Mwaka mmoja uliopita ungeweza kuamini kuwa Mtanzania aliyetwaa tuzo ya
Mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani hatoitwa Ikulu na Rais
Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupongezwa?
Jibu la swali hilo ni
hapana; hasa ukizingatia kuwa wapo wanamichezo na wasanii waliotwaa tuzo
ndogo zaidi lakini wakaalikwa katika ofisi kuu hiyo ya nchi kwa ajili
ya kukutana na Rais.
Mwaka mmoja baadaye, Rais wa Tano John
Magufuli amejikita katika kushughulikia matatizo halisi ya Watanzania na
kufunga milango kwa wageni wasio na shughuli muhimu kwenda Ikulu,
gazeti hili limebaini.
Ikulu pia imekomesha tabia iliyokuwa
imezoeleka ya wageni kujazana kila siku sehemu ya mapokezi kwa ajili ya
kwenda kuomba misaada mbalimbali kwa Rais, kama ilivyokuwa imezoeleka
kwenye serikali iliyopita.
Gazeti hili lilifanikiwa kufika Ikulu
sehemu ya mapokezi na kukuta viti vikiwa vitupu tofauti na awamu
iliyopita ambapo mapokezi ya Ikulu ilikuwa ikitaka kufanana na eneo la
shughuli hiyo katika hospitali yoyote ya mkoa nchini.
Viti vilijaa hadi kufikia hatua ya wageni hao kukaa kwa kupokezana.
Wakati
leo ametimiza siku ya 80 tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, Rais
Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wachache muhimu,
hali inayoashiria kuwa Ikulu sasa ni mahala patakatifu, kama ambavyo
Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alipata kuusia katika moja ya
hotuba zake za kukumbukwa, ya Mei Mosi 1995 jijini Mbeya.
Miongoni
mwa viongozi ambao Rais Magufuli amekutana nao Ikulu tangu aingie
madarakani ni Sheikh Mkuu, Aboubakar Zuberi, Rais wa awamu ya Pili,
Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na
Kikwete.
Rais Magufuli pia alikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd kuzungumzia hali ya
mkwamo wa kisiasa inayoendelea visiwani humo.
Wengine aliokutana
nao kwa mazungumzo Ikulu hivi karibuni ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume
ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM
Taifa, Abdalah Bulembo, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Profesa Musa Jumma Assad na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Kutoalikwa Ikulu kwa Samatta ndiko kumedhihirisha
kwamba sasa milango ya kwenda kumuona Rais haiko wazi sana kama
ilivyokuwa kwenye awamu hiyo ya nne.
Rais Magufuli pia amepokea
hati za mabalozi mbali mbali wanaoiwakilisha nchi zao ambao walifika
Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Januari 7, Samatta alinyakua
tuzo hiyo ya pili kwa ubora kwa wachezaji wa Afrika, baada ya Mchezaji
Bora wa Afrika ambayo ilikwenda kwa Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon.
Tuzo hizo hutolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kama
Samatta angetwaa tuzo hiyo mwaka mmoja uliopita kwa mfano, isingekuwa
rahisi kupita wiki moja bila Mbwana Sammatta kualikwa na Rais Ikulu.
Rais mstaafu Kikwete, ambaye ni mwenyekiti wa CCM, ameshakutana na Samatta kwenye Ofisi Ndogo za chama hicho, Lumumba jijini.
Baada
ya ushindi wake, Samatta alipokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Michezo na Wasanii, Nape Nnauye, ambaye alimpa gari lake atumie kwa muda
pia.
Miongoni mwa wageni waalikwa wa mara kwa mara wa Kikwete
Ikulu ni pamoja na mwanamuziki maarufu wa zamani Ray C ambaye Desemba
10, 2012 alikwenda kumshukuru kwa kumsaidia tiba ya matumizi ya madawa
ya kulevya.
Habari ambazo Nipashe inazo, Ray C bado anaendelea
kupata tiba ya kuacha dawa za kulevya katika Hospitali ya Mwananyamala
jijini Dar es Salaam.
Diamond Platnumz amewahi kualikwa mara
kadhaa Ikulu, hata pale alipotwaa tuzo ndogo ambazo zilikabidhiwa kwenye
hata klabu za usiku nje ya nchi.
Timu ya Azam imewahi kualikwa
Ikulu baada ya kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Kagame la Afrika
Mashariki na Kati, taji ambalo Simba na Yanga zimelichukua jumla ya mara
11 katika historia.
Wachambuzi wa mambo walisema hali hiyo
inadhihirisha kwamba Rais Magufuli amejikita katika kushughulikia
matatizo ya msingi ya nchi, hasa vita dhidi ya ufisadi wa rasilimali za
taifa, upatikaji wa huduma za jamii na uimarishaji wa miundombinu.
Dalili
kwamba Ikulu sasa ni mahali patakatifu ilianza kujidhihirisha wakati wa
kuapishwa kwa Baraza la Mawaziri mwishoni mwa mwaka jana.
Mawaziri
hao waliapishwa bila mbwe mbwe wala shamra shamra kama ilivyozoeleka
kwenye awamu ya nne, wahusika wakifika Ikulu bila kuambatana na utitiri
wa ndugu na jamaa ambao chini ya Kikwete waliwalaki kwa maua na mashada
baada ya kuapishwa.
Kwenye awamu ya nne, baadhi ya wateule
walikuwa wakienda kuapishwa Ikulu na wake au waume zao, watoto, ndugu,
majirani na jamaa zao na kupata fursa ya kupiga picha na Rais mara baada
ya zoezi la kuapishwa.
Utaratibu huo umefutika baada ya Rais
Magufuli kuonekana kujikita kwenye masuala ya msingi kama kupanga safu
ya uongozi wake kwa kuwafuta kazi watendaji ambao anaona hawawezi kwenda
na kasi yake.
Aidha, punde baada ya kuingia Ikulu Novemba 5,
mwaka jana Rais Magufuli alifuta kitengo cha mapokezi ya wageni kwenye
lango kuu la Ikulu na kuagiza watendaji wa serikali katika ngazi zote
kutatua kero za wananchi mahala walipo ili kuwapunguzia usumbufu.
Kitengo
cha Lishe kilichokuwepo Ikulu wakati wa serikali ya awamu ya nne
kilivunjwa na watendaji wake kurudishwa kwenye Wizara mama walizotoka.chanzo NIPASHE
No comments:
Post a Comment