Tuesday, November 18, 2014

Mujuru atuhumiwa kutaka kumuua Rais Mugabe


Joice Mujuru Makamu wa Rais wa Zimbabwe

Joice Mujuru Makamu wa Rais wa Zimbabwe anakabiliwa na tuhuma za kutaka kumuua Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo. Gazeti la Sunday Mail linalochapishwa Zimbabwe limeandika katika toleo la jana kwamba, 
Bi. Joice Mujuru pamoja na wasaidizi wake wawili wanahusishwa kwenye njama za kutaka kumuua Rais Mugabe aliyeiongoza nchi hiyo tokea ilipojipatia uhuru wake mwaka 1980. 
 
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mirengo ya kisiasa ndani ya chama tawala cha ZANU PF inafanya juhudi ya kupata satua na ushawishi mkubwa kwa wanachama wa chama hicho, kabla ya kufanyika mkutano mkuu uliopangwa kuitishwa mwezi ujao. 

Bi Joice Mujuru amekuwa akishirikiana bega kwa bega na Rais Mugabe kwa kipindi kirefu, lakini katika miezi ya hivi karibuni amekuwa kwenye malumbano makali ya kisiasa na Grace Mugabe, mke wa Rais Robert Mugabe. 

Grace Mugabe amekuwa akimtuhumu Joice Mujuru Makamu wa Rais kwa kupanga njama za kumpindua Rais Mugabe. 

Vita vya kugombania madaraka ndani ya chama tawala vimeshadidi baada ya Grace Mugabe ambaye ni mkuu wa umoja wa vijana wa chama tawala, kupata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa Emmerson Mnangwaga mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama tawala cha ZANU PF. 

No comments: