|
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akisisitiza jambo katika Kikao na Waandishi wa Habari katika Kuadhimisha siku ya Kuzaliwa (Maulid) ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) jijini Dar es salaam. |
TAARIFA KWA UMMA
Ndugu zangu Waislam wenzangu Asalam Alaykum Warahmatullah
Wabarakatu,Amani ya Mwenyezimungu iwe kwenu wote. Napenda kwanza niwape hongera
kwa waisla wote watanzania kwa tukio hili la kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume
Muhammad (s.a.w.w), napenda niwape Hongera kwa sababu ya tukio hili kubwa la
kuzaliwa kiongozi huyu.
Kama ambayo nawapa hongera Watanzania wote Waislam na
wasiokuwa waislam kwa kushirikiana na watanzania wenzao katika tukio hili la
Maulid, katika tukio hili la kuzaliwa Mtume wa Huruma, Mtume wa Upendo, mtume
wa Mapenzi, Mtume wa Maelewano, Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Katika siku hii ya Maulid na katika kuadhimisha kuzaliwa kwa
Mtume huyu napenda kuzungumza jambo moja ambalo ni nzito na la muhimu, na sisi
kama watanzania wote kwa ujumla Waislam na wasiokuwa waislam tunalihitajia
tukio hilo, au tunayahitajia maelezo hayo yanayohusiana na Mtume wetu Mtume
Muhammad (s.a.w.w).
Tukio hili napenda nimesome Mtume kwenye upande wa kazi moja
kubwa ambayo sisi kama watanzania tunahitajia nayo ni kazi ya Kuwaunganisha
watu,Moja ya kazi kubwa muhimu ambayo mtume huyu tunaemkumbuka Maulid na
kuzaliwa kwake leo,moja ya kazi kubwa nyeti na muhimu aliyoifanya ilikuwa ni
kuwaunganisha watu.
|
Hawa ni baadhi ya waandishi wa habari upande wa Television wakiwa makini kumsikiliza Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala. |
Mtume Muhammad (s.a.w.w) yeye sambamba na mitume wengine wote
waliopita,moja ya kazi yao kubwa ilikuwa ni “Tauhidil Kalima” ni Tauhidil Umma”
ilikuwa ni kuwaunganisha watu, kwanzia Mtume Adam (a.s) mpaka kufikia Mtume
Ibrahim (a.s), mpaka kufikia Mtume Mussa (a.s), Mpaka kufikia Mtume Issa /
Yeu(a.s) na hatimae kufikia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), hao wote moja ya
mafunzo yao muhimu na makubwa ilikuwa ni kuwafanya watu wawe kitu kimoja.
Hakuna
Mtume aliekuja kuja kufundisha mafundisho ya kuwatenga watu, hakuna mtume wa
Mungu aliyekuja kuwafunza watu kutengana, bali watu wote walikuja kuwaunganisha
watu kuwa kitu kimoja.Siku hii ambayo leo tunakumbuka Mazazi ya Mtume Muhammad
(s.a.w.w) naamimi ya kwamba darasa hili la Umoja aliyoifunza Mtume Muhammad
(s.a.w.w), aliyoifunza Nabii Issa / Yesu (a.s), naamini darasa hili muhimu Watanzania wanalihitajia leo kuivaa na
kuiunga Mkono kwa hali na mali.
Dini zote zilizotoka kwa Mungu, Vitabu vyote vilivyotoka kwa
Mungu,ikiwemo Taurati,ikiwemo Injiir, ikiwemo Zabour na ikiwemo Qur’an
takatifu, vitabu vyote hiyo ukijaribu kivisoma kwa umakini vyote vimekuja
kumuunganisha Mwanadamu na wala sio
kumgawanya Mwanadamu, Kama Mitume walifanya kazi za kuwaunganisha watu na
vitabu vya mungu ukivisoma vyote vinakazi ya kuwaunganisha watu.
Hatuna kitabu cha Mungu kinachowagawanya watu,hatuna kitabu
cha mungu kinachowabagua watu, hatuna kitabu cha mungu kinachowatenga watu,
kwahivyo dini zote zilizotoka kwa mungu zote zimelingania kuwafanya watu kuwa
kitu kimoja,
zote zinawataka watu wasikilizane na waelewane, na mimi naamini na
mtakubaliana na mimi watanzania wenzangu ya kwamba Moja ya mafunzo muhimu leo
hii yanayotakikana kwa watanzania wote pamoja na tofauti za dini zao, wawe
Waislam, wawe Wakristo, wawe Mayahudi na wawe wenye dini zingine
zinazojulikana, naamini yakwamba mafunzo haya wanayahitajia Watanzania.
Na ninaamini vilevile taifa hili kwa darasa hili na somo hili
linalofunzwa katika siku hii ya kumbukumbu ya kuzaliwa Muhammad (s.a.w.w)
vilevile naamini Watanzania pamoja na Taifa kwa ujumla linahitajia.Bwana Mtume
Muhammad (s.a.w.w) ameishi sehemu mbili huyu amabe tunamkumbuka leo hii kualiwa
kwake, Bwana huyu ameishi katika mji wa Makka, ameishi vilevile katika mji wa
Madina.
Katika Mji wa Makka katika kazi alizozifanya nataka kuonyesha vipi
Mtume alipokuwa Makka alijitahidi kuwaunganisha watu na si kuwagawanya.
Watu wa Makka au Wakazi wa Makka walikuwa na Dini tofauti,
walikuwepo Wakristo, walikuwepo Mayahudi, walikuwepo wanaoabudu Masanam
wanaoabudu Hubal, Lata Manata walikuwa ni waungu wao wakiwaabudu, lakini
angalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyoishi na watu wa Makka, aliishi na watu
wa makka mpaka wenyewe wakawa wanasema “Hatujawahi kukuona wewe ukiongopa
katika jambo” huu ni ushuhuda au ushahidi unaotolewa na watu sio Waislam ndani
ya ardhi ya Makka.
Hii ni kuonesha ya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) moja ya
masomo yake muhimu yalikuwa ni kuwaunganisha watu, yaani kuunganisha Umma,
yaani ni kuwafanya watu kuwa kitu kimoja na ilikuwa nikuwafanya watu waelewane,
wasikilizane na wala sio kwenda kinyume na hivyo.
Wanamuambia Mtume (s.a.w.w)
hatujawahi kukusikia wewe Ukiongopa,Historia inatuambia Mtume huyu tunaekumbuka
leo kuzaliwa kwake, alikuwa akijulikana kwa siku mbili muhimu, sifa ya ukweli
na sifa ya uaminifu, Sifa ya Ukweli na Uminifu Mtume (s.a.w.w) ndani ya nchi ya
Makka aliitwa na Waislam na wasiokuwa Waislam, sio waislam tu walimpa sifa
hiyo.
Waislam na wasiokuwa waislam kwanini, kwasababu Mtume
(s.a.w.w) katika Mafunzo yake ya Makka ilikuwa Watu wa Makka wawe kitu kimoja,
ilikuwa jamii ya Makka iwe wamoja, naamini masomo haya, mafundisho haya na
mahubiri haya leo hii sisi katika taifa hili la Tanzania tunayahitajia kwa kiasi
kikubwa.
Katika kuunganisha jamii ya Makka, watu wa Makka waislam na wasiokuwa
waislam amana zao, fedha zao, vitu vyao vilikuwa vikiwekwa nyumbani kwa Mtume
Muhammad (s.a.w.w), kwa Ibara iliyokuwa nzuri nyumba ya Mtume ndio ilikuwa
Benki ya Watu wa Makka, naamini ya kwamba ilikuwa umoja wa hali ya juu.
Umoja uliompelekea mtu anaeabudu sanam, mtu anaemuamini Nabii
Issa / Yesu (a.s) kwamba ndio Mtume wake, mtu anaeamini Nabii Mussa (a.s) ndio
Mtume wake na Taurati na Injiir ndio vitabu vyao lakini amana zake anaziweka
nyumbani kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika
kuwaunganisha watu kuwafanya kuwa Kitu kimoja alijitahidi kupambana na utumwa
na kujaribu kuondoa utumwa kwa hali na
mali katika jamii, alijitahidi kuwaondoa wanaoitwa Watumwa, akajaribu kufunza
mafunzo ambayo yataondoa Utumwa katika jamii ili watu wawe kitu kimoja.
Mtume akafunza kwamba kunyanganya ni jambo halifai ambapo kwa kipindi hicho
lilikuwa ni jambo la kawaida, utapeli ni jambo halifai, akafunza rushwa haifai,
akafunza uharibifu haufai yote yalikuwa ni mafunzo yake, kwanini kwasababu
yanalenga kuifanya umma, kuifanya jamii kuwa kitu kimoja.
Mtume Muhammad
(s.a.w.w) akajitahidi jambo moja muhimu naamini leo linahitajika mmno kujaribu
kunyanyua heshima na hadhi ya Mwanamke, Mwanamke alikuwa akionekana ni mtu wa
daraja la pili,mtume akainyanyua hadhi ya mwanamke, mtume akafundisha hakuna
Mfumo Dume ndani ya Uislam, mtume akafunza yakwamba mwanamke anayohaki ya
kurithi kama vile anavyorithi mwanaume, mtume akafunza yakwamba mwanamke ni
mmoja katika wanafamilia.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) akafunza kuwa mwanamke anayohaki
sawa kama vile mwanamume, mtume akafunza kuwa mwanamke anayohaki ya kumiliki
kama vile anavyomiliki mwanaume, Mtume akafunza mwanamke anayohaki yakushiriki
katika maamuzi, anayohaki ya kushiriki katika kupiga kura, anayohaki ya
kuendesha gari lake.
Haya ndio yalikuwa mafunzo ya Mtume Muhammad (s.a.w.w)
katika kuonesha na katika kuunganisha jamii.Na nizungumze jambo nzuri zaidi
Mtume Muhammad (s.a.w.w) walikuwepo baadhi ya wanawake wakimtembelea
akinyanyuka kwa sababu ya kwaheshimu wanawake hao, kwahivyo naamini ya kwamba
mafunzo haya ya kuwaunganisha watu ya kuwafanya watu kuwa kitu kiomja na dhana
ya mwanamke kama alivyoifundisha Mtume , naamimi ya kwamba ni funzo muhimu
watanzania wote wanalihitajia.
Vilevile jambo nzuri la kupendeza Mtume Muhammad (s.a.w.w)
akajaribu kutengeneza na sio tu kuunganisha watu Mtume alivuka zaidi ya hivyo,
Mtume alivuka na akatengeneza udugu, yaani Mtume alitengeneza Umoja hakuishia
hapo na akaingia kutengeneza udugu ikawa huyu ni ndugu wa huyu, Yule ni ndugu
wa Yule yote kwa nini ni kuakikisha jamii yote inakuwa kitu kimoja.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipohama kwenda madina, alipofika
madina akaendelea na kazi hiyo hiyo akajitahidi kuunganisha katika ya watu
waliohama kutoka makka kwenda madina, akajitahidi kuwaunganisha hawa wawe kitu
kimoja, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alijitahidi kuunganisha kati ya Makabila
mawili yaliyokuwepo madina, kabila la AUS NA AZRAJ akayaunganisha makabila hayo
na kuhakikisha yanakuwa kitu kimoja,
si hivyo tu Mtume alipofika Madina
akatengeneza umoja wa watu wa Madina, umoja huo ulikuwa unawakusanya Wakristo,
unawakusanya Mayahudi na unawakusanya Waislam.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) akatengeneza kamati ya amani ya
kuwalinda watu wa Madina Waislam na Wasiokuwa Waislam, kamati ya kuwalinda
Waislam, Wakristo, Mayahudi walioko katika ardhi ya Madina, Mtume Muhammad
(s.a.w.w) akakaa meza moja na watu hawa anaotofautiana nao Kidini, Kifikra na
Kimtazamo.
Kwa umuhimu wa kikao kile cha Amani na Maelewano na umoja kwa
watu wa Madina ningependa kunukuu beti kama mbili au tatu katika vitabu vya
kihistoria bakubaliano yanaandikwa kwa kusemwa “Haya ni makubaliano kutoka kwa
Muhammad (s.a.w.w) Mtume wa Mungu baina ya Waumini na Waislam, kwa ibara nzuri
Mtume (s.a.w.w) anawaita Mayahudi, anawaita Wakristo anawaita kwa jina la
WAUMINI,
kwahivyo makubaliano yake anasema ni kati ya Waumini na
Waislam mpaka mwisho wa makubaliano.leo naamini mafunzo haya tunayahitajia,
kwamba kumbe sisi tunaoamini Qu’an na wenzetu wanaoamini Injiir na wanaoamini
Taurati na Zabuuri Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae leo tunakumbuka kuzaliwa
kwake hawa anawaita WauminiAnasema tena
“ Na hakika Mayahudi wa Bani Aufu, hawa
mayahudi na wanaowafuata mayahudi yani Wakristo na wengineo hawa wote ni waumii
ni umma mmoja ni jamii moja, wao wanadini yao na waislam wana dini yao, kama
kuna mtu alifundisha kuheshimiana katika dini, kuheshimu dini za watu basi
Mtume Muhammad (s.a.w.w) atakuwa mtu wa kwanza na atakuwa anaongoza,
Mtume pia anasema “Kati ya mayahudi na wakristo wote walioko
madina wao akishambuliwa Mwislam lazima wanyanyuke kumsaidia mwislam na mwislam
watakapompata yahudi, watakapompata Mkristo anashambuliwa wao ni lazima na wao
wanyanyuke wamsaidie Mkristo,” huyu ndio Mtume tunaemkumbuka leo hii,mtume wa
huruma, mtume wa maelewano.
Mtume anasema tena “ yeyote atakaeishi hapa
Madina awe Mwislam awe Mkristo awe
Myahudi yupo katika amani haya ndio makubaliano ya Mtume ambae tunakumbuka
kuzaliwa kwake na tunamsheherekea Mtume aliefunza hivi.aliewaunganisha watu hivi,
Nikimalizia nisema neon moja nzuri kwamba mafunzo yake yote
Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika maisha yake yote yalikuwa yamegubikwa kwenye
huruma,mtume alikuwa mtume wa huruma,
akiwaonea huruma watu wa aina zote, kwa
hivyo siku hii ya kuzaliwa mtume na siku hii ya Maulidi ya Mtume (s.a.w.w).Moja
ya Mafunzo makubwa ya kujifunza ni sisi kama watanzania kupambika na huruma ya
Mtume (s.a.w.w), yule unaetofautiana nae Kidini, Kirai na Kifikra umuonee huruma
sio uwe na roho mbaya dhidi yake, yule ambae unamuona hayuko katika dini yangu
yupo katika dini nyingine, wewe wajibu wako kwa kumfuata Mtume ni kumuonea
huruma.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakufunza ukatili, Mtume hakufunza
chinjachinja, mtume hakufunza kukunja uso, mtume hakufunza roho mbaya, yoyote
anaekuambia mtume amefunza roho mbaya, mtume amefunza chinjachinja, mtume
amefunza kukunja uso, huyo bado hajamuelewa Mtume Muhammad (s.a.w.w),
Mwenyezimungu anasmea katika Qur’an kumuambia Mtume Muhammad (s.a.w.w)
“wewe
umekubalika kwa sababu ya huruma uliyokuwa nayo” ndio maana Waislam, Mayahudi
na Wakristo walikuwa wakihifadhi amana zao nyumbani kwa Mtume.Katika mafunzo
aliyofunza Mtume yalikuwa ni Mapenzi, ni mahaba , ni upendo, maelewano,
masikilizano, kumpenda jirani yako ndicho mtume alichofunza, Mtume alifunza
waislam kupendana wenyewe kwa wenyewe, Mtume alifunza Waislam kupendana na
Wasiokuwa Waislam,
mtume alifunza kuwapenda mafakiri, alifunza kuwapenda
masikini, alifunza kuwapenda wajane, alifunza kuwapenda mayatima
Alifunza kuwapenda watu wanaoishi katika mazingira magumu,
alifunza kuwapenda kila watu wenye aina yoyote ya matatizo, hayo ndio yalikuwa
mafundisho yake katika maisha yake, Mtume alifunza kusaidiana, Mtume alifunza
ukarimu, Mtume alifunza kuvumiliana hata kwa mtu mnaetofautina Kidini na
kifikra.
Mtume anawaambia anawaambia waabudu Masanam “Nyie mnadini yenu,na mimi
nina dini yangu” ndivyo mtume alivyofunza akatufundisha ya kwamba “Hakuna
kulazimishwa mtu katika dini” yaani hakuna kumlazimisha mtu kuifuata dini,
jambo la kufuata dini ni jambo la kukinaika na kuridhia kwa mtu mwenyewe
binafsi, mafunzo haya leo yanahitajika.Mtume alifunza kuishi kwa usalama,
kuishi pasina mivutano, kuishi pasina misuguano, haya ndio yalikuwa mafunzo
yake.
Mwisho ni wito wetu kwa Watanzania kwa siku hii ya kuzaliwa
Mtume Muhammad (s.a.w.w), Kama mafunzo ya mtume yalikuwa ni huruma, siku hii ya
kuzaliwa mtume tunatoa wito kwa watanzania wawe na tabia ya kuhurumiana,
matajiri wawahurumie masikini, wenye nacho wawahurumie wasiokuwa nacho, wenye
elimu wawahurumie wasiokuwa na elimu, wenye uwezo wawaahurumie wasiokuwa na
uwezo.
Katika siku hii ya Maulidi moja ya ujumbe muhimu tuubebe ni
upendo na maelewano aliyoyafunza Mtume Muhammad (s.a.w.w) tuondoke na somo la
maelewano kama watanzania, tupendane,hakuna sababu ya sisi kubaguana kwa sababu
mitume wetu wote walikuja kufunza maelewano, mitume wetu wote walikuja kufunza
kusikilizana, mitume wetu wote walikuja kufunza kuvumiliana, mitume wetu wote
walikuja kufunza mtu aipende nchi yake, mtu kuwapenda watu wake,
kupenda nchi
yako ni katika imani.Hayo ndio mafunzo yaliyofunzwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w)
na ninaamini ndio mafunzo yaliyofunzwa
na Nabii Issa / Yesu (a.s) na ndio mafunzo ya Nabii Mussa / Mosses (a.s), na
ndio mafunzo ya Yohana na ndio mafunzo ya Mitume wote wa Mwenyezimungu (swt),
katika siku hii ya Maulid turudi katika mambo hayo.
Mwisho niseme dini za mungu zimekuja kufunza amani, zimekuja
kufunza utulivu, “Wewe mungu wewe ni amani” mungu mwenye anaeabudiwa na
Waislam, anaeabudiwa na Wakristo, anaeabudiwa na Mayahudi, anaeabudiwa na
Majusi mungu huyo anaitwa amani, “na wewe mungu kwako inatoka amani na kwako
vilevile inarudi amani, “Mungu tufanye hapa Tanzania, na duniani kote tunaishi
kwa amani.
Mitume wote wa Mwenyezimungu wamekuja kufunza amani, na Mungu
tunakuwanae ni Mungu wa Amani, si Mungu wa Vita, si Mungu wa mivutano bali ni
Mungu wa Amani na Masikilizano, Mungu tunakuomba utupe amani ya nchi yetu,
Tanzania uzidi kuiboresha na kuifanya ni kisiwa cha amani na kisiwa cha
masikilizano, uzidikuwafanya watanzania hawajui kubaguana kwa sababu ya dini
zao, wabakie ni ndugu,
wanasikilizana,wanaelewana, Mwenyezimungu tunakuomba
vilevile Viongozi wan chi yetu, Utawala tuliokuwa nao Mungu uwape
Hekima,busara, Utulivu waweze nao wawe ni chachu kuendeleza amani tuliyokuwanayo, na watuongoze kwa busara na
utulivu mpaka mwenyezimungu utakapoturudisha kwako.
Asanteni sana na hongereni
Watanzania wote kwa kuzaliwa Kiongozi wa watu wote wa huruma, upendo na
maelewano Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Imetolewa
Na:
Kiongozi
Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
10-12-2016,
Jumamosi.