alisema nchi ina polisi 45,000 na kati yao wanaoishi kambini ni 10,000 tu na kwamba kuishi uraiani kunashusha nidhamu.

“Hii ni changamoto kwa sababu ukitaka kuwakusanya wote hutaweza maana wengi wanaishi uraiani. Rekodi za kimataifa askari mmoja anapaswa kulinda watu 350. Kwa Afrika askari mmoja analinda kati ya watu 500 hadi 700 lakini kwa Tanzania analinda watu 1,000 hadi 1,200,” alisema.

Alisema ili kufikia rekodi za kimataifa, nchi inapaswa kuwa na askari kati ya 95,000 hadi 100,000 na idadi hiyo itakuwa ikiongezeka kila mwaka. Mwaka huu askari 3,600 watahitimu mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.    

No comments: