Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa uchache kesi
120 za ukatili wa kijinsia na ubakaji zimeripotiwa Sudan Kusini tangu
kuibuka machafuko mapya nchini humo majuma matatu yaliyopita.
Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa
Mataifa amesema kuwa, kikosi cha kusimamia amani cha umoja huo kingali
kinapokea taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubakaji na ubakaji
wa makundi.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa, baadhi ya wabakaji hao walikuwa na sare za jeshi.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kikosi cha kusimamia
amani cha UN huko Sudan Kusini kimeongeza doria zake na kinafanya juhudi
za kuwalinda wanawake katika mji mkuu Juba na katika miji mingine
kutokana na kukithiri kesi za ubakaji na ukatili wa kijinsia.
Amesema, Umoja wa Mataifa unazitaka
pande zote hasimu nchini Sudan Kusini kuwashughulikia wale wote
wanaopatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia
na ubakaji.Machafuko mapya mjini Juba yaliibuka tarehe saba mwezi huu ambapo hadi
sasa watu zaidi ya 300 wameripotiwa kuuawa na makumi ya maelfu ya
wengine wamelazikika kukimbia nchi.
Kadhalika machafuko hayo yameathiri
makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana 2015 kati ya mahasimu
hao wawili.Riek Machar hajaonekana hadharani tangu kulipotokea machafuko mjini Juba
hali ambayo imepelekea kuibuka tetesi kwamba, huenda kiongozi huyo
ameuawa. Hata hivyo Balozi wa Sudan Kusini nchini Kenya Jimmy Deng
Makuach amekanusha madai hayo.
No comments:
Post a Comment