Wiki hii Chama Cha Wananchi (CUF) kilipata mtikisiko baada ya Profesa
Ibrahim Lipumba kutangaza uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa
chama hicho katika kipindi ambacho wengi hawakutegemea.
Uamuzi wa Profesa Lipumba uliitikisa pia ngome ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kwa kuzingatia kuwa ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa
wenyeviti wote wa vyama vinavyounda umoja huo.
Ukifuatilia kwa kina sababu alizozitoa Profesa Ibrahim Lipumba, ni
pamoja na kuona kuwa Ukawa imepoteza muelekeo kwa kuwa imeshindwa
kuzingatia tunu za taifa ikiwemo tunu ya uadilifu.
“Nimeshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyotufikisha hapa. Hata
hivyo, dhamira na nafsi inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ya Ukawa
tumeshindwa kuenzi na kuzingatia Tunu za Taifa za utu, uzalendo,
uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji,” alisema Profesa Lipumba.
Maelezo ya Profesa Lipumba katika kipengele hicho yanaunga mkono
kauli ya Kiongozi Mkuu wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema kuwa
vyama vingine vya upinzani havizingatii tunu ya uadilifu tofauti na
chama chake ambacho kimeamua kuiweka tunu hiyo kwenye azimio lake la
Tabora.
Zitto Kabwe aliyasema hayo alipokuwa anawahutubia wanachama wa chama
hicho mjini Kigoma huku akiwapima mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na
Dk. John Magufuli na kudai kuwa hawana ubavu wa kupambana na ufisadi.
Ni kama Profesa Lipumba na Zitto Kabwe waliongea lugha moja katika vipindi tofauti katika kipengele hicho.
Ingawa Profesa Lipumba alishiriki katika kumsafisha Edward Lowassa na
kumkaribisha Ukawa, alirudi kusema hadharani kuwa nafsi yake inamsuta
hivyo ametafuta kile ambacho wazungu wanaita ‘peace of mind’.
Hata hivyo, muungano wa Ukawa una madhara chanya ya kidemokrasia katika taifa letu ambayo hata Zitto Kabwe alikiri kuyaona.
“Uchaguzi wa mwaka huu hata kama chama kimojawapo kitashinda hakiwezi
kuunda serikali peke yake. Na kama kuna jambo ambalo tutalifanya
wapinzani na wananchi wasitusamehe ni kushirikiana na CCM,” alisema
Zitto Kabwe.Chanzo dar24