Licha ya makelele ya jamii ya kimataifa na watetezi
wa haki za binadamu, utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain umemtia
nguvuni kiongozi mwingine wa Kiislamu.
Habari zinasema kuwa, maafisa usalama wa utawala wa Manama
wamevamia makazi ya Seyyid Majid al-Mashaal, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Wanazuoni wa Kiislamu Bahrain mapema leo na kumkamata msomi huyo
mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa haujatoa taarifa au sababu za
kumkamata mwanachuoni huyo wa Kiislamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba
ya Uajemi.Haya yanajiri siku chache baada ya utawala wa Manama kuakhirisha kesi
dhidi ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim, msomi mtajika wa Kiislamu nchini
humo iliyotazamiwa kuanza kusikilizwa Jula 27.
Siku moja kabla ya kesi
hiyo, taarifa ya wasomi wa Kiislamu nchini Bahrain ilisema kuwa,
mashitaka anayolimbikiziwa Ayatullah Qassim ambaye utawala wa Manama
umemvua uraia ni ya kubuni na wala hayana mashiko na kwamba kesi dhidi
yake inakiuka katiba, haki za binadamu zilizoanishwa katika sheria za
nchi hiyo na hata za kimataifa.
Mwezi uliopita wa Juni, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika
na masuala ya uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza alilaani vikali
uamuzi wa mahakama ya rufaa ya Bahrain wa kuidhinisha hukumu iliyotolewa
dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Al-Wifaq na
kuongeza adhabu hiyo ya kifungo hadi miaka tisa.
Sheikh Salman alitiwa
nguvuni mwezi Disemba mwaka 2014 baada ya kutoa hotuba kadhaa za kupinga
siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Khalifa.
No comments:
Post a Comment