Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya
Lebanon amekosoa vikali safari ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali
ya Saudi Arabia katika utawala wa Kizayuni wa Israel wiki jana na
kusisitiza kuwa Riyadh inahuisha uhusiano wake na Tel Aviv pasina na
kuzingatia maslahi ya Wapalestina.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema utawala wa Aal-Saud unatoa
mfano mbaya kwa mataifa mengine na haswa ya Kiislamu katika kufufua
uhusiano wake na utawala haramu wa Israel.
Akizungumza kwa njia ya
televisheni katika marasimu ya kukumbuka kifo cha Ahmad Zahri, mmoja wa
makamanda wa harakati hiyo ya Kiislamu, Sayyid Nasrullah amesema sio
jambo la mbali kwa utawala wa Riyadh katika hatua yake ya pili ya
kufufua uhusiano wake na Israel, kutangaza kuutambua rasmi utawala huo
bandia unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapelestina.
Matamshi ya Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon
yanajiri siku chache baada ya ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya
Riyadh ukiongozwa na Jenerali Anwar Eshki, kamanda mkuu wa zamani wa
Saudia kuutembelea utawala ghasibu wa Israel na kukutana na kufanya
mazungumzo na wakuu wa utawala huo katili wakiwemo wabunge wa bunge la
Knesset.
Eshki ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kituo cha Mafunzo ya Kiistratejia
na Sheria cha Mashariki ya Kati kilichoko Jeddah alikutana na kufanya
mazungumzo na Dore Gold, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Israel na Mshirikishi wa Masuala ya Harakati za Israel katika ardhi za
Palestina zinazokaliwa kwa mabavu Yoav Mordechai miongoni mwa maafisa
wengine wa utawala huo wa Kizayuni.
No comments:
Post a Comment