Tuesday, June 9, 2015

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei 2015 umeongezeka

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kuongezeka kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Mei 2015 leo jijini Dar es salaam.Mfumuko wa Bei wa bei kwa mwezi Mei,2015 umefikia asilimia 5.3 kutoka asilimia 4.5 iliyokuwepo mwezi Aprili, 2015.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei 2015 umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.3 kutoka asilimia 4.5 ya mwezi Aprili 2015 kutokana na kuongezeka kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam amesema kuwa kuongezeka kwa mfumuko wa Bei nchini kumesababishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa za vyakula zinazotumiwa kwa wingi na kaya binafsi kwa mwezi Mei.
Amesema bidhaa za vyakula na zile zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo ni Nyama,Choroko, Maharage,samaki, nyama,unga wa mihogo.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni bei za mavazi ya wananume kwa asilimia 5.6, mavazi ya wanawake kwa asilimia 3.5, vyakula kwenye migahawa kwa asilimia 4.1 na huduma za malazi kwa asilimia 4.2.
Kuhusu Fahirisi za bei kwa maana ya namna bei zinavyopanda kutoka kipindi kimoja hadi kingine kwa mwezi Mei zimeongezeka hadi kufikia 157.86 kutoka 157.21 za mwezi Aprili 2015 kutokana kuongezeka kwa bei ya bidhaa za vyakula ambazo ni mahindi, unga wa mahindi, samaki wabichi, ndizi ,mbogamboga,viazi mviringo ,maharage na mihogo.
Kwa upande wa baidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Fahirisi za bei kwa kipimo cha mwezi Kwesigabo amesema kuwa Mafuta ya Dizeli ambayo yamechangia kwa asilimia 3.2 na na mafuta ya Petroli kwa asilimia 5.8.
Aidha,kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Mei , 2015 amesema umefikia shilingi 63 na senti 35 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 63 na senti 61 za mwezi Aprili 2015.
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Mei ,2015 na Aprili ,2015 umepungua, hii inamaanisha sasa mtu anahitaji kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua mwezi Mei"
Kwa upande wa mfumuko wa Bei wa mwezi Mei 2015 kwa nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana , Kenya umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 6.87 na kutoka 7.08 mwezi Aprili,2015 huku Uganda mfumuko wa bei kwa mwezi Mei ,2015 ukiongezeka hadi asilimia 4.90 kutoka asilimia 3.60 za mwezi zilizokuwepo mwezi Aprili, 2015.(Muro)

No comments: