Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran
amesisitiza juu ya kufanyika juhudi kadiri inavyowezekana kwa ajili ya
kulinda umoja na mshikamano baina ya Waislamu na kusimama kidete mbele
ya mabeberu.
Ayatullah Sadeq Amoli Larijani
amesema hayo leo katika kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya
Vyombo vya Mahakama na kusisitiza kwamba, hii leo Ulimwengu wa Kiislamu
unahitajia umoja na mshikamano zaidi kuliko wakati wowote ule hivyo kuna
haja ya watu wote kufanya juhudi kwa ajili ya kulinda umoja huo.
Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama
nchini Iran amesema kuwa, kuzusha mifarakano ni sera za maadui wa
Uislamu na kubainisha kwamba, miamala ya madola ya Kiistikbari
inaonyesha kuwa, iko tayari kufanya chochote kwa ajili ya kuzusha
mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu na siku zote madola hayo yamo
mbioni kudhoofisha Waislamu sambamba na kupenya na kuwa satuwa katika
Ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Sadeq Amoli Larijani ameongeza kuwa, njia pekee ya
kukabiliana na siasa hizo za kikoloni ni kuongezwa kiwango cha ufahamu
na kumtambua adui baina ya Waislamu.
Amesema, kuwalingania watu umoja ni
jukumu la watu wote wenye vipaji, maulama na wasomi wa Ulimwengu wa
Kiislamu na kuongeza kuwa, jinai za maadui wa Uislamu nchini Yemen,
Iraq, Syria, Afghanistan na kwingineko ni ishara kwamba, uistikbari wa
dunia unataka kuangamiza kizazi cha mwanadamu.
No comments:
Post a Comment