Watu watatu wamejeruhiwa baada ya mtu
aliyekuwa na bunduki kushambulia msikiti na kufyatua risasi ovyo
akiwalenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada zao katika mji wa Zurich
nchini Uswisi usiku wa kuamkia leo.
Marco Bisa, msemaji wa polisi mjini Zurich amethibitisha
kutokea hujuma hiyo na kubainisha kuwa, wawili kati ya waliofyatuliwa
risasi katika hujuma hiyo wako katika hali mbaya na kwamba wameanza
kusaka mhusika wa jinai hiyo. Inaarifiwa kuwa, aliyetekeleza jinai hiyo
ni kijana wa miaka 30 hivi, ambaye alifanikiwa kutoroka baada ya kufanya
hujuma hiyo.
Abukar Abshirow, mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo amesema
msikiti huo ambao umepakana na Kituo cha Kiislamu katika barabara ya
Eisgasse mjini Zurich, umekuwepo katika eneo hilo tangu mwaka 2012 na
kwamba hawajawahi kushuhudia kitendo cha aina hii cha chuki dhidi ya
Uislamu.
Licha ya kuwa kuna Waislamu zaidi ya laki nne nchini Uswisi, lakini
katiba ya nchi hiyo mwaka 2009 ilipiga marufuku kujengwa minara zaidi ya
minne iliyopo, katika misikiti zaidi ya 150 nchini humo.
Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka kwa kiasi
kikubwa katika nchi nyingi za Ulaya na Marekani. Hivi karibuni kuta za
msikiti mmoja wa eneo la Bron katika mji wa Lyon, nchini Ufaransa
ziliandikwa maneno ya kibaguzi na vitisho dhidi ya Waislamu.
Aidha Septemba mwaka huu, Kituo cha Kiislamu katika eneo la Fort
Pierce jimbo la Florida nchini Marekani kiliteketezwa moto na watu wenye
chuki dhidi ya Uislamu, wakati Waislamu walikuwa wanajitayarisha
kusherehekea Siku Kuu ya Idul Adh'ha.
No comments:
Post a Comment