Monday, January 11, 2016

"Dk. Shein na mawaziri wake wamekuwa wakibakia madarakani kwa ubabe tu"Maalim Seif Shariff

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad ametangaza rasmi kuwa yeye si makamu tena kwa sababu muda wa serikali iliyoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein kikatiba ulikwisha tangu tarehe 2 Novemba, 2015.
Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 28(2), muda halali wa rais utakuwa umefikia kikomo itakapotimu miaka mitano tangu siku ambayo kiongozi huyo alikula kiapo cha utii cha kushika wadhifa huo.
Wakati huohuo, amesema Rais John Magufuli anapaswa kuchukua uongozi wa juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, baada ya kuonekana kuwa wenzake hawana nia njema.

Maalim Seif amewaambia wahariri na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam leo kwamba Dk. Shein na mawaziri wake wamekuwa wakibakia madarakani kwa ubabe tu kwa kuwa kikatiba muda wa serikali yake ulishakwisha.

“Mimi si Makamu wa Kwanza tena. Kama kubakia basi nimebaki kwa sababu ya kuweka kinga tu ya wafuasi wetu kwa kuwa hata mwenzangu Dk. Shein ambaye pamoja na mimi ndio hatutegemei kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi, yupo lakini si rais halali kwa sababu hiyo hiyo ya kumaliza muda wake,” amesema.

Hilo la kama yeye bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais au laa, ni moja ya maswali aliyoulizwa katika mkutano huo aliouitisha kwa lengo la kuzungumzia mazungumzo yanayofanyika ya kutafuta utatuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.

“Ukweli uongozi wa Dk. Shein upo kibabebabe tu lakini ulishamaliza muda wake rasmi Novemba 2, 2015. Ndio maana tunasema kwamba kitendo cha Jecha Salim Jecha kuufuta uchaguzi pasina kuwa na mamlaka kumeifanya Zanzibar kutokuwa na serikali wala Baraza la Wawakilishi,” amesema.

Amesema yeye yupo kwa sababu na hao wenzake wanaendelea kushikilia nafasi zao, lakini kwake kuwepo ni muhimu kwa kuwa bila ya hivyo wafuasi wake watapata madhara makubwa.

Maalim Seif ametoa msimamo huo huku akiwa ameshasoma taarifa ndefu ya maandishi iliyojaa ufafanuzi wa vifungu mbalimbali vya sharia kuelezea msimamo wake na Chama cha Wananchi (CUF) kuwa Dk. Shein si rais halali na wala mawaziri si halali.

CUF ilishatangaza kuwa mawaziri wake saba katika Baraza la Mawaziri la Dk. Shein hawapo kazini tangu Novemba 12 siku ambayo kimahesabu ilitarajiwa kuwa ya mwisho kwa mamlaka ya Rais kuweza kuitisha Baraza la Wawakilishi iwapo kungetokea dharura kabla ya kuapishwa kwa baraza jipya baada ya uchaguzi.

Maalim Seif ambaye aliambatana mkutanoni hapo na wasaidizi wake katika chama, wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT), amesema mazungumzo yake na Dk. Shein pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar, yamefikia hatua ngumu kukamilika.

Amesema kwamba baada ya kuwa hawajaafikiana kutoka na kila upande kubaki na msimamo wake – yeye akishikilia kuwa uchaguzi haukufutwa kihalali kwa mujibu wa sharia, na wenzake CCM Dk. Shein na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kushikilia lazima uchaguzi urudiwe – ilitakiwa Dk. Shein aitishe kikao cha mwisho cha kusomwa taarifa ya yale waliyojadiliana.

“Dk. Shein amekuwa akikwepa kuitisha kikao hicho kwa wiki mbili ameshinda kukiitisha licha ya mimi kumuandikia barua na kumkumbusha… amekuwa akisema kwamba bado wanahitaji muda zaidi kujadiliana na wenzake,” amesema na kuamini kuwa tayari mwenendo huo ni uthibitisho kuwa tangu awali Dk. Shein hakuwa na nia njema katika kuitisha mazungumzo hayo.

Maalim Seif amesema baada ya vikao vinane kufanyika huku wananchi wakiwa wamekaa kimya wakisubiri, anadhani ni muhimu wananchi wajulishwe kinachoendelea hasa kwa kuwa haoni kama viongozi wenzake hao wa CCM wana dhamira njema ya kuondoa mgogoro.
 Katibu Mkuu wa CUF na Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hatma ya mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar
Katika taarifa aliyoisoma huku matangazo ya mkutano huo yakirushwa moja kwa moja hewani na vituo vitatu vya televisheni – Azam, ITV na Star TV – Maalim Seif amesema badala ya Dk. Shein kuitisha kikao cha kuwezesha taarifa iliyoandaliwa na sekretarieti kusomwa, zipo taarifa za uhakika kuwa CCM imeagiza Tume ya Uchaguzi ikutane Januari 14, ili kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio.

Amesema hoja ya uchaguzi wa marudio ilishindwa mapema, kwa sababu haina msingi wowote wa kisheria hasa kwa vile Tume yenyewe iliridhika kuwa uchaguzi ulikwenda vizuri mpaka hatua ya utangazaji wa matokeo.

“Hata ukisoma tovuti ya Tume ya Uchaguzi utakuta taarifa ya mwisho iliyomo ni inayosema uchaguzi katika hatua zake zote mpaka kufikia kutangaza matokeo ya kura ulikwenda vizuri… ukizingatia na taarifa za waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa, hakuna hoja ya kurudiwa uchaguzi.

“Hawa CCM kila wanakokwenda na hata katika mazungumzo wanapotakiwa wawasilishe mezani ushahidi wa uchaguzi kuvurugika wanashindwa kutoa vielelezo vyovyote. Sasa uchaguzi urudiwe kwa hoja ipi kama hakuna ushahidi kuwa uliharibika,” amesema.

Maalim Seif amesema wakati Jecha anatoa tangazo la kufuta uchaguzi, Oktoba 28, mwenyekiti huyo mwenyewe alikuwa ameshatangaza matokeo ya majimbo 33 na majimbo yaliyobaki kura zilishajumuishwa.

Amesema Oktoba 28 ilikuwa siku ya mwisho kisheria kwa Tume kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya urais na kwa hivyo “ilitakiwa Jecha aongoze kikao cha kukamilisha kazi hiyo lakini hakuonekana kazini, na makamu mwenyekiti akalazimika kuendesha kikao lakini ghafla Jecha akasikika anatoa tangazo la kufuta uchaguzi, hatua ambayo hana mamlaka nayo kisheria.”

Maalim Seif amesita kueleza CUF itakachokifanya iwapo Tume itaridhia shinikizo za uongozi wa juu wa CCM Zanzibar, kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio.

Hata hivyo amesema hali hiyo itakapotokea itakuwa ni juu ya kikao cha juu cha chama – Baraza Kuu la Uongozi – kutoa uamuzi baada ya kupata maelezo ya matokeo ya mazungumzo.

Amesema ni wakati sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kutumia mamlaka yake kuongoza juhudi za utatuzi wa mgogoro huo kwa kuwa bado anaamini kuwa ana dhamira ya kutimiza ahadi yake ya kusisitiza haja ya mgogoro huo kutatuliwa kwa amani na maridhiano.

No comments: