Tuesday, November 18, 2014

'Daesh inakiuka Uislamu na ubinaadamu


Wanamgambo wa kikundi cha Daesh wakiwaua watu bila kuwa na makosa.

Serikali ya Morocco imeitaka jamii ya kimataifa kupambana vilivyo na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Ripoti iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imesisitiza kuwa, vitendo vinavyofanywa na kundi hilo ni kinyume kabisa na misingi ya dini ya Kiislamu na ni kinyume na ubinaadamu.

Sanjari na kulaani mauaji ya Peter Kassig, aliyekuwa akishikiliwa na wanachama wa kundi hilo la kitakfiri linalofanya jinai kwa jina la Uislamu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imetaka kuzidishwa juhudi katika mapambano dhidi ya kundi hilo. 

Jana kundi hilo lilisambamba mkanda wa video ulioonyesha kuuawa Peter Kassig. Peter alitekwa nyara na kundi hilo mwaka jana nchini Syria na kupelekwa kusikojulikana. 

Kwengineko Wizara ya Ulinzi nchini Iraq, imetangaza kupinga mpango wowote wa Marekani kwa kuingia kijeshi kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa wanachama wa Daesh. Khaled al-Obeidi, Waziri wa Ulinzi wa Iraq amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo ndilo litakaloukomboa mji huo bila kuhitajia msaada wa Marekani. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo viongozi kadhaa wa Iraq, wametangaza upinzani wao juu ya mpango wa Marekani kutuma askari wake wengine kwa ajili ya kupambana na kundi hilo, wakisema kuwa hatua hiyo ni uvamizi mwengine wa Washington dhidi ya ardhi yao. 

Baadhi wamenukuliwa wakisema kuwa, operesheni za Marekani nchini Iraq dhidi ya Daesh, itakuwa na matokeo mabaya kwa taifa na watu wa Iraq.

No comments: