Tuesday, September 27, 2016

Nasrallah: Uwahhabi ni hatari zaidi ya utawala wa Kizayuni

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, amesema anaitazama itikadi ya misimamo mikali ya Uwahhabi kuwa hatari zaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sayyed Hassan Nasrallah amenukuliwa na gazeti la Al Akhbar la Lebanon tolea la Jumanne akisema, "Uwahhabi ni shari zaidi ya Israel, hasa kwa kuzingatia kuwa lengo la itikadi hiyo ni kuwaangamiza wengine na kufuta kila kitu kuhusu Uislamu na Historia yake.".

Akihutubu katika hadhara ya wasoma mashairi ya maombolezo, Sayyed Nasrallah ameashiria kuibuka kundi la kitakfiri la Daesh au ISIS na kusema: "Mradi huu ulianzishwa mwaka 2011 na si suala la Kisuni na Kishia. Mashirika ya kijasusi yamehusika na tunapaswa kutumia fursa hii kukabiliana na Uwahhabi na kuuangamiza." Aidha amesema mgogoro uliopo hivi sasa  si baina ya Shia na Sunni bali ni mgogoro ulioibuliwa na Mawahhabi.

Ameongeza kuwa, Uwahhabi ni itikadi inayotawala Saudia na inapigiwa debe na watu wanaopata himaya ya Riyadh ambao wanawavutia magaidi kote duniani. Amesema magaidi wa ISIS wanatumia itikadi ya Uwahhabi kuwatuhumu Waislamu wengine kuwa ni makafiri na hivyo kuwaua.

Sayyid Nasrallah ameashiria tishio jingine kubwa zaidi ya Uwahhabi na Uzayuni kuwa ni 'Ushia wa Uingereza' ambao unafadhiliwa na mashirika ya kijasusi ya London. Amesema wanaohubiri Ushia huo wanajidai kuwa wanazuoni wa kidini katika hali ambayo ni mamluki wa mashirika ya kijasusi ya maadui.

Kiongozi wa Hizbullah amesema hana matumani ya suluhisho la kisiasa katika mgogoro wa Syria na kuongeza kuwa yanayojiri katika medani ya vita ndiyo yatakayoamua hatima ya nchi hiyo ya Kkiarabu

No comments: