Wednesday, September 23, 2015

Serikali Imefanikiwa Kuboresha Utendaji Kazi wa Utumishi wa Umma kwa Kuendesha Mikutano Kupitia Njia ya Video (Tehama)

Baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakiwa katika kikao kazi  kupitia njia ya video kwa makatibu tawala wa mikoa na wasaidizi wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali  za mitaa na wakuu wa idara za utawala na rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa  kwenye  mikoa ya Dares Salaam, Kagera, Tanga,Tabora,Manyara, Morogoro, Rukwa na Katavi kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Wakala wa Mafunzo kwa Mtandao iliyopo jijini Dares Salaam.
 Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma HAB Mkwizu wa pili kulia   akifafanua jambo wakati  kikao kazi  kupitia njia ya video kwa makatibu tawala wa mikoa na wasaidizi wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali  za mitaa na wakuu wa idara za utawala na rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa  kwenye  mikoa ya Dares Salaam, Kagera, Tanga,Tabora,Manyara, Morogoro, Rukwa na Katavi kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Wakala wa Mafunzo kwa Mtandao iliyopo jijini Dares Salaam.
                    Picha zote na Magreth Kinabo – MAELEZO


Serikali imefanikiwa   kuboresha  utendaji kazi wa utumishi wa umma kwa kuendesha mikutano kupitia njia ya video(TEHAMA) katika taasisi zake,wizara idara ili kuongeza kwa ufanisi na tija kwa gharama nafuu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwa muda mfupi.
Hayo yalisemwa na   Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma HAB Mkwizu    wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu uendeshaji wa  kikao kazi  kupitia njia ya video kwa makatibu tawala wa mikoa na wasaidizi wao, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na wakuu wa idara za utawala na rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa kwenye mikoa ya Dares Salaam, Kagera, Tanga,Tabora,Manyara, Morogoro, Rukwa na Katavi kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Wakala wa Mafunzo kwa Mtandao iliyopo jijini Dares Salaam.
“Serikali imebuni sera ya TEHAMA na Serikali Mtandao katika kutekeleza majukumu yetu kwa kulenga tija na ufanisi. Leo tunazungumzia  mpango wa Matokeo Mkubwa Sasa (BRN) ili tupate matokeo ya  BRN  kwa ufanisi  na kwa wakati hatuna budi kutumia TEHAMA,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo.
 Mkwizu alisema mkutano huo ni wa  awamu ya kwanza  kufanyika kwa kupitia njia hiyo, hivyo vikao vitatu vimefanyika, kikao cha kwanza  kufanyika kilifanyika  Septemba 15,mwaka huu ambao ulihusisha watendaji hao kwenye mikoa ya Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Dodoma , Ruvuma Kigoma,Lindi na Geita.
Aliongeza kwamba mkutano wa awamu ya  pili  ulifanyika Septemba 17, mwaka huu ambapo ulihusisha watendaji hao kwenye mikoa ya Arusha, Singida,Pwani,Iringa, Mara,Mtwara, Shinyanga, Njombe  na Simiyu.
Alizitaja   mada  zilizojadiliwa katika mikutano hiyo kuwa ni Sheria ya watu wenye ulemavu  ya mwaka 2010 na kanuni zake, wajibu wa waajiri katika ufuatiliaji na uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma , ukaguzi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma, ambalo ni jukumu la msingi la Tume ya  Utumishi wa Umma,ambao wanakagua mifumo yamenejimmenti  rasilimali watu ya utumishi wa umma na kuona inatekelezwa vipi  na tathimini ya kazi katika utumishi wa umma ili kulinganisha kazi mbalimbali na hatimaye kuja na mapendekezo kazi mbalimbali watu walipwe vipi kulingana na unyeti, madaraka ili zinazofanana zilipwe sawa na zisizofanana zilipwe tofauti.
Alisema awamu ya pili ya uendeshaji wa mikutano kwa kutumia njia hiyo itafanyika Novemba mwaka huu.
Mkwizu alifafanua kwamba   tayari  Serikali  imeshaweka mwongozo katika taasisi zake na mamlaka za Serikali ili ziweze kufanya mikutano au kikao kazi kwa njia video. Hivyo mikoa yote imeshafungiwa vifaa maalum kwa ajili ya matumizi hayo isipokuwa mikoa mipya ambayo ambayo hujiunga na mikoa mama. 
Kwa upande wake Mkurungezi Mtendaji wa  Wakala wa Mafunzo wa Serikali Mtandao(TaGLA), Charles Senkondo alisema ulianzishwa mwaka 2011 ili kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma.
 Alisema mfumo huo umewezesha madaktari bingwa wa hapa nchini kuweza kutibu wagonjwa kwa kuwasiliana na madaktari  wenzao mabingwa kutoka nje ya nchi, watu kufanya usaili na kupata kazi za kimataifa na mahakama kuendesha kesi kwa kuwasiliana na mashahidi  walioko nje ya nchi.
Alizitaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na baadhi ya watu kuwa  na fikra potofu katika matumizi ya TEHAMA, wengine wanafikiri ni kitu kigumu na kuwa na  woga wa kutumia lakini kutokana na ushirikiano  wanaoupata kutoka kwa wadau mbalimbali wameendesha mikutano mingi na wanao uwezo  wa kutoa ushauri na mwongozo inayosaidia kuendesha mikutano kupitia njia hiyo ili iweze kufanyika vizuri.
“Watanzania wafahamu kwamba wakala wa mafunzo kwa njia ya mtandao imeanzishwa na Serikali kwa ajili yao, hivyo ninatoa wito waweze kuitumia na kupeleka taarifa kwa urahisi ambazo  zinawafikia watu wengi kwa wakati mmoja na sisi tuko  tayari kutoa ushauri ili mikutano kufanyika ipasavyo”, alisema Senkondo.

No comments: