Tuesday, December 13, 2016

“Tusheherekee Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa kupambika na Huruma yake” Sheikh Jalala

                                   
Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala akisisitiza jambo katika Kikao na Waandishi wa Habari katika Kuadhimisha siku ya Kuzaliwa (Maulid) ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) jijini Dar es salaam.
                               TAARIFA KWA UMMA
Ndugu zangu Waislam wenzangu Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu,Amani ya Mwenyezimungu iwe kwenu wote. Napenda kwanza niwape hongera kwa waisla wote watanzania kwa tukio hili la kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), napenda niwape Hongera kwa sababu ya tukio hili kubwa la kuzaliwa kiongozi huyu.

Kama ambayo nawapa hongera Watanzania wote Waislam na wasiokuwa waislam kwa kushirikiana na watanzania wenzao katika tukio hili la Maulid, katika tukio hili la kuzaliwa Mtume wa Huruma, Mtume wa Upendo, mtume wa Mapenzi, Mtume wa Maelewano, Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Katika siku hii ya Maulid na katika kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume huyu napenda kuzungumza jambo moja ambalo ni nzito na la muhimu, na sisi kama watanzania wote kwa ujumla Waislam na wasiokuwa waislam tunalihitajia tukio hilo, au tunayahitajia maelezo hayo yanayohusiana na Mtume wetu Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Tukio hili napenda nimesome Mtume kwenye upande wa kazi moja kubwa ambayo sisi kama watanzania tunahitajia nayo ni kazi ya Kuwaunganisha watu,Moja ya kazi kubwa muhimu ambayo mtume huyu tunaemkumbuka Maulid na kuzaliwa kwake leo,moja ya kazi kubwa nyeti na muhimu aliyoifanya ilikuwa ni kuwaunganisha watu.
 
Hawa ni baadhi ya waandishi wa habari upande wa Television wakiwa makini kumsikiliza Kiongozi Mkuu wa Waislam Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) yeye sambamba na mitume wengine wote waliopita,moja ya kazi yao kubwa ilikuwa ni “Tauhidil Kalima” ni Tauhidil Umma” ilikuwa ni kuwaunganisha watu, kwanzia Mtume Adam (a.s) mpaka kufikia Mtume Ibrahim (a.s), mpaka kufikia Mtume Mussa (a.s), Mpaka kufikia Mtume Issa / Yeu(a.s) na hatimae kufikia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), hao wote moja ya mafunzo yao muhimu na makubwa ilikuwa ni kuwafanya watu wawe kitu kimoja.

Hakuna Mtume aliekuja kuja kufundisha mafundisho ya kuwatenga watu, hakuna mtume wa Mungu aliyekuja kuwafunza watu kutengana, bali watu wote walikuja kuwaunganisha watu kuwa kitu kimoja.Siku hii ambayo leo tunakumbuka Mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) naamimi ya kwamba darasa hili la Umoja aliyoifunza Mtume Muhammad (s.a.w.w), aliyoifunza Nabii Issa / Yesu (a.s), naamini darasa hili muhimu  Watanzania wanalihitajia leo kuivaa na kuiunga Mkono kwa hali na mali.

Dini zote zilizotoka kwa Mungu, Vitabu vyote vilivyotoka kwa Mungu,ikiwemo Taurati,ikiwemo Injiir, ikiwemo Zabour na ikiwemo Qur’an takatifu, vitabu vyote hiyo ukijaribu kivisoma kwa umakini vyote vimekuja kumuunganisha  Mwanadamu na wala sio kumgawanya Mwanadamu, Kama Mitume walifanya kazi za kuwaunganisha watu na vitabu vya mungu ukivisoma vyote vinakazi ya kuwaunganisha watu.

Hatuna kitabu cha Mungu kinachowagawanya watu,hatuna kitabu cha mungu kinachowabagua watu, hatuna kitabu cha mungu kinachowatenga watu, kwahivyo dini zote zilizotoka kwa mungu zote zimelingania kuwafanya watu kuwa kitu kimoja, 

zote zinawataka watu wasikilizane na waelewane, na mimi naamini na mtakubaliana na mimi watanzania wenzangu ya kwamba Moja ya mafunzo muhimu leo hii yanayotakikana kwa watanzania wote pamoja na tofauti za dini zao, wawe Waislam, wawe Wakristo, wawe Mayahudi na wawe wenye dini zingine zinazojulikana, naamini yakwamba mafunzo haya wanayahitajia Watanzania.

Na ninaamini vilevile taifa hili kwa darasa hili na somo hili linalofunzwa katika siku hii ya kumbukumbu ya kuzaliwa Muhammad (s.a.w.w) vilevile naamini Watanzania pamoja na Taifa kwa ujumla linahitajia.Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) ameishi sehemu mbili huyu amabe tunamkumbuka leo hii kualiwa kwake, Bwana huyu ameishi katika mji wa Makka, ameishi vilevile katika mji wa Madina. 


Katika Mji wa Makka katika kazi alizozifanya nataka kuonyesha vipi Mtume alipokuwa Makka alijitahidi kuwaunganisha watu na si kuwagawanya.

Watu wa Makka au Wakazi wa Makka walikuwa na Dini tofauti, walikuwepo Wakristo, walikuwepo Mayahudi, walikuwepo wanaoabudu Masanam wanaoabudu Hubal, Lata Manata walikuwa ni waungu wao wakiwaabudu, lakini angalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) alivyoishi na watu wa Makka, aliishi na watu wa makka mpaka wenyewe wakawa wanasema “Hatujawahi kukuona wewe ukiongopa katika jambo” huu ni ushuhuda au ushahidi unaotolewa na watu sio Waislam ndani ya ardhi ya Makka.

Hii ni kuonesha ya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) moja ya masomo yake muhimu yalikuwa ni kuwaunganisha watu, yaani kuunganisha Umma, yaani ni kuwafanya watu kuwa kitu kimoja na ilikuwa nikuwafanya watu waelewane, wasikilizane na wala sio kwenda kinyume na hivyo.

Wanamuambia Mtume (s.a.w.w) hatujawahi kukusikia wewe Ukiongopa,Historia inatuambia Mtume huyu tunaekumbuka leo kuzaliwa kwake, alikuwa akijulikana kwa siku mbili muhimu, sifa ya ukweli na sifa ya uaminifu, Sifa ya Ukweli na Uminifu Mtume (s.a.w.w) ndani ya nchi ya Makka aliitwa na Waislam na wasiokuwa Waislam, sio waislam tu walimpa sifa hiyo.

Waislam na wasiokuwa waislam kwanini, kwasababu Mtume (s.a.w.w) katika Mafunzo yake ya Makka ilikuwa Watu wa Makka wawe kitu kimoja, ilikuwa jamii ya Makka iwe wamoja, naamini masomo haya, mafundisho haya na mahubiri haya leo hii sisi katika taifa hili la Tanzania tunayahitajia kwa kiasi kikubwa.

Katika kuunganisha jamii ya Makka, watu wa Makka waislam na wasiokuwa waislam amana zao, fedha zao, vitu vyao vilikuwa vikiwekwa nyumbani kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa Ibara iliyokuwa nzuri nyumba ya Mtume ndio ilikuwa Benki ya Watu wa Makka, naamini ya kwamba ilikuwa umoja wa hali ya juu.

Umoja uliompelekea mtu anaeabudu sanam, mtu anaemuamini Nabii Issa / Yesu (a.s) kwamba ndio Mtume wake, mtu anaeamini Nabii Mussa (a.s) ndio Mtume wake na Taurati na Injiir ndio vitabu vyao lakini amana zake anaziweka nyumbani kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuwaunganisha watu kuwafanya kuwa Kitu kimoja alijitahidi kupambana na utumwa na kujaribu kuondoa utumwa  kwa hali na mali katika jamii, alijitahidi kuwaondoa wanaoitwa Watumwa, akajaribu kufunza mafunzo ambayo yataondoa Utumwa katika jamii ili watu wawe kitu kimoja.
Mtume akafunza kwamba kunyanganya  ni jambo halifai ambapo kwa kipindi hicho lilikuwa ni jambo la kawaida, utapeli ni jambo halifai, akafunza rushwa haifai, akafunza uharibifu haufai yote yalikuwa ni mafunzo yake, kwanini kwasababu yanalenga kuifanya umma, kuifanya jamii kuwa kitu kimoja.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) akajitahidi jambo moja muhimu naamini leo linahitajika mmno kujaribu kunyanyua heshima na hadhi ya Mwanamke, Mwanamke alikuwa akionekana ni mtu wa daraja la pili,mtume akainyanyua hadhi ya mwanamke, mtume akafundisha hakuna Mfumo Dume ndani ya Uislam, mtume akafunza yakwamba mwanamke anayohaki ya kurithi kama vile anavyorithi mwanaume, mtume akafunza yakwamba mwanamke ni mmoja katika wanafamilia.


Mtume Muhammad (s.a.w.w) akafunza kuwa mwanamke anayohaki sawa kama vile mwanamume, mtume akafunza kuwa mwanamke anayohaki ya kumiliki kama vile anavyomiliki mwanaume, Mtume akafunza mwanamke anayohaki yakushiriki katika maamuzi, anayohaki ya kushiriki katika kupiga kura, anayohaki ya kuendesha gari lake. 

Haya ndio yalikuwa mafunzo ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kuonesha na katika kuunganisha jamii.Na nizungumze jambo nzuri zaidi Mtume Muhammad (s.a.w.w) walikuwepo baadhi ya wanawake wakimtembelea akinyanyuka kwa sababu ya kwaheshimu wanawake hao, kwahivyo naamini ya kwamba mafunzo haya ya kuwaunganisha watu ya kuwafanya watu kuwa kitu kiomja na dhana ya mwanamke kama alivyoifundisha Mtume , naamimi ya kwamba ni funzo muhimu watanzania wote wanalihitajia.

Vilevile jambo nzuri la kupendeza Mtume Muhammad (s.a.w.w) akajaribu kutengeneza na sio tu kuunganisha watu Mtume alivuka zaidi ya hivyo, Mtume alivuka na akatengeneza udugu, yaani Mtume alitengeneza Umoja hakuishia hapo na akaingia kutengeneza udugu ikawa huyu ni ndugu wa huyu, Yule ni ndugu wa Yule yote kwa nini ni kuakikisha jamii yote inakuwa kitu kimoja.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipohama kwenda madina, alipofika madina akaendelea na kazi hiyo hiyo akajitahidi kuunganisha katika ya watu waliohama kutoka makka kwenda madina, akajitahidi kuwaunganisha hawa wawe kitu kimoja, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alijitahidi kuunganisha kati ya Makabila mawili yaliyokuwepo madina, kabila la AUS NA AZRAJ akayaunganisha makabila hayo na kuhakikisha yanakuwa kitu kimoja, 

si hivyo tu Mtume alipofika Madina akatengeneza umoja wa watu wa Madina, umoja huo ulikuwa unawakusanya Wakristo, unawakusanya Mayahudi na unawakusanya Waislam.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) akatengeneza kamati ya amani ya kuwalinda watu wa Madina Waislam na Wasiokuwa Waislam, kamati ya kuwalinda Waislam, Wakristo, Mayahudi walioko katika ardhi ya Madina, Mtume Muhammad (s.a.w.w) akakaa meza moja na watu hawa anaotofautiana nao Kidini, Kifikra na Kimtazamo.

Kwa umuhimu wa kikao kile cha Amani na Maelewano na umoja kwa watu wa Madina ningependa kunukuu beti kama mbili au tatu katika vitabu vya kihistoria bakubaliano yanaandikwa kwa kusemwa “Haya ni makubaliano kutoka kwa Muhammad (s.a.w.w) Mtume wa Mungu baina ya Waumini na Waislam, kwa ibara nzuri Mtume (s.a.w.w) anawaita Mayahudi, anawaita Wakristo anawaita kwa jina la WAUMINI, 

kwahivyo makubaliano yake anasema ni kati ya Waumini na Waislam mpaka mwisho wa makubaliano.leo naamini mafunzo haya tunayahitajia, kwamba kumbe sisi tunaoamini Qu’an na wenzetu wanaoamini Injiir na wanaoamini Taurati na Zabuuri Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae leo tunakumbuka kuzaliwa kwake hawa anawaita WauminiAnasema tena 

“ Na hakika Mayahudi wa Bani Aufu, hawa mayahudi na wanaowafuata mayahudi yani Wakristo na wengineo hawa wote ni waumii ni umma mmoja ni jamii moja, wao wanadini yao na waislam wana dini yao, kama kuna mtu alifundisha kuheshimiana katika dini, kuheshimu dini za watu basi Mtume Muhammad (s.a.w.w) atakuwa mtu wa kwanza na atakuwa anaongoza,

Mtume pia anasema “Kati ya mayahudi na wakristo wote walioko madina wao akishambuliwa Mwislam lazima wanyanyuke kumsaidia mwislam na mwislam watakapompata yahudi, watakapompata Mkristo anashambuliwa wao ni lazima na wao wanyanyuke wamsaidie Mkristo,” huyu ndio Mtume tunaemkumbuka leo hii,mtume wa huruma, mtume wa maelewano.

Mtume anasema tena “ yeyote atakaeishi hapa Madina  awe Mwislam awe Mkristo awe Myahudi yupo katika amani haya ndio makubaliano ya Mtume ambae tunakumbuka kuzaliwa kwake na tunamsheherekea Mtume aliefunza  hivi.aliewaunganisha watu hivi,
Nikimalizia nisema neon moja nzuri kwamba mafunzo yake yote Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika maisha yake yote yalikuwa yamegubikwa kwenye huruma,mtume alikuwa mtume wa huruma,


 akiwaonea huruma watu wa aina zote, kwa hivyo siku hii ya kuzaliwa mtume na siku hii ya Maulidi ya Mtume (s.a.w.w).Moja ya Mafunzo makubwa ya kujifunza ni sisi kama watanzania kupambika na huruma ya Mtume (s.a.w.w), yule unaetofautiana nae Kidini, Kirai na Kifikra umuonee huruma sio uwe na roho mbaya dhidi yake, yule ambae unamuona hayuko katika dini yangu yupo katika dini nyingine, wewe wajibu wako kwa kumfuata Mtume ni kumuonea huruma.

Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakufunza ukatili, Mtume hakufunza chinjachinja, mtume hakufunza kukunja uso, mtume hakufunza roho mbaya, yoyote anaekuambia mtume amefunza roho mbaya, mtume amefunza chinjachinja, mtume amefunza kukunja uso, huyo bado hajamuelewa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mwenyezimungu anasmea katika Qur’an kumuambia Mtume Muhammad (s.a.w.w)

 “wewe umekubalika kwa sababu ya huruma uliyokuwa nayo” ndio maana Waislam, Mayahudi na Wakristo walikuwa wakihifadhi amana zao nyumbani kwa Mtume.Katika mafunzo aliyofunza Mtume yalikuwa ni Mapenzi, ni mahaba , ni upendo, maelewano, masikilizano, kumpenda jirani yako ndicho mtume alichofunza, Mtume alifunza waislam kupendana wenyewe kwa wenyewe, Mtume alifunza Waislam kupendana na Wasiokuwa Waislam,

 mtume alifunza kuwapenda mafakiri, alifunza kuwapenda masikini, alifunza kuwapenda wajane, alifunza kuwapenda mayatima
Alifunza kuwapenda watu wanaoishi katika mazingira magumu, alifunza kuwapenda kila watu wenye aina yoyote ya matatizo, hayo ndio yalikuwa mafundisho yake katika maisha yake, Mtume alifunza kusaidiana, Mtume alifunza ukarimu, Mtume alifunza kuvumiliana hata kwa mtu mnaetofautina Kidini na kifikra.

Mtume anawaambia anawaambia waabudu Masanam “Nyie mnadini yenu,na mimi nina dini yangu” ndivyo mtume alivyofunza akatufundisha ya kwamba “Hakuna kulazimishwa mtu katika dini” yaani hakuna kumlazimisha mtu kuifuata dini, jambo la kufuata dini ni jambo la kukinaika na kuridhia kwa mtu mwenyewe binafsi, mafunzo haya leo yanahitajika.Mtume alifunza kuishi kwa usalama, kuishi pasina mivutano, kuishi pasina misuguano, haya ndio yalikuwa mafunzo yake. 

Mwisho ni wito wetu kwa Watanzania kwa siku hii ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Kama mafunzo ya mtume yalikuwa ni huruma, siku hii ya kuzaliwa mtume tunatoa wito kwa watanzania wawe na tabia ya kuhurumiana, matajiri wawahurumie masikini, wenye nacho wawahurumie wasiokuwa nacho, wenye elimu wawahurumie wasiokuwa na elimu, wenye uwezo wawaahurumie wasiokuwa na uwezo.

Katika siku hii ya Maulidi moja ya ujumbe muhimu tuubebe ni upendo na maelewano aliyoyafunza Mtume Muhammad (s.a.w.w) tuondoke na somo la maelewano kama watanzania, tupendane,hakuna sababu ya sisi kubaguana kwa sababu mitume wetu wote walikuja kufunza maelewano, mitume wetu wote walikuja kufunza kusikilizana, mitume wetu wote walikuja kufunza kuvumiliana, mitume wetu wote walikuja kufunza mtu aipende nchi yake, mtu kuwapenda watu wake, 

kupenda nchi yako ni katika imani.Hayo ndio mafunzo yaliyofunzwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ninaamini ndio mafunzo  yaliyofunzwa na Nabii Issa / Yesu (a.s) na ndio mafunzo ya Nabii Mussa / Mosses (a.s), na ndio mafunzo ya Yohana na ndio mafunzo ya Mitume wote wa Mwenyezimungu (swt), katika siku hii ya Maulid turudi katika mambo hayo.

Mwisho niseme dini za mungu zimekuja kufunza amani, zimekuja kufunza utulivu, “Wewe mungu wewe ni amani” mungu mwenye anaeabudiwa na Waislam, anaeabudiwa na Wakristo, anaeabudiwa na Mayahudi, anaeabudiwa na Majusi mungu huyo anaitwa amani, “na wewe mungu kwako inatoka amani na kwako vilevile inarudi amani, “Mungu tufanye hapa Tanzania, na duniani kote tunaishi kwa amani.

Mitume wote wa Mwenyezimungu wamekuja kufunza amani, na Mungu tunakuwanae ni Mungu wa Amani, si Mungu wa Vita, si Mungu wa mivutano bali ni Mungu wa Amani na Masikilizano, Mungu tunakuomba utupe amani ya nchi yetu, Tanzania uzidi kuiboresha na kuifanya ni kisiwa cha amani na kisiwa cha masikilizano, uzidikuwafanya watanzania hawajui kubaguana kwa sababu ya dini zao, wabakie ni ndugu, 

wanasikilizana,wanaelewana, Mwenyezimungu tunakuomba vilevile Viongozi wan chi yetu, Utawala tuliokuwa nao Mungu uwape Hekima,busara, Utulivu waweze nao wawe ni chachu kuendeleza amani  tuliyokuwanayo, na watuongoze kwa busara na utulivu mpaka mwenyezimungu utakapoturudisha kwako.

Asanteni sana na hongereni Watanzania wote kwa kuzaliwa Kiongozi wa watu wote wa huruma, upendo na maelewano Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Imetolewa Na:
Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala
10-12-2016, Jumamosi.

No comments: