Usajili wa Raia
una jukumu la msingi katika kutekeleza matakwa ya utawala bora na
maendeleo ya kiuchumi katika taifa lolote lile duniani.
Hayo yamesemwa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Maimuna Tarishi wakati
akifungua mkutano wa wadau wa kujadili Rasimu ya Mkakati wa Usajili na
Uhifadhi wa Takwimu za Matukio Muhimu ya Binadamu uliofanyika jijini Dar
es Salaam.
Tarishi amesema
Usajili wa Raia ni wajibu wa kisheria kwa kuwa unasaidia katika upangaji
wa mipango madhubuti ya maendeleo pamoja na kuiletea maendeleo jamiii
kulingana na Mkakati wa Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi Tanzania
(KUKUTA II).
Katibu Mkuu huyo
wa Wizara ya Katiba na Sheria amebainisha kuwa mfumo wa Usajili wa Raia
uliopo sasa Tanzania Bara umekuwa ukifanya kazi kwa kusuasua na hivyo
kusababisha baadhi ya wananchi kutotambulika katika kumbukumbu rasmi za
kiutawala.
“Kwa mujibu wa
Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2012, ni asilimia 15 tu ya
watanzania ndio waliosajiliwa na kupata vyeti, hali inayowaacha wengi
pasipo kutambulika popote katika kumbukumbu rasmi za kiutawala,” amesema
Tarishi.
Ameongeza kuwa
usajili ya vifo ndio uko katika hali mbaya zaidi ambapo ni matukio
machache ya vifo yanayoandikishwa na sababu za vifo hivyo hazibainishwi
kwa usahihi au hazibainishwi kabisa hali inayosababisha ugumu katika
kutekeleza majuku kwa upande wa sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ambaye
ofisi yake ni mdau muhimu wa mfumo huu, amesema lengo la mkakati huu ni
kuanzisha mfumo wa Usajili wa Raia ambao unakidhi vigezo vya kimataifa
ambao ni wa kudumu na unaofikia watu wote katika kusajili matukio muhimu
ya binadamu na kuzalisha takwimu za matukio hayo katika namna ambayo ni
endelevu na ya kuaminika.
Dkt. Chuwa
amesema mfumo huu wa Usajili wa Raia ukikamilika utasaidia kupata huduma
zote za usajili katika sehemu moja kwa vituo vyote vya usajili nchini.
Nae Kaimu Afisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) Emmy
Hudson amesema mfumo uliopo sasa uko mbali na wananchi walio wengi hasa
wa maeneo ya vijijini kwasababu ngazi ya chini ya usajili ni ofisi ya
Katibu Tawala wa Wilaya.
Changamoto hii
na nyingine inasababisha huduma hii ya usajili kutofika kwa urahisi kwa
wananchi walio wengi hali ambayo inaleta uhitaji wa mabadiliko ambayo
ili tufanikiwe, RITA inahitaji peke yake haitamudu kuzikabili changamoto
za mfumo pasipo kuhusisha wadau mbalimbali katika kuboresha mfumo huu.
Usajili wa Raia
ulianzishwa na sheria ya kikoloni mnamo mwaka 1917. Kwa mujibu wa sheria
hiyo usajili ulikuwa ni lazima kwa wakazi wa Tanganyika na baada ya
uhuru, sheria hii ilirithiwa ambapo licha ya mabadiliko kadhaa ambayo
yamekuwa yakifanyika bado wananchi wamekuwa na kasumba ya kutokuona
umuhimu wa Usajili wa Raia nchini.chanzo Fullshangwe
No comments:
Post a Comment