Kwa akali watu watano wameuawa katika hujuma ya kikatili dhidi ya msikiti mmoja katika mji wa Quebec nchini Canada usiku wa kuamkia leo.
Mohamed Yangui, Rais wa Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu
mjini Quebec amesema waumini watano wa Kiislamu waliuawa walipokuwa
wakisali Sala ya Ishaa jana usiku, baada ya wavamizi kuvamia msikiti huo
na kuwamiminia risasi ovyo. Ameongeza kuwa, watu kadhaa wana majeraha
ya risasi kufutia hujuma hiyo ya kinyama.
Polisi katika eneo hilo inadai kuwa imewakamata washukiwa wawili wa hujuma hiyo na kwamba yumkini mmoja amefanikiwa kutoroka.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani shambulizi hilo dhidi
ya msikiti na kulitaja kama hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu.
Katika
ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trudeau amesema:
"Tunalaani hujuma hiyo dhidi ya pahala pa kutekelezea ibada na kimbilio
la waumini, kitendo hiki ni cha kioga na serikali inatoa mkono wa pole
kwa wahanga wa hujuma hii, na tuko tayari kutoa msaada wa aina yoyote
kwa familia za wahanga hawa."
Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kimekuwa kikilengwa
na watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu mara kwa mara. Mwezi
Juni mwaka jana wakati wa Ramadhani, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu
na Waislamu waliacha kichwa cha nguruwe katika mlango wa msikiti huo.
Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada
uliteketezwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia
Uislamu.
No comments:
Post a Comment