HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MOTO WAUNGUZA SEHEMU YA MLIMA MERU
Moto mkubwa umezuka mwishoni mwa
wiki hii na kuunguza sehemu ya Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya
Arusha. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha moto huo ni vitendo
haramu vya urinaji wa asali ndani ya msitu wa hifadhi hiyo.
Wananchi wapatao 200 kutoka vijiji
jirani vya Olosinoni na Kisimiri Juu wakishirikiana na TANAPA
wamefanikiwa kuudhibiti moto huo ili usiweze kuleta madhara makubwa kwa
binadamu hususan wageni wanaotembelea hifadhi kwa lengo la kupanda Mlima
Meru.
Hadi sasa hakuna wageni
waliodhurika na moto huo na tahadhari zote zimechukuliwa ili kudhibiti
madhara zaidi kwa binadamu na shughuli za utalii ndani ya hifadhi.
Shirika la Hifadhi za Taifa
linaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya vitendo vya kuingia ndani
ya hifadhi bila kibali kwa shughuli ambazo zinaweza kuwa chanzo cha
kuzuka kwa mioto hii ambayo husababisha uharibifu wa mazingira pamoja na
kuharibu vyanzo vya maji.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa
moto huo unadhibitiwa kwa haraka, TANAPA imeongeza nguvu kazi ya
wananchi wakishirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuweza kuudhibiti
moto huo.
Mwisho, taarifa kamili juu madhara
yaliyosababishwa na moto huo itatolewa mara baada ya kukamilika kwa
zoezi la kuzima moto na umma utaendelea kupewa taarifa ya maendeleo ya
zoezi la uzimaji wa moto kila wakati.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
21.09.2015
dg@tanzaniaparks.com
www.tanzaniaparks.com.
chanzo-fullshagwe
No comments:
Post a Comment