|
Profesa Makame Mnyaa Mbarawa |
MIKAKATI ya serikali ya kutoa wataalamu wengi wa sayansi imeendelea
kutetekelezwa kwa kasi, ambapo imetia saini mikataba kusambaza huduma za
mtandao kwenye shule mbalimbali nchini.
Mikataba hiyo iliyotiwa saini jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, iko
miwili ya kupeleka huduma za mawasiliano vijijini na kuunganisha mtandao
wa intaneti katika shule utakaogharimu sh. bilioni 26.28.
Katika mikataba hiyo, serikali imeonya kuwa itazifuta kampuni ambazo
zitashindwa kutekeleza makubaliano ya kufikisha mawasiliano kwa wakati
katika vijiji 480 vilivyoainishwa.
Onyo hilo la serikali linatokana na kampuni hizo kushindwa kutekeleza
makubaliano ya mkataba wa kupeleka huduma za mawasiliano vijijini,
ambapo nyingi zimetekeleza kwa asilimia 50 tu.
Akizungumza wakati wa kutia saini mikataba hiyo, Profesa Mbarawa alisema
awamu ya tatu ya kupeleka mawasiliano vijijini utahusisha kata 102
ambapo vijiji 480 vitanufaika nayo.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ulihusisha kata 52, ambao
ulitekelezwa mwaka 2013 na umekamilika kwa asilimia 99.05 na awamu ya
pili ilihusisha kata 86 na ulitakiwa kukamilika mwaka jana na hadi sasa
umetekelezwa kwa asilimia 50.
“Awamu ya kwanza kuna kata nne kati ya 52 ambazo bado hazijamazilizika,
jambo ambalo halikubaliki na kama mtu ameshindwa kutekeleza mkataba wake
afungiwe na katika hili sitakubali,” alisema.
Mkataba wa mradi huo ambao utahusisha kata 102 na kugharimu sh. bilioni
14.02 umesainiwa kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) na kampuni
za utoaji huduma za mawasiliano.
Kampuni zilizotia saini mkataba wa utoaji huduma ya mawasiliano kwa
awamu ya tatu na idadi ya kata katika mabano ni Tigo (42), Vodacom (36),
TTCL (19) na Airtel (5).
Alisema bado kuna changamoto kubwa ya mawasiliano katika maeneo ya
vijijini, hivyo kuzitaka kampuni hizo kuhakikisha zinatekeleza mikataba
ili kila mwananchi apate huduma popote alipo.
Waziri huyo alisema katika kuhakikisha huduma ya mawasiliano inawafikia
wananchi wote, serikali ilianzisha utoaji wa ruzuku kwa kampuni
zinazotoa husika ili kupeleka mawasiliano kwenye maeneo yenye uchumi
hafifu.
Alisema serikali kupitia UCAF itatoa ruzuku ya asilimia 100 ambayo
inatolewa kulingana na eneo yakiwemo maeneo ya mipakani ambayo ni lazima
yawe na mawasiliano wakati wote ili kuimarisha ulinzi na usalama.
Alisema UCAF ilianzishwa mwaka 2006 ambapo hadi mwaka 2010 anaingia
katika wizara hiyo hakukuwa na kazi yoyote iliyotekelezwa ambapo
alilazimika kubadilisha uongozi jambo ambalo limeleta mafanikio na sasa
mawasiliano yanaendelea kufika kwa wananchi.
“Ni mafanikio makubwa yaliyopatikana itakuwa kichekesho kwa waziri
atakayekuja ashindwe kufanya vizuri zaidi, na akishindwa kuna tatizo kwa
sababu sasa teknolojia imebadilika,” alisema.
Awali, Mtendaji Mkuu wa UCAF, Mhandisi Peter Ulanga, alisema mbali na
kutia saini mkataba na kamapuni za mawasiliano, pia waliingia mkataba na
kamapuni ya Avanti inayotoa huduma za mtandao wa intaneti kwa ajili ya
kuziunganishia shule 250 za serikali.
Pia alisema wataanzisha vituo 25 vya kufundishia walimu wa masomo ya
teknolojia ya habari na mawasiliano, mradi unaotarajiwa kukamilika ndani
ya mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya UCAF, Profesa John Nkoma,
aliwaomba wananchi wabadilike na kutumia huduma ya intaneti kwa faida na
si vinginevyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk.
John Mngodo, alisema huduma ya kuunganisha intaneti katika shule za
serikali itasaidia kuboresha elimu.
l