Habari Kamili
Serikali yawatahadharisha wananchi
kuzingatia matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili
kuondoa vitendo vya uhalifu hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa
kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi Prisca Ulomi wakati wa mkutano na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Bi Prisca amesema kuwa
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kutambua umuhimu wa TEHAMA
wameamua kuandaa muswada wa Sheria za Matumizi Sahihi na Salama ya
Mtandao (Cyber Laws).
Akieleza zaidi Bi Prisca amesema
kuwa Muswada wa sheria hizo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa
Binafsi (The Personal Data Protection Bill), Muswada wa Sheria ya Biashara ya
Miamala ya Kielektroniki (Electronic Transaction Bill), na Muswada wa
Sheria ya Kuzuia Uhalifu kwa njia ya Kompyuta na Mtandao (Computer and Cyber
Crimes Bills).
“Sheria hizo zitasaidia kuimarisha
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini kwa kudhibiti
uhalifu kwa kutumia mitandao na kuwalinda watoto dhidi ya matumizi yasiyofaa ya
mitandao”. alisema Bi Prisca.
Bi Prisca aliongeza kuwa serikali
imetumia gharama kubwa kuweka miundombinu ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha
na kuharakisha utoaji wa huduma mbalimbali na kubainisha kuwa wapo baadhi ya
watu wanatumia vibaya teknolojia hiyo, hivyo kunaumuhimu wa kuwepo sheria
zitakazodhibiti uhalifu kupitia mitandao.
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia imetoa rai kwa wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya
mitandao na badala yake watumie vizuri mitandao hiyo kwa maendeleo yao na taifa
kwa ujumla hali inayoweza kuathiri ukuaji wa sekta hiyo nchini.