Thursday, July 28, 2016

Rais Robert Mugabe ataka wanaomkosoa wapatiwe adhabu kali

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amewatahadharisha mashujaa wa vita vya uhuru ambao wameonya kuwa huenda wakakataa kuunga mkono serikali yake kufuatia mporomoko mkubwa zaidi wa uchumi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Rais Mugabe amewaonya maveterani wa vita wanaomkosoa akieleza kwamba, watakabiliwa na adhabu kali endapo hawataachana na msimamo wao huo. 

Mashujaa hao wanaonya kuwa watakataa kumuunga mkono Mugabe endapo hataweka mikakati ya kukomesha ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi uliokithiri nchini humo na kusababisha maandamano makubwa zaidi.


Rais Mugabe amewaonya mashujaa hao alipokuwa akihutubia umati wa wafuasi wa chama tawala cha Zanu-PF. 
Aidha rais huyo amewataka viongozi wa chama cha mashujaa kuwachagua viongozi wapya.

Mugabe amesema kuwa, viongozi wa mashujaa hao wa vita vya ukombozi kutoka mikononi mwa wakoloni kuwa walikuwa wameshawishiwa na mataifa ya Magharibi.
Mugabe ameonya kuwa wale ambao wanaendeleza maandamano yaliyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni huenda wakafungwa jela kwani taifa hilo halina haja ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.


Hivi karibuni maveterani wenza wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambao wamekuwa waungaji mkono wake wakubwa, kwa mara ya kwanza kabisa walimtuhumu kiongozi huyo kuwa ni dekteta, matamshi ambayo yalitathminiwa na weledi wa mambo kama yataimarisha harakazi za upinzani dhidi ya Mugabe mwenye umri wa miaka 92.

No comments: