Saturday, July 30, 2016

Hizbullah: Saudia inarejesha uhusiano na Israel bila gharama

Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amekosoa vikali safari ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Saudi Arabia katika utawala wa Kizayuni wa Israel wiki jana na kusisitiza kuwa Riyadh inahuisha uhusiano wake na Tel Aviv pasina na kuzingatia maslahi ya Wapalestina.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema utawala wa Aal-Saud unatoa mfano mbaya kwa mataifa mengine na haswa ya Kiislamu katika kufufua uhusiano wake na utawala haramu wa Israel. 


Akizungumza kwa njia ya televisheni katika marasimu ya kukumbuka kifo cha Ahmad Zahri, mmoja wa makamanda wa harakati hiyo ya Kiislamu, Sayyid Nasrullah amesema sio jambo la mbali kwa utawala wa Riyadh katika hatua yake ya pili ya kufufua uhusiano wake na Israel, kutangaza kuutambua rasmi utawala huo bandia unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapelestina.

Matamshi ya Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon yanajiri siku chache baada ya ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya Riyadh ukiongozwa na Jenerali Anwar Eshki, kamanda mkuu wa zamani wa Saudia kuutembelea utawala ghasibu wa Israel na kukutana na kufanya mazungumzo na wakuu wa utawala huo katili wakiwemo wabunge wa bunge la Knesset.


Eshki ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kituo cha Mafunzo ya Kiistratejia na Sheria cha Mashariki ya Kati kilichoko Jeddah alikutana na kufanya mazungumzo na Dore Gold, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel na Mshirikishi wa Masuala ya Harakati za Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu Yoav Mordechai miongoni mwa maafisa wengine wa utawala huo wa Kizayuni.

Adhabu kali kwa wanawake wanaovaa vazi la hijabu Bulgaria

Serikali ya Bulgariia imetangaza kuwa itawatoza faini wanawake wa Kiislamu wanaoheshimu kikamilifu vazi lao la hijabu. 

Serikali ya Bulgaria imetangaza kuwa itatoa adhabu na kuwatoza faini ya euro 150 kwa mara ya kwanza na euro 500 kwa mara ya pili kwa wanawake wanaovaa hijabu kamili ya Kiislamu katika maeneo ya umma. 


Kiasi hicho cha pesa kimetajwa kuwa ni zaidi ya mshahara wa kiwango cha  wastani wa kila mwezi nchini Bulgaria.Kupigwa marufuku vazi la hijabu nchini Bulgaria kumewafanya wanawake Waislamu kutoka majumbani mwao kwa nadra sana. 

Katika kipindi cha wiki za hivi karibuni viongozi wa serikali ya Bulgaria wamechukua hatua kali dhidi ya wanawake wa Kiislamu nchini humo.

Bahrain yaendeleza ubabe, yamkamata kiongozi mwingine wa Kiislamu

Licha ya makelele ya jamii ya kimataifa na watetezi wa haki za binadamu, utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain umemtia nguvuni kiongozi mwingine wa Kiislamu.

Habari zinasema kuwa, maafisa usalama wa utawala wa Manama wamevamia makazi ya Seyyid Majid al-Mashaal, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Bahrain mapema leo na kumkamata msomi huyo mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa haujatoa taarifa au sababu za kumkamata mwanachuoni huyo wa Kiislamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.Haya yanajiri siku chache baada ya utawala wa Manama kuakhirisha kesi dhidi ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim, msomi mtajika wa Kiislamu nchini humo iliyotazamiwa kuanza kusikilizwa Jula 27. 


Siku moja kabla ya kesi hiyo, taarifa ya wasomi wa Kiislamu nchini Bahrain ilisema kuwa, mashitaka anayolimbikiziwa Ayatullah Qassim ambaye utawala wa Manama umemvua uraia ni ya kubuni na wala hayana mashiko na kwamba kesi dhidi yake inakiuka katiba, haki za binadamu zilizoanishwa katika sheria za nchi hiyo na hata za kimataifa.

Mwezi uliopita wa Juni, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza alilaani vikali uamuzi wa mahakama ya rufaa ya Bahrain wa kuidhinisha hukumu iliyotolewa dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Al-Wifaq na kuongeza adhabu hiyo ya kifungo hadi miaka tisa. 

Sheikh Salman alitiwa nguvuni mwezi Disemba mwaka 2014 baada ya kutoa hotuba kadhaa za kupinga siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Khalifa.